Ujue ugonjwa maburg usiotibika, umefafana na Ukimwi, tofauti ni...

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 11:06 AM Nov 14 2024



Matabibu wakimhdumia mgonjwa anayesadikiwa na maradhi ya maburg.
Picha: Mtandao
Matabibu wakimhdumia mgonjwa anayesadikiwa na maradhi ya maburg.

KUNA ugonjwa mpya sasa unaoitwa maburg, unaosababishwa na virusi vyenye jina hilo, ukiwa na sifa; unaambukizwa kwa haraka sana.

Ni miongoni mwa magonjwa ya mlipuko yenye sifa za homa za virusi zinazosababisha kutokwa damu mwilini.

Hadi sasa Wizara ya Afya inatoa mafunzo kuelimisha umma, kuhusiana na magonjwa ya mlipuko aina hiyo, ikifahamisha jamii, moja ya makundi yanayopewa elimu ni waandishi wa habari, ikiaminika ni watoaji elimu kwa umma, kwa kuwa wao ni kioo cha jamii na wanafikisha ujumbe mbali.

Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Afya kwa Umma katika Idara ya Kinga, katika Wizara ya Afya, Dk. Ona Machangu, akielimisha wanahabari kuhusu ugonjwa huo, akiwapa mbinu na namna mbalimbali ya kujikinga na maambukizi yake, hali kadhalika kubainisha dalili zinavyopatikana ugonjwa huo na mengi.

Dk. Machangu anaanza kwa kuelekeza namna ugonjwa huo unavyoenea na kuambukizwa, akibainisha unaenezwa haraka kutoka kwa mtu mwenye maambukizi hadi kwa mwingine, kupitia njia nyingi, ikiwamo kugusana ngozi.

Pia anataja hali ya kugusa maji ya mwili wa mgonjwa kama vile damu, mate, matapishi, kinyesi, machozi, kamasi, jasho au mkojo.

Vilevile anataja namna ya kugusa au kuosha maiti ya mtu aliyefariki akiwa na dalili za ugonjwa wa marburg, vyombo, nguo, matandiko au godoro la mwenye maambukizi ya virusi vya marburg.

Dk. Machangua anasema, suala la kuchangia vitu vyenye ncha kali na mwenye maambukizi ya ugonjwa huo, ikiwamo kujamiiana na mtu mwenye virusi vya marburg.

Mjamzito huyo anaelezwa kuwa na uwezo wa kumwambukiza mtoto wake maradhi hayo, ilhali bado yuko tumboni au wakati anapomnyonyesha, anaweza kupata maambukizi hayo.

Aidha, inatajwa maambukizi hayo yanaweza kutokea kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, iwapo mtu atakula au kugusa mzoga au wanyama wenye virusi vya ugonjwa huo, kama vile popo, tumbili, nyani au sokwe.

Aidha ugonjwa huo unathibitishwa kuambukiza kwa njia ya hewa, kama unavyodhaniwa na wengi.

UNAFANANA NA UKIMWI

Inatajwa kwamba, licha ya kutoambukizwa kwa njia ya hewa, ugonjwa huo huwa unatajwa wasifu wake unapoangaliwa kwa kina, unatajwa maambukizi yake yanashabihiana na Ugonjwa wa Ukosefu wa Kinga Mwilini (UKIMWI).

Hiyo inafafanuliwa kwamba, kuna baadhi ya aina ya maambukizi yanafanana na jinsi yanavyopatikana maambukizi hayo ya Ukimwi.

Eneo moja linalofanana linatajwa ni katika vitu vyenye ncha kali, kuosha maiti ya mwathirika, kujamiiana, hata suala la kumnyonyesha mtoto.

Hapo ni pale mama anayeathirika humhamishia mtoto maambukizi, pale mama atakapokuwa hajaanza kutumia dawa ipasavyo.

Dk. Norman Jonas, Bingwa Mratibu Kitaifa wa Huduma za Afya ya Jamii, anawaambia wanahabari kuwa dalili zake huanza kuonekana kati ya siku mbili hadi 21, baada ya kupata maambukizi. 

Anafafanua kuwa dalili hizo, ni pamoja na mwili kuishiwa nguvu, vidonda vya koo, vipele vya ngozi, maumivu ya tumbo, kutapika.

Vilevile ni katika eneo la kutokwa na damu katika sehemu za wazi kama vile puani na kwenye matundu mengine, kutapika, pia kuharisha damu.

Dk. Jonas anasema, pale mtu anaona mojawapo kati ya dalili hizo, moja kwa moja inampa viashiria kwamba kuna dalili za ugonjwa huo hatari.

Aidha, mtaalamu huyo anabainisha kwamba ugonjwa huo hauna tiba maalumu wala chanjo, mgonjwa hutibiwa kulingana na dalili zikiambatana na ugonjwa huo.

Akafafanua uwezekano wa mgonjwa kuishi huongezeka pale mtu anapopata matibabu kwa wakati kutoka kwenye kituo cha huduma za afya.

NAMNA KUJIKINGA 

Jinsi ya kujikinga nao, inatajwa ni kuepuka kugusana na mgonjwa, kama kusalimiana na kugusana.

Hiyo inaweka tahadhari ya msingi kwamba, mara zote kwa kuepuka ama kugusa au kuosha maiti ya mtu aliyefariki, akiwa na dalili za ugonjwa wa maburg.

Pia, wataalamu wanashauriwa kunawa mikono kila mara kwa maji tiririka, huku wakiacha kuchangia vitu vyenye ncha kali, vikiwamo nyembe na sindano.

Wizara ya Afya inatoa angalizo kwa wananchi ama kutomtenga au kumnyanyapaa mtu yeyote aliyeruhusiwa kutoka karantini, kwa kuwa mtu anapopewa ruhusa hiyo, ni tayari ameshathibitishwa na wataalamu kuwa hana ugonjwa huo.

Ilibainika kwamba, suala la kumnyanyapaa mhusika, linaangukia katika tafsiri ya ubaguzi kiafya. 

Mnamo Oktoba 26, mwaka huu, Wizara ya Afya ikaendeleza utoaji elimu  dhidi ya magonjwa ya mlipuko nchini, kwa viongozi wa dini.

Hiyo ni hatua inayogusa utoaji elimu kwa viongozi, wafikishe elimu na ufahamu kwa waumini na jamii kwa ujumla, kupitia ngazi ya viongozi hao.

Naibu Waziri wa Afya, Godwin Mollel, ambaye kitaalamu pia ni daktari wa tiba, anasema Tanzania inapoukamata ulimwengu wa kiroho kwa binadamu, itaibuka ngazi ya juu, bila ya kupata magonjwa hayo kupitia viongozi husika.

Dk. Mollel anaitaja sayansi zote na wanasanyansi wake duniani, waangukia mtazamo anaoutaja kuwa: “Dini ni jicho muhimu kutuonesha tupite wapi tusipite wapi, ili nchi iwe salama, nyinyi viongozi wa dini mmeshika ulimwengu...kupitia elimu hii naomba mkawe sikivu na nchi yetu ibaki salama.” 

Miongoni mwa nchi za Kiafrika zinazotajwa kuwa na mlipuko ya maradhi hayo zinatajwa Guinea ya Ikweta, majirani zake Cameroon ma katika ukanda wa Afrika Mashariki, zimo Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), na Uganda.