JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya, linawashikilia watuhumiwa wawili kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Tawi la Machinjioni Kata ya Bwawani Michael Kalinga (36), Mkazi wa Makongolosi wilayani Chunya kwa kumpiga na kitu butu kichwani.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi ( ACP) Wilbert Siwa, jana alithibitisha watuhumiwa hao kukamatwa, alisema tukio hilo limetokea Desemba 02, mwaka huu majira ya saa 5:30 eneo la Mikoroshini wilayani Chunya.
Alisema Kalinga alikutwa amefariki na mwili wake kutelekezwa porini umbali wa mita 250 kutoka barabara ya Makongolosi kuelekea Lupatingatinga.
Alisema mwili wa marehemu ulikutwa na majeraha kichwani sehemu ya utosini baada kupigwa na kitu butu, na watuhumiwa hao ambao pia walimpora pikipiki yenye namba za usajili MC.464 ELL aina ya Kinglion.
Baada ya kupata taarifa za mauaji hayo, Polisi tulianza msako mkali ambapo Desemba 03, mwaka huu, huko Mlowo Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, tulifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wa mauaji ya Mwenyekiti huyo,” alisema ACP Siwa.
Alisema walifanikiwa kuwakuta watuhumiwa hao, wakiwa na pikipiki ya marehemu Kalinga, aliongeza kuwa upelelezi wa shauri hilo unaendelea kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria kuchukuliwa.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya. linatoa onyo kwa baadhi ya wananchi ambao wanaendelea kujihusisha na vitendo vya uhalifu kuacha mara moja kwani uhalifu haulipi na badala yake wajihusishe na shughuli halali za kujipatia kipato.
Kwa mujibu wa Baba mzazi wa marehemu, Michael Kalinga, Anderson Kalinga, mazishi yamefanyika jana katika Kata ya Makongolosi wilayani Chunya.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED