MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeaachia huru askari watatu wa Jeshi la Polisi, baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha kuwa walitumia silaha kumpora Grace Matage Sh Milioni 90, huku ikishangaa tukio hilo kuchukua zaidi ya mwezi mmoja bila kuripotiwa polisi.
Askari hao ni Koplo Ramadhani Tarimo (42) maarufu kama Rasta, Koplo Majid Abdallah (35), Koplo Stella Mashaka (41) Mkazi wa Railway, wengine waliyoachiwa katika kesi hiyo ni Ashiraf Sango (31) na Emmanuel Jimmy( 31).
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Franco Kiswaga wa Mahakama hiyo amesema jukumu ya kusibitisha shtaka ni upande wa Jamhuri, katika mashahidi wote saba hakuna hata mmoja aliyethibitisha kuwa askari hao walifanya unyang’anyi kwa kutumia silaha.
"Hakuna sehemu yoyote mashahidi akiwemo muhanga mwenyewe kueleza kuwa kabla na baada ya tukio hili walitumia silaha wakachukua fedha hizo, kwa mazingira haya Mahakama inawaachia huru kwa sababu upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha bila kuacha shaka lolote,"amesema
"Tukio hili lilitokea Agosti 28,2023 lakini halikuripotiwa siku hiyo kituo cha polisi lililipotiwa mwezi mwingine badae, Mahakama inajiuliza unyang’anyi wa kutumia silaha inawezekanaje ukatokea na mashashidi wote wakaa kimya, hili linatoa shaka,"amesema Hakimu Kiswaga
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo, Agosti 28, 2023 katika eneo la Kurasani, karibu na Ofisi za Uhamiaji, lililopo wilaya ya Ilala, ambapo siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja waliiba Sh milioni 90 kutoka kwa Grace Donald Matage.
Inadaiwa kabla na baada ya kufanya wizi huo, walimtishia Grace kwa bunduki ili waweze kujipatia fedha hizo bila kikwazo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED