KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI, imesema inaridhishwa na kazi inayofanywa na Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), huku wakielekeza kuharakisha mazungumzo na wawekezaji mbalimbali ili miradi 84 iliyo katika hatua mbalimbali ianze utekelezaji wake.
Kamati hiyo imetoa maelekezo hayo Novemba 11,2024 wakati wa mafunzo kuhusu shughuli mbalimbali za kituo kwa lengo la kuwajengea uelewa wa miradi mbalimbali ambayo wameitambua kama muhimu kwa uwekezaji kitaifa hadi serikali za mitaa.
Mjumbe wa kamati hiyo na Mbunge wa Jimbo la Hai (CCM), Saashisha Mafuwe amesema maamuzi yanachukua muda mrefu kwenye mazungumzo na kwamba ni muhimu PPPC ikatathimini maeneo yenye urasimu na kuja na mkakati, ikiwamo kuwa na eneo moja la kukusanya miradi ili kupunguza urasimu, pia kuwe na maonyesho ya kutangaza kazi zetu ili kupata wawekezaji.
“Kwenye ofisi yako (PPPC) ainisha maeneo yenye urasimu kama hizi sheria za manunuzi, usahindani ili viondolewe kazi iende kwa kasai, ikiwamo vivutio vya kikodi. Vitu vyote hivi vikusanye wasilisha kwetu wabunge na upeleke serikalini ili viondolewe.
“Ukitengeneza mazingira mazuri utapata wawekezaji humu ndani, wenzetu Kenya wamepata wawekezaji kwenye barabara na wanakusanya fedha, tukishapata wawekezaji maana yake miradi yetu ya barabara itakamilika na tutakusanya fedha.”
Aidha, amesema utayari wa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye PPP ni mkubwa na kwamba ni muhimu wakaharakisha miradi mingi itoke kwenye makaratasi kwenda kwenye utekelezaji na matokeo kuonekana, na kwamba itawezekana ikiwa kwenye kila halmasahauri wanakuwa na mtu maalum kwa ajili ya PPP.
“Mfano kuna timu za mipira zinaendeshwa na halmashauri, zinatakiwa zipate wawekezaji zitoke zisimamiwe taifa tutaona tija, tofauti na sasa zinavyoendeshwa zinatia hasara.Tuweke utaratibu mzuri wa kukusanya miradi halmashauri ikiwamo kuondoa urasimu wa mamlaka kukizana.
Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Salome Makamba amesema awali alikuwa anachanganya kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na PPPC lakini namna walivyojipambanua kwa nguvu kubwa na matokeo yanaonekana jambo ambalo linahalalisha kwanini PPP waendelee kuwepo.
“Namtia moyo David Kafulila (Mkurugenzi PPPC), kazi unayofanya inaonekana na matunda tunayaona, wabunge tunachotaka ni tija kwa nchi yetu.Ila bado naona tuna miradi ya kimkakati ikiwamo wa gesi asilia ambao una zaidi ya miaka 11 na kila tukiuliza serikalini wanajibu mazungumzo yanaendelea, mmezungumza hadi mradi umepitwa na wakati kiasi kwamba tukienda sokoni sasa thamani ya gesi si ile ya wakati ule,”amesema.
Awali, Mkurugenzi wa PPPC, David Kafulila amesema safari ya PPP ilianza mwaka 2009 ilitukwa sera, baadaye sheria 2010 na kutukwa kanuni 2011 kwa ajili ya kutekeleza , lengo ni kutoa fursa za ubia kati ya mamlaka za serikali na sekta binafsi.
“Kumekuwa na changamoto ni mamlaka za serikali kutengeneza mikataba na wawekezaji, nyingine ni uelewa wa mamlaka za serikala na hasa masuala ya ubia, historia isiyoridhisha ya miakata iliyotia saini huko nyuma na hivyo kujenga picha hasi kwa uwekezaji wa PPP,”amesema.
Amesema PPPC kilianzishwa kisheria namba 103 ya mwaka 2014 lakini kwasababu mbalimbali hakikuanza kazi na kuna wakati majukumuya ubia yalifanywa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu baadaye Wizara ya Fedha jambo ambalo ni sahihi kwa kuwa ndio kipimo cha dunia.
“Kimsingi Rais Samia alitekeleza sheria iliyopitishwa na bunge, na mwaka huu ndio tumeranza rasmi mchakato wa miradi. Kazi kubwa ya PPPC ni kutambua mikataba kuhakikisha serikali inaingia mikataba yenye thamani, nyaraka zote zinapituwa na kituo ili kuisaidia mamlaka zoete za serikali kuhusiana na uamuzi wa uwekezaji.
Kafulila amesema lengo ni kuhakikisha serikali haiingii mikataba mibovu, na kwamba hakuna mkataba utakaopitia PPPCukawa mbovu na kwamba zipo mamlaka zinaweza kuingia mikataba kwa sheria zao lakini hautahusika na sheria ya ubia.
Aidha,amesema miradi midogo imeruhusiwa kwa mamlaka kupitisha iko ngazi ya halmashauri kwa miradi midogo ya chini ya Dola mil 20, na kwamba mwekezaji anaweza kuja kutaka kuwekeza kwenye mradi ambao serikali ingetumia fedha nyingi, na kwa kutekeleza wananchi watapata huduma na serikali mapato.
“Tuko makini sana, tunaangalia mambo mengi sana ili kuhakikisha serikali inanufaika, mwekezaji ananufaika na wananchi wanapata huduma.PPP inasaidia serikali kutekeleza miradi kwa mtaji wa umma na wananchi kupata huduma muhimu za kijamii. Ni jukumu la serikali kufanya miradi, ila unatumia mitaji ya umma kutekeleza miradi. Sheria yetu imeweka vivutio vya kikodi ili kupata miradi mingi,”amesema Kafulila.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED