Mawakili wa utetezi kesi ya wanandoa wakwaa kisiki Kisutu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:29 PM Nov 13 2024
Wanandoa  Bharat Nathwan (57), Sangita Bharat (54).
Picha: Mtandao
Wanandoa Bharat Nathwan (57), Sangita Bharat (54).

HAKIMU Mkazi Mkuu Aaron Lyamuya wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam amekataa kujitoa kusikiliza kesi ya tuhuma za kujeruhi inayomkabili Bharat Nathwan (57), Sangita Bharat (54) kwa madai kuwa hakuna sababu ya msingi iliyotolewa na upande wa utetezi.

Aidha, amesema amekuwa akiwakubalia watu kujitoa katika kesi zao ambao hawana mawakili mahakamani kwa sababu hawana uelewa wa sheria, lakini sababu iliyotolewa na Wakili Mkongwe wa sheria, Gabriel Mnyele haina mashiko ya yeye kujitoa. 

Hakimu Lyamuya alitoa uamuzi huo mdogo jana, baada ya mawakili wa washtakiwa hao Mnyele na Edward Chuwa kuomba ajitoe kwa sababu amewakataliwa pingamizi zao mbili wakati kesi hiyo inasikilizwa kwa mashahidi wa upande wa Jamhuri. 

"Katika hoja hizi zilikuwa za upande mmoja tu za Wakili Mnyele hili suala sio geni la kutaka hakimu au jaji kujitoa kwenye kesi ni mambo ya kawaida, lakini unatakiwa utoe sababu za msingi za kisheria na sio hisia tu," 

"Ikiwa sababu zitaonesha kwamba kuna haki haitotendekeka au upendeleo wowote au unarafiki au ndugu kwenye kesi basi unajitoa, katika maelezo ya Mnyele nilitarajia haya anayajua angeeleza sababu za msingi,"alisema Hakimu Lyamuya

 "Ingekuwa hoja hii imeletwa na mtu wa mtaani asiyejua sheria ningefikiria kujitoa lakini kwa mtu senior kama Mnyele siwezi kujitoa kwa kuwa hakuna sababu za msingi,"alisema 

Aliendelea kueleza kwamba, kuwakatalia pingamizi sio sababu wao walitakiwa kutafuta wapi walikosea sio kuhamaki hawafanyi uamuzi kwa mahesabu, kwa sababu nimewakatalia mara mbili basi ndiyo atoe uamuzi tofauti hiyo haiwezekani.

 "Ningekuwa nafanya hivyo kwa kutoa uamuzi kwa namba ningekuwa nafanya sijakaa kwenye kiti hiki," 

"Kesi nitaendelea nayo mimi hadi mwisho sijitoi kwa sababu hakuna sababu ya msingi iliyotolewa na Wakili Mkongwe Mnyele, kama mtakuwa hamjaridhika hadi mwisho mtakata rufaa kwamba nilikataa kujitoa ila sio sasa,"alisema 

Hakimu baada ya kumaliza kutoa uamuzi wake, Wakili Chuwa akaanza kuzungumza kile ambacho alizungumza Mnyele ndipo akamuhoji kwamba anataka afanye nini wakati tayari ameshatoa uamuzi, anapanga tarehe ya kuendelea kusikilizwa. 

Baada ya hakimu kusema hayo, Wakili Chuwa alimgekia hakimu na kumueleza kwamba kwa nini anazungumza kwa jazba," Khe mimi sijaongea jazba nimekueleza kwamba napanga tarehe nyingine ya kusikiliza hiyo jazba inatoka wapi wakati tayari nimeshatoa uamuzi", 

"Kwanza hata tai haujavaa hauko proper, halafu unazungumza vitu ambavyo havipo hapa kuna wanafunzi wa sheria watajifunza nini kutoka kwako?, haya nipange tarehe ngapi kesi,"alisema 

Kesi imeahirishwa hadi Desemba 3,2024 saa tano asubuhi, Shahidi namba tano. Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (Assistant Inspector) Calvin (36) ataendela kutoa ushsiwake. 

Awali, shahidi huyo, hakuweza kumaliza kutoa ushahidi wake, kutokana na ubishani uliyotokea kwa Wakili Mnyele kudai kuwa hawezi kuelezea kile alichokiona kwenye CCTV Kamera kwa sababu ni suala la kieletroniki. 

Wanandoa hao ambao ni raia wa Tanzania asili ya kihindi wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashtaka manne waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria. 

Ilidaiwa kuwa Nathwan anatuhumiwa Julai 21,2023 akiwa eneo la mtaa wa Mrima-Kisutu, jingo la Lohana, ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kinyume cha sheria alimsababishia madhara makubwa Kiran Lalit kwa kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo la saruji iliyochanganywa.