KIPIGO cha mabao 4-0 ilichokipata Simba, Mei 15, 2021, kwenye mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs, ndiyo sababu iliyoifanya timu hiyo kuomba mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Pamba Jiji FC ulioahirishwa na Bodi ya Ligi urudishwe.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zimesema kuwa uongozi wa Simba pamoja na Kocha Mkuu, Fadlu Davids, walikaa na kushauriana kuwa mchezo huo ulioahirishwa kwa ajili ya kutoa fursa kujiandaa vizuri na mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravo do Maquis ya Angola, unaotarajiwa kuchezwa, Novemba 26, mwaka huu, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, na kuamua urudishwe ili kuwafanya wachezaji wasikae muda mrefu bila kucheza.
Viongozi wa Simba walikumbuka kilichowapata kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Kaizer Chiefs ambapo waliomba waahirishiwe baadhi ya michezo yao ya Ligi Kuu na kukaa wiki mbili bila mchezo wowote kitu ambacho kilichangia kufungwa idadi hiyo ya mabao katika mchezo wa kwanza uliochezwa Afrika Kusini, kabla ya kushinda mabao 3-0 mchezo wa marudiano, Mei 22, 2021, lakini hayakuweza kuifanya kutoaga mashindano hayo na kushindwa kwenda hatua ya nusu fainali, ikitolewa kwa jumla ya mabao 4-3.
Bodi ya Ligi iliahirisha michezo ya Ligi Kuu kati ya Simba dhidi ya Pamba Jiji, na Yanga dhidi ya Fountain Gate iliyokuwa ichezwe Novemba 21, mwaka huu, ili kuzipa muda timu hizo kujiandaa na mechi za kimataifa.
Yanga inajiandaa na mechi dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan, Novemba 26, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
"Simba tuna uzoefu na michezo hii ya kimataifa, kama huna utimamu wa mwili na ukikaa bila kucheza kwa wiki mbili au zaidi itakupa tabu, ndiyo maana viongozi wetu na kocha Fadlu waliiomba Bodi ya Ligi mechi yao irudishwe kwenye ratiba ya awali," kilisema chanzo ndani ya Simba.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema mchezo huo utapigwa Ijumaa ya Novemba 22, Uwanja wa CCM Kirumba, akiwataka mashabiki wengi kujitokeza kwa wingi.
Alisema mchezo huo, pamoja na kwamba ni wa Ligi Kuu, lakini utakuwa ni kama wa kujipima nguvu kuelekea katika mechi dhidi ya timu hiyo ya Angola.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda, alisema waliitoa michezo hiyo miwili na kusema wataipangia tarehe nyingine ili kuzipa muda timu hizo kujiandaa na michezo wa kimataifa, huku baadhi ya wachezaji wao wakiwa kwenye timu za taifa, lakini mchezo dhidi ya Simba wameupanga uchezwe Novemba 22, huku wa Yanga ukitarajiwa kupangiwa tarehe nyingine.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED