Kafikisha tiba 96% kusonga sifuri, ‘mbishi’ anayejitokeza unyanyapaa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:42 AM Nov 14 2024

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipomwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika mdahalo kitaifa unaohusu Ukimwi, Septemba mwaka jana.
Picha:Mtandao
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipomwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika mdahalo kitaifa unaohusu Ukimwi, Septemba mwaka jana.

ILIKUWA mwezi Juni 2021, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akiwa na miezi mitatu tu madarakani, akatamka katika kikao cha Umoja wa Mataifa kilichofanyika kwa njia ya mtandao, kwamba Tanzania inaunga mkono mshikamano wa kimataifa kutokomeza Ukimwi.

Ni mkutano wa siku tatu uliotathmini maendeleo yaliyofikiwa duniani katika kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo, tangu kufanyika mkutano kama huo mwaka 2016. 

Rais Dk. Samia akasema: “Ukimwi siyo tena hukumu ya kifo nchini Tanzania kama ilivyokuwa miaka 38 iliyopita. Vifo vitokanavyo na Ukimwi vimepungua kutoka elfu 64 kwa mwaka 2010 hadi elfu 32 mwaka 2020. 

“Maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yamepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2010, hadi asilimia saba mwaka 2020.”

Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa wakati huo, Amina J. Mohammed, akachangia hoja kwamba hatua dhidi ya Ukimwi inafanikiwa, pale penye utashi kisiasa, mshikamano na sayansi na hata kuwezesha kuutokomeza ifikapo mwaka 2030.

Ni mkutano uliopitisha azimio la kisiasa kuongeza juhudi za kutokomeza Ukimwi duniani, Rais Dk. Samia akihakikisha inaunga mkono mshikamano huo wa kimataifa katika vita hivyo.

2022 NA UNYANYAPAA 

Akihutubia Siku ya Ukimwi Duniani, katika maadhimisho kitaifa yaliyofanyika mkoani Lindi katika Uwanja wa Michezo Ilulu, Manispaa ya Lindi, Rais Dk. Samia akasema jitihada kubwa zinafanywa na serikali yake, kushirikiana na washirika wa maendeleo.

Hata hivyo akakiri, kuwapo changamoto ya unyanyapaa kwa waathirika kwamba halijafanyiwa kazi vizuri, akidokeza kuwapo mkakati wa tatu wakati huo, unaolenga kusaidia kuondoa unyanyapaa.

“Kuna jambo ambalo hatujalifanyia vizuri, nalo ni suala zima la unyanyapaa. Bado lipo na ndio maana tumekuja na mikakati hiyo ili kuondosha huo unyanyapaa.

“Safari tunayokwenda katika mkakati unaofuata ni kufikia malengo ya ‘sifuri tatu’ ifikapo mwaka 2030, lakini kwa mpango wetu 2026 ni kutokomeza Ukimwi kuwa sifuri na maambukizi mapya ya VVU, sifuri ya kifo na sifuri ya unyanyapaa.”

Katika vita hivyo, Rais akasisitiza utekelezaji wa mpango huo ni vyema kushirikiana jamii zote na lisikabki kuwa la Wizara ya Afya pekee.

Hapo akaielekeza wizara hiyo, pia Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), kwa kushirikiana na sekta zote wadau, kuhusu mapambano hayo kuwekewa mkazo kwenye jitihada na mikakati ya kuzuia maambukizi mapya, upimaji VVU na matumizi ya dawa za kinga - ARV, ili kutokomeza vifo vyake.

KILICHOJIRI 2023

Ulikuwa mwaka uliofuata baada ya tukio la Lindi mnamo Septemba mwaka 2023, kukawapo, tukio la ‘Mdahalo wa Kitaifa Kuimarisha Ubia Baina ya Serikali, Wadau na Jamii kwa Uendelevu wa Mafanikio ya Mwitikio wa Ukimwi nchini.

Kwenye tukio hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Dodoma, mgeni rasmi mwalikiwa Rais Dk. Samia, aliwakilishwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Hapo akasema kwamba malengo ya mwaka 2025 ni kwamba: “Leo hii (Septemba, 2023) tayari asilimia 96 ya watu wanaoishi na mambukizi ya VVU wanajua hali zao.’

Majaliwa akaendelea: “Asilimia 98 ya wanaojua hali zao wapo kwenye tiba ya ARV na kati yao, asilimia 97 wameweza kufubaza wingi wa virusi kwenye damu.  

“Jukumu kubwa la taifa tulilo nalo ni kulinda na kuyaendeleza mafanikio haya kwa nguvu za pamoja na umoja hadi tufikie malengo ya sifuri tatu ifikapo mwaka 2030.”

Majaliwa akafafanua kuwa serikali itaendelea kuimarisha uwekezaji na mifumo endelevu ya upatikanaji rasilimali fedha, kwa ajili ya afua mbalimbali za Ukimwi, ikiwa ni pamoja na Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (Aids Trust Fund) na mipango katika ngazi ya halmashauri na taifa kwa ujumla, ili malengo ya  kutokomeza ugonjwa yafikiwe.

Waziri Mkuu akawahakikishia wadau hao akiwamo Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na VVU (NACOPHA), kuyafanyia maoni kazi yao ya mdahalo, akinena: “Suala la ubia halikwepeki tunatambua umuhimu wa ushirikiano na tutalitekeleza kwa maslahi mapana ya Watanzania.

“Serikali itazidi kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali waliopo nchini na nje ya nchi hasa katika uwekezaji, kutoa elimu, vifaa tiba, wataalamu, maboresho ya sera na miongozo mbalimbali ya masuala ya UKIMWI.

“Tumewasikia wadau na pia tumepata maoni kutoka kwa ndugu zetu WAVIU. Maoni haya yatasaidia kuboresha mikakati ya serikali kuhakikisha tunafikia malengo.”

Anasema, licha ya utafiti kuonyesha kupungua unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya VVU nchini, bado matendo hayo na ukatili wa kijinsia yanaendelea kuwa kikwazo cha kuzifikia na kuzitumia huduma za VVU kwenye jamii, shuleni, vyuoni na sehemu za kazi.

Mwenyekiti wa NACOPHA, Leticia Moris, anasema baraza hilo limetimiza miaka 21 tangu kuanzishwa, akiishukuru serikali na wadau wa maendeleo kuendelea kuhakikisha huduma mbalimbali, zikiwamo dawa za kufubaza VVU zinaendelea kupatikana.

OKTOBA 2024

Akiwa ziarani Geita mwezi uliopita, Rais Dk. Samia akahutubia mkutano, akinena: “Kwa upande wa VVU, nchi yetu imekuwa ikipambana na janga hilo zaidi ya miongo minne sasa.

“Kwa mujibu wa utafiti wa hali ya Ukimwi nchini, kiwango cha maambukizi ya VVU kwa watu wazima, yaani vijana kuanzia miaka 15 kwenda juu ni asilimia 4.4 kwa mwaka 2022/2023.”