WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, amebaini kuwapo wimbi la maeneo ya huduma za kijamii yakiwamo shule na nyumba za ibada kubadilishwa matumizi kwa kujengwa maduka ya biashara na baa.
Pia amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga, kuendelea kuwachukulia hatua watumishi na kampuni za upimaji ardhi zinazobainika kuzalisha migogoro ya ardhi kwa kupima na kuuza maeneo ya wananchi.
Akifungua Wiki ya Ardhi jana jijini hapa, Waziri Ndejembi alisema wataalamu wametoa vibali vya kubadili matumizi maeneo ya makazi, huduma za kijamii na ya wazi yaliyotengwa yamekuwa ya biashara kinyume cha utaratibu.
Aliagiza wataalamu kuhakikisha mitaa inabaki kama ilivyopangwa kama ni biashara, makazi au huduma za kijamii.
“Nawaomba sana tumieni taaluma zenu katika kuhakikisha tunapanga miji yetu vizuri. Kuna mitaa imepimwa hata zimamoto haiwezi kuingia. Kuna kaugonjwa kameingia kakubadili matumizi maeneo ya makazi, kesho unakuta kuna fremu za biashara, baa kwenye eneo la makazi ya watu na ukifuatilia unakuta mabadiliko ya matumizi yamefanyika.
“Kuna maeneo mengi tu yamebadilishwa. Hata hapa Dodoma naweza kuwabeba niwapeleke muone najua kwenye mipango tumetenga maeneo ya shule, ya ibada lakini unakuja baadaye unabadili matumizi, tufanye kazi kwa weledi,” alisema.
Kuhusu upimaji wa viwanja unaofanywa na sekta binafsi, Ndejembi alisema kumekuwa na kampuni zinazopima zimeanza kuuza viwanja bila makubaliano na watu waliowapa kazi ya kupima na kwamba tayari serikali imeanza kuchukua hatua na tayari kampuni kati ya tatu au nne zimefutwa hatua na kutaka kasi hiyo iongezeke.
“Migogoro mingi inazalishwa na kampuni hizi za kupima ardhi mezani kwangu ninayo zaidi ya 20. Tuanze kuchukua hatua mara moja kwa kampuni ambazo zinatuzalishia migogoro.
“Kwa mfano kuna mwananchi mmoja ameomba shamba lake lipimwe amefuata taratibu zote na akaunganishwa na kampuni binafsi ya kupima lakini ikapima na kuanza kuuza viwanja yenyewe bila mwananchi mwenye eneo lake kujua viwanja vimeanza kuuzwa alishtuka watu waliouziwa wanafanya maendelezo, kampuni ilipoulizwa inaingilia huku na kutokea huku. Ni muhimu watendaji wetu kuhakikisha wananchi wanakuwa salama,” alisema.
Aliwataka watumishi wa sekta hiyo kuwa na nidhamu kuzingatia weledi na kujiepusha kuwa sehemu ya migogoro.
Kuhusu matumizi ya mfumo wa kidigitali wa e-ardhi, waziri huyo alisema umeanza kutoa huduma kwenye baadhi ya halmashauri katika mikoa mitano ya Arusha, Dodoma, Pwani, Tabora na Shinyanga na unalenga kuleta mageuzi katika sekta ya ardhi nchi.
“Mfumo umezingatia maeneo yote muhimu ya utoaji wa huduma, umefungamanishwa na mifumo mingine ya serikali ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa zingine muhimu na kuleta ufanisi katika sekta ya ardhi kwa wananchi,” alisema.
Alibainisha kuwa mfumo utaharakisha utoaji huduma, kuimarisha uwazi na uadilifu, kupunguza gharama na muda, kusaidia kufikia malengo yaliyowekwa kwenye makusanyo, utoaji hatimiliki, upimaji na uthamini wa ardhi.
Alisema mfumo huo utasaidia wananchi wa mijini na vijijini kupatiwa huduma kwa usawa bila urasimu.
“Nimepata taarifa kuwapo kwa watumishi wachache wanaokwepa kutumia mfumo kutoa huduma zinazotarajiwa kwa visingizio mbalimbali na kwa maslahi yao binafsi, nakuagiza Katibu Mkuu kila mtumishi ambaye mfumo huu umeanza kutumika ahakikishe anautumia kikamilifu na uendelee kuchukua hatua dhidi ya wasiotaka kuutumia,” alisema.
Ndejembi alikemea watumishi wanaofanya kazi kwa mazoea na kuharibu taswira ya sekta hiyo na kwamba hatawavumilia watakaobainika kuanzisha migogoro kwa maslahi yao binafsi.
“Tunataka kuondoa sura iliyopo kwenye jamii, unapotamka Wizara ya Ardhi kitu cha kwanza kinachokuja kichwani mwa mwananchi ni mgogoro, na hii migogoro mingi inasababishwa na wale ambao sio waadilifu, nataka tutoke kwenye dhana ya Wizara ya Migogoro iwe Wizara inayotatua changamoto za wananchi,” alisema.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Anthony Sanga, alisema katika wiki hiyo ya ardhi wataalamu watajadili masuala mbalimbali ikiwamo utafiti uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhusu sekta ya ardhi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED