Kila la heri Simba, Yanga shindeni mechi zenu za kwanza nyumbani

Nipashe
Published at 07:01 PM Nov 25 2024
Uwanja
Mtandao
Uwanja

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, Yanga na Simba, kesho na keshokutwa watashuka dimbani katika michezo yao ya kwanza hatua za makundi ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga, kesho watashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kucheza na mabingwa wa Sudan, Al Hilal Omdurman, katika mchezo wa raundi ya kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.

Kesho kutwa, Simba nayo itakuwa kwenye uwanja huo huo kucheza mchezo wake wa kwanza, hatua ya makundi, Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravo do Maquis ya Angola.

Katika hatua hii, lengo namba moja kwa timu zote ni kutinga hatua ya robo fainali, hivyo kama zinataka kufika huko zinapaswa kushinda michezo yao hiyo ya kwanza ili kuongeza ari ya upambanaji.

Kwa bahati nzuri timu zote zinacheza nyumbani, hivyo tunatarajiwa zitatumia vema faida ya kucheza nyumbani ili kupata ushindi, ikiwezekana mnono.

Tunajua hatua hizi za makundi timu nyingi kufanya kila mbinu kuhakikisha zinashinda kwenye viwanja vyao vya nyumbani na zikienda ugenini hulazimisha angalau sare. Hivyo ili kufika robo fainali kwenye michuano hii Simba na Yanga zinatakiwa ziwe na utamaduni wa kushinda mechi zake nyumbani.

Mahesabu ya hatua hizi za makundi ni kwamba timu inayoshinda mechi zake tatu za nyumbani kwa ushindi mnono, hata kama ikipoteza zile za ugenini ina uwezekano mkubwa wa kuvuka na kwenda robo fainali, kama ilivyofanya Simba, 2019 Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo pamoja na kupoteza michezo yake yote mitatu ugenini, tena ilichapwa mabao 5-0 dhidi ya AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Al Ahly ya Misri, lakini ushindi wa mabao machache tu kwenye michezo ya nyumbani uliifanya kushika nafasi ya pili nyuma ya Wamisri hao.

Huu ni wakati wa wachezaji kujituma, kwani michuano hii hutazamwa na klabu nyingi Afrika na nje ya bara hili. Kujituma kwao, kupambana kwa ajili ya timu, kutawafanya pia kujiwekea mazingira mazuri ya kujipandisha thamani, hivyo kununuliliwa na klabu kubwa zaidi ndani na nje ya Afrika.

Luis Miquissone alionekana wakati akiichezea Simba kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2021, alipoifunga Al Ahly na wakaamua kuondoka naye na hilo liliwahi pia kutokea 2011, Mbwana Samatta alipokuwa akiichezea Simba kwenye mechi dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, wakaondoka naye kwa dau kubwa.

Kifupi hii ndiyo michuano ya kujiuza, kama ambavyo Fiston Mayele wa Yanga walipocheza Kombe la Shirikisho misimu miwili iliyopita alionekana na Pyramids.

Lakini pia, katika kaufanikisha hilo, tunawaomba mashabiki wa Simba na Yanga kujitokeza kwa wingi uwanjani kwa ajili ya kuzipa sapoti timu zao kwani siku zote shabiki ni mchezaji wa 12.

Katika hilo, Kocha Pitso Mosimane wakati huo akiwa Al Ahly, aliwahi kukiri kuwa mara nyingi wanapokuja kucheza hapa nchini, hasa na Simba hufikiria zaidi mashabiki wanaojazana uwanjani na kushangilia kwa nguvu, jambo ambalo lilikuwa likiwavuruga.

Akawa anaziasa timu zinapokwenda kucheza Benjamin Mkapa, kujiandaa kisaikolojia. Hivyo hii ni sifa kubwa kwa Watanzania na hawatakiwi kuiacha. Japo bado hawajakuwa na utamaduni wa kushangilia kwa muda wote wa dakika 90 kwa nguvu ile ile, lakini angalau kwa hiki walichojaliwa nacho wanapaswa kujazana uwanjani kesho na keshokutwa kuzipa sapoti Yanga na Simba.

Sisi tunazitakia kila la kheri timu zote mbili ambazo ni nembo ya soka la Tanzania ili zipate ushindi.