MUHAS yakutanisha madaktari bingwa kujadili ugonjwa wasaratani

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 04:19 PM Dec 03 2024
DAKTARI Bingwa wa saratani kutoka Chuo cha Clearview Cancer Institute nchini Marekani, Dk. Jeremy Hon
Picha: Mpigapicha Wetu
DAKTARI Bingwa wa saratani kutoka Chuo cha Clearview Cancer Institute nchini Marekani, Dk. Jeremy Hon

DAKTARI Bingwa wa saratani kutoka Chuo cha Clearview Cancer Institute nchini Marekani, Dk. Jeremy Hon, amewashauri madaktari na wauguzi nchini kuwa na kauli nzuri ya kuwasiliana na wagonjwa wa saratani ili kuwapa moyo kwani wengi wao umekata tamaa kutokana na ugonjwa huo unachukua muda mrefu kupona.

Bingwa huyo ametoa kauli hiyo jana wakati wa Kongamano la nne la Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (MUHAS) lililoandaliwa kwa kushirikiana na Idara ya Utafiti, Machapisho na Ubunifu ya MUHAS, lilikutanisha wataalam kujadili maendeleo katika matibabu ya saratani.

Dk. Hon, alisema kuwa kuwa daktari pekee haitoshi bali ni jinsi ya kuhudumia wagonjwa kwani ni njia bora ya kuwapunguzia mzigo wa ugonjwa huo. Dk. Hon alitoa wito kwa MUHAS kufanya utafiti zaidi na kuhimiza serikali kuhakikisha upatikanaji wa matibabu ya saratani kwa bei nafuu kupitia mazungumzo na kampuni ya dawa.

Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof.Appolinary Kamuhabwa, naye alisisitiza umuhimu wa ujuzi kwa madaktari wanaotibu saratani huku akibainisha siyo tu kuhusu teknolojia za kisasa bali pia uwezo wa kuwasiliana vyema na wagonjwa na kuwapa matumaini.

Prof. Kamuhabwa alisema MUHAS, kupitia ofisi yake ya kimataifa, itaendelea na mazungumzo zaidi na wabobezi katika kada ya afya ili kupata uzoefu wa kutibu saratani na agonjwa mbalimbali ili kuboresha huduma na kuwahamasisha madaktari wachanga.


Naye Dk. Chacha Mwita, mtaalam wa magonjwa ya mlipuko kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), alisisitiza umuhimu wa wananchi kuwahi kufanya vipimo vya wali vya ugonjwa huo ili kupunguza vifo.

Alisema kuwa saratani inayogunduliwa mapema ni rahisi kutibika, hivyo ameitaka jamii kutafuta huduma za matibabu mara wanapogundua dalili zisizo za kawaida.

Alitoa takwimu akibainisha kuwa Tanzania inakabiliwa na takriban visa vipya 44,000 vya saratani kila mwaka, na kusababisha vifo takriban 29,000.

Aliongeza kuwa aina za saratani zinazotawala nchini ni saratani ya mlango wa kizazi, tezi dume, matiti, na utumbo mpana. Katika ORCI pekee, visa vipya 7,252 vya saratani hugunduliwa kila mwaka, ambapo asilimia 73 ya wagonjwa ni wanawake.

Alisisitiza umuhimu wa programu za uchunguzi wa mapema, hasa kwa saratani ya mlango wa kizazi, ambazo zimefanikiwa kupunguza maambukizi ya aina hiyo ya saratani.

Hata hivyo, alieleza changamoto za wagonjwa kufikia huduma, ambapo karibu asilimia 40 ya wagonjwa hawapati huduma zinazohitajika, licha ya takwimu kuonyesha visa 44,000 vya saratani kila mwaka.

Aidha, Dk. Mwita alitaja sababu kadhaa zinazochangia ongezeko la saratani, zikiwemo kuongezeka kwa umri wa kuishi, ukuaji wa idadi ya watu, na mitindo isiyofaa ya maisha kama uvutaji sigara, lishe duni, na ukosefu wa mazoezi.