MWENYEKITI wa Ngome ya Vijana wa Chama cha ACT- Wazalendo, Abdul Nondo, amesimulia alivyotekwa na kuteswa huku akisisitiza watekaji walimtishia atauawa endapo atasimulia lolote lililojiri walipomteka.
Nondo anayedaiwa kutekwa Desemba Mosi mwaka huu kwenye Stendi ya Mabasi ya Magufuli, wilayani Ubungo, Mkoa wa Dar es Salaam, alitoa kauli hiyo jana akiwa Hospitali ya Aga Khan, jijini jana.
"Watekaji walinichukua kwa nguvu, licha ya kelele na vuta nikuvute, sikusaidika na kulikuwa na bodaboda moja na watu wengine wakiangalia tukio lile likiendelea, lakini hawakunisaidia.
"Walinifunga kitambaa cheusi kwenye macho, kamba mikononi… walinisafirisha kwa mwendo huku nikipigwa na baadaye walinining`iniza mahali, miguu juu huku wakinipiga kwenye unyayo, walinipiga mgongoni na mikononi.
"Nilitolewa na kubadilishwa gari lingine… wakanifungua pingu, wakanifunga kamba na kunining`iniza katika gari dogo kutoka ‘hardtop’ kisha kunisukumiza kwenye fukwe hizo, wakaondoka…
"Nilihisi upepo na mawimbi ya bahari, ndipo nikapata msaada kwenda ofisi za chama. Nilikuwa na hali mbaya, sikuweza kwenda nyumbani maana ninaishi mwenyewe, hivyo salama yangu ilikuwa ni kwenda ofisini na ndipo nilipoletwa hospitalini," alisema Nondo.
Alisema haikuwa rahisi kwake kusikiliza mazungumzo ya waliomteka kwa kuwa walikuwa wananong`ona.
"Walikuwa wananong`onezana wao tu kiasi kwamba huwezi kusikiliza na kipindi hicho wamenifunga kitambaa cheusi kwenye macho, na wamenifunga kamba mikono na wameirudisha nyuma mgongoni.
"Walikuwa wananikanyaga na mwingine akaweka chuma katikati ya miguu halafu akaning`iniza juu, akawa ananipiga kwenye nyayo za miguu, ananipiga kwenye ‘joint’, ananipiga mgongoni, ananipiga tu, ananiambia 'wewe si cha mdomo, endelea, sisi tunakuua leo'. Yaani hakuna stori ambayo inaweza kunifanya kujua kwamba hawa watu walikuwa wanataka nini kwangu," alidai.
Nondo alidai watekaji walimwambia kwamba kilichomponza mpaka akatekwa "ni kuongeaongea sana".
Alidai watekaji walimwambia amekuwa akionywa mara kadhaa, lakini aliendelea kuzungumza, hivyo huo ulikuwa mwisho wake.
Nondo alidai kuwa baada ya kumtupa ufukweni, walimwambia akitoka huko aende moja kwa moja nyumbani kwake na asisimulie lolote mahali popote.
"Wakaniambia... 'haya ukitoka hapa moja kwa moja nenda nyumbani, na nyumbani kwako tunapajua, tusisikie unaongea chochote, tusisikie sijui unakwenda kwenye vyombo vya habari, tusisikie unamwambia yeyote, tukikusikia unafanya hivyo, awamu ya pili sisi tunakuja... tukikuchukua kama tulivyokuchukua leo, tunakuua, tunaweza tukakuchukua sehemu yoyote na hiyo awamu tukija kukuchukua tunakuua," alidai Nondo.
Mwenyekiti huyo alidaiwa kutekwa kwenye Stendi ya Mabasi ya Magufuli mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kuteremka kwenye basi, akitokea mkoani Kigoma, alikokuwa anashiriki kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Alidai alichukuliwa kwa nguvu na watu sita ambao walimfunga mikono na miguu pamoja na kumfunika uso na baadaye kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED