MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imebaini kuna ongezeko la wanawake wengi kununua na kutumia dawa za kulevya aina ya skanka ambayo ni aina ya bangi.
Wamesema kundi hilo hutumia dawa hizo kwa sababu mbalimbali zikiwamo migogoro ya kimapenzi, msongo wa mawazo na wengine kuzitumia kwa starehe.
Kamishna Jenerali wa Malamka hiyo, Aretas Lyimo, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akiwasilisha taarifa ya operesheni iliyofanyika nchi nzima kati ya mwezi Oktoba na Novemba, mwaka huu.
Lyimo alisema skanka ni aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu na husababisha madhara zaidi kiafya.
“Wauzaji waliokamatwa walipohojiwa soko lao kubwa, walieleza kuwa wanunuzi wengi ni wanawake hata hivyo utafiti uliofanyika kwa baadhi ya saluni na kundi la wadada watumiaji, walidai kuwa skanka inawapunguzia mawazo na wakati mwingine huwasababishia uraibu.
“Hutumia kwa sababu ya msongo wa mawazo kutokana na hali ngumu ya maisha pamoja na usaliti katika mapenzi.
“Kwa wanawake walioshindwa kumudu hali hiyo wamejikuta wakitumia dawa hiyo kama suluhisho na hii ni baada ya heroin kupungua kwa kiasi kikubwa nchini kutokana na matokeo ya udhibiti,” alisema.
Kamishna Lyimo alisema heroin kwa sasa imepungua na inayopatikana imebainika kuchanganywa na vitu vingine kama unga wa dona pamoja na masega, hivyo hupoteza uwezo kwa watumiaji na kuwalazimu wengi wao kuingia katika matumizi ya skanka.
“Pamoja na udhibiti huo lakini bado watumiaji wameanza kutumia dawa tiba zenye asili ya kulevya ambazo hutumika kwa wagonjwa wa saratani na wale wenye maumivu makali kama mbadala wa dawa za kulevya.
“Hata hivyo, serikali inaweka utaratibu maalum wa kudhibiti dawa hizo kutouzwa katika kila duka la dawa lengo ni kupunguza ongezeko la waraibu.
Kamishna Lyimo alisema katika operesheni hizo walikamata kilogramu 1,066.105 za dawa za kulevya, mililita 447 za dawa tiba zenye asili ya kulevya na kuteketeza jumla ya ekari 157,4 za mashamba ya bangi na lita 19,804 za kemikali bashirifu pamoja na kuwakamata watuhumiwa 58.
Alisema kati ya dawa hizo, kilogramu 687.32 za skanka na kilogramu moja ya hashishi zilikamatwa eneo la Goba, Dar es Salaam, zikiwa zimefichwa ndani ya nyumba ya mtuhumiwa.
Alisema hashishi hutengenezwa kwa mchanganyiko wa maua na mafuta ya mbegu za bangi na inapovutwa huzalisha kemikali hatari zinazosababisha magonjwa ya akili kwa haraka.
“Katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere mamlaka imekamata mililita 120 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Codein zikiwa zinasafirishwa kwenda nje ya nchi pamoja na mililita 327 zilizokutwa nyumbani kwa mtuhumiwa eneo la Tabata Kinyerezi, Dar es Salaam.
“Dawa hizo ziliingizwa nchini kinyume na taratibu zikiwa zimeweka chapa bandia ya dawa za kuogeshea mbwa na paka ili kuepuka kubainika,” alisema Kamishna Lyimo.
Alisema jijini Dodoma wamekamatwa watuhumiwa wawili, Suleiman Mbaruku (52) maarufu Nyandana na Kimwaga Lazaro (37) wote wakazi wa Mtaa wa Kinyali, Kata ya Viwandani, ambao wamekamatwa na jumla ya gramu 393 za heroin.
“Nyanda, ni kinara wa biashara ya dawa za kulevya mkoani humo na alikuwa akifuatiliwa kwa muda mrefu, hata hivyo waraibu wengi walioko katika Kituo cha ltega kinachohudumia watu wenye uraibu, yeye ndiye kawaharibu na dawa hizo,” alisema Kamisha Lyimo.
Alisema kupitia operesheni za kanda wamekamata kilo 303.553 za bangi, gramu 103.8 za heroin na kilo 63 za mirungi katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema mamlaka imebaini baadhi ya wafanyabiashara wa shisha huchanganya dawa za kulevya pasipo wateja kufahamu lengo likiwa ni kuimarisha biashara zao.
“Utafiti na sampuli zilizochukuliwa umeonesha baadhi ya wafanyabiashara kukiuka sheria za nchi. Tunatarajia kuiweka shisha katika udhibiti,” alisema Kamishna Lyimo.
Katika hatua nyingine, Kamishna huyo alitaja changamoto zinazowakabili katika utendaji kazi ni uwapo wa vipenyo vingi katika mipaka ya nchi hivyo watu wasiowaadilifu hutumia kama njia ya kuvusha dawa za kulevya.
“Rushwa na mfanyabiashara wa dawa za kulevya ni kitu kimoja. Tumeingia makubaliano na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU) ili tuweze kushirikiana kudhibiti hali hii.
“Unakuta shamba la bangi au mirungi katika eneo ambalo kuna viongozi wa serikali, unajiuliza hawakuliona hili? Lakini pia katika mipaka inavukaje kwa magari ya mizigo wakati wapo watu wa ukaguzi,” alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED