Kampeni ziwe za kistaarabu, kashfa matusi viepukwe

Nipashe
Published at 11:30 AM Nov 22 2024
Kampeni ziwe za kistaarabu, kashfa matusi viepukwe
Picha:Mtandao
Kampeni ziwe za kistaarabu, kashfa matusi viepukwe

KAMPENI za uchaguzi wa Serikali za Mitaa, zimeanza rasmi juzi nchini kwa vyama vyote vya siasa vilivyojitosa kwenye uchaguzi huo kunadi wagombea wao.

Kikubwa wananchi wanachotaka kukisikia kwenye kampeni hizo ni sera za vyama na viongozi watakaochaguliwa watakavyoweza kutatua kero zao.

Kampeni za kashfa, matusi wananchi hawataki kuzisikia wanataka kusikia viongozi hao watawafanyia nini kuondoa malalamiko ya mara kwa mara kwenye mitaa yao.

Ahadi zitakazotolewa kwenye kampeni hizo ndizo wananchi zitakazowafanya wawachague wanaojinadi badala ya kusikiliza kashfa na matusi.

Katika uzinduzi wa kampeni hizo juzi, vyama mbali mbali vitakavyoshiriki kwenye uchaguzi huo vimejinadi kufanya kampeni za kistaarabu kwa kuepuka kejeli na matusi.

Akizindua kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM), Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla, amewahakikishia wananchi kuwa chama chake ndio kinachoongoza na kwamba ajenda na hoja nyingi ni kuwashawishi wananchi wakichague.

Aliahidi kuwa chama kitasimamia falsafa ya R4 za Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kampeni hizo kistaarabu.

Viongozi watakaoshinda kwenye uchaguzi huo, wameonywa kutotanguliza maslahi yao mbele na kwamba chama kinaweza kuwaondoa katikati ya muhula wa uongozi. 

Aidha, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimejinadi katika mikoa mbali mbali kupitia viongozi wake, akiwamo Tundu Lissu, Freeman Mbowe, John Mrema, Godbless Lema na Salum Mwalimu.

Viongozi hao wamejinasibu kuwa ushindi ni lazima kwa wagombea wao na lengo ni kuleta mabadiliko.

Chama cha ACT-Wazalendo nacho kilitawanyika katika maeneo mbali mbali kunadi wagombea wake kuanzia juzi.

Chama hicho kupitia Ofisa Habari wake, Abdallah Hamis, kilisema kuwa kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, ataendesha kampeni mkoani Pwani wakati kiongozi mstaafu, Zitto Kabwe, atapiga kambi Kigoma.

Vyama vitatu tayari vimeanza kampeni hizo na kuweka ratiba ya mikoa itakayofanyika kampeni hizo.

Tunachotarajia ni kuona kampeni zinamalizika kwa amani mpaka siku ya kupiga kura, wananchi wachague wagombea wa vyama vilivyonadi sera zao vizuri na kueleweka.

Inapotokea vyama kwenda kinyume na lengo la kampeni, hapo ndipo dhana ya kunadi sera inapotea na kuingia kwenye siasa chafu za kuchafuana kwa matusi na kejeli.

Wananchi wamechoka kusikia matusi wanachotaka ni kuletewa maendeleo kwenye mitaa yao. Na hii inatokana na wengi wanaochaguliwa wanapoingia kwenye uongozi wanajisahau na ahadi zote walizotoa hazitekelezwi.

Wanachotaka wananchi ni kuona wanapowasilisha kero zao kwa viongozi waliowachagua wanazishughulikia na ikiwezekana kwa kushirikisha wananchi wa mitaa yao. Kwa sababu kila mtu anapoona kiongozi wake ana dhamira ya kuleta maendeleo lazima ataungwa mkono.

Kinachosubiriwa ni kuona matokeo ya kampeni hizo yanaleta mabadiliko kwa kuwajenga wagombea watakaopita kufanya vizuri kwenye uongozi.

Kura ndio mwamuzi wa mwisho, jinsi chama kitakavyonadi sera zake na wagombea wake ndivyo wananchi watakavyoshawishika kuchagua.

Vivyo hivyo, matokeo yatakapotangazwa ni matarajio yetu yatapokewa kwa amani na kama kuna pingamizi zitumike njia sahihi za kudai haki badala ya kudai kwa vurugu hali inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa ndio utakaoonyesha ukomavu wa Watanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani.

Mungu ubariki uchaguzi wa Serikali za Mitaa.