MVUA ya kwanza ni ya kupandia. Huu ni msemo wa miaka mingi ambao unawakumbusha wakulima kujiandaa katika shughuli zao za kila siku na pia kuhakikisha wanautumia msimu kwa umakini ili kupata mazao ya kutosha.
Kama ilivyo ada, hivi sasa mvua imeanza kunyesha katika maeneo mengi nchini na huu ndio msimu wa wakulima katika sehemu hizo kuanza kulima mashamba yao na kupanda mazao ya chakula kama mahindi. Ni msimu ambao ni muhimu katika kuelekea kupata mazao mengi kwa ajili ya chakula na mengine kuuza ili kujikwamua kiuchumi.
Kutokana na ukweli huo, wakulima wanasisitizwa kuanza kutumia mvua inayonyesha kupanda mazao katika mashamba waliyoyaandaa kwa ajili ya kilimo. Kwa wale ambao huchelewa au kuzembea kuandaa mashamba, hujikuta katika mazingira magumu kwa kuwa watapata mavuno kidogo au kuambulia patupu na kukutana na msemo kwamba majuto ni mjukuu.
Ni msimu ambao ni wa muhimu kwa wakulima ndiyo maana hata serikali imekuwa ikisisitiza kwa viongozi wa mikoa na wilaya kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo unakuwa wa kutosha na wa bei iliyowekwa.
Msisitizo huo wa serikali unatokana na ukweli kwamba usalama na upatikanaji wa chakula ni miongoni mwa sababu za kustawi kwa amani na utulivu. Pia serikali imekuwa ikisisitiza hivyo kwa sababu sekta ya kilimo inaajiri Watanzania wengine, hivyo ni chanzo cha kuwawezesha watu wengi kujipatia kipato kwa kuuza mazao yao baada ya kuvuna kisha kijikomboa na umaskini wa hali na wa kipato.
Kutokana na ukweli huo, wakati wakulima, pamoja na wengine walioko katika ajira rasmi ambao hujishghulisha na kilimo biashara, wanahamasika kuhakikisha wanatimiza wajibu wao, ni vyema upatikanaji wa pembejeo kwa maana ya mbolea ya kupandia na kukuzia na viuatilifu ukawa wa kutosha. Wakuu wa wilaya na mikoa wanapaswa kuhakikisha kuwasimamia maofisa kilimo na wakurugenzi wa halmashauri ugawaji wa pembejeo hasa mbolea ufanyike bila kasoro yoyote.
Kama wahenga wasemavyo katika msafara wa mamba kenge wamo, wakati msimu wa kilimo unapowadia, kuna wajanja hujitokeza na kuingilia mchakato wa mauzo ya mbolea kwa bei ya juu tofauti na ile iliyopangwa na serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA). Watu hao hununua mbolea kwa bei elekezi kisha kuilangua kwa bei ya juu kwa wakulima, hivyo kuwafanya wapate uchungu wa kuingia gharama kubwa.
Watu hao ambao baadhi yao hijivika kofia ya mawakala, hishirikiana na baadhi ya maofisa wa serikali hasa watendaji wa idara ya kilimo katika halmashauri kulangua mbolea na kuificha na baadaye kuiuza kwa bei kubwa au ya magendo.
Kwa mantiki hiyo, ni wakati sasa wa wakuu wa mikoa na wilaya kuamka na kuanza kusimamia kikamilifu upatikanaji wa mbolea ili wakulima wasihangaike kuipata au kuuziwa kwa bei ya magendo tofauti na ile iliyowekwa. Aidha, kusimamia ugawaji pekee hakutoshi bali kinachotakiwa pia ni kuwatambua mawakala katika maeneo husika na kuhakikisha wanauza kwa kufuata taratibu.
Katika misimu kadhaa iliyopita, suala la kukosekana kwa mbolea au upungufu tofauti na kiasi kinachotakiwa lilijitokeza sana kwenye baadhi ya maeneo, hivyo kusababisha wakulima kukosa pembejeo hizo na kupata mazao kwa kiwango kidogo. Hali hiyo ilisababisha wale wenye uwezo kumudu kununua mbolea kwa gharama kubwa na wale wasio na uwezo kushindwa kumudu.
Suala la mbolea ni nyeti sana katika msimu huu wa kilimo, hivyo serikali kupitia taasisi zake zinazosimamia upatikanaji na usambazaji wa bidhaa hiyo, ihakikishe hakuna malalamiko kama misimu iliyopita ili kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa wingi na nchi kuwa na chakula cha kutosha.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED