WAHITIMU 264 wa Chuo Kikuu cha Hubert Kairuki (HKMU) wanatarajiwa kutunukiwa shahada zao wakiwemo 115 wa binadamu wakati wa mahafali ya 22 siku ya Jumamosi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Makamu Mkuu wa chuo hicho,Profesa Yohana Mashalla, alisema mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa chuo hicho, Spika mstaafu Anne Makinda.
Alisema katika mahafali hayo, Mkuu wa Chuo atatunuku Vyeti, Stashahada, Shahada na Shahada za Uzamili za wahitimu wa HKMU
Profesa Mashalla alsiema katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 264 wamemaliza masomo yao, kati yao wako wanawake 170 na wanaume 94.
Alisema wahitimu katika mahafali hayo ni wahitimu 15 watakaotunukiwa Stashahada ya Ustawi wa Jamii, 71 watatunukiwa Stashahada ya Uuguzi, 8 watatunukiwa Shahada za Ustawi wa Jamii.
Alisema wahitimu 34 watatunukiwa shahada za Uuguzi na 115 watatunukiwa Shahada za Udaktari wa Binadamu ambapo wanawake watakuwa 63 na wanaume 52.
Profesa alisema wanawake wawili watatunukiwa Shahada za Uzamili ya Udaktari wa Binadamu katika Tiba na Afya ya Watoto (MMED, Paediatrics & Child Health).
Alisema wanaume wawili watagtunukiwa Shahada za Uzamili ya Upasuaji (MMED, Surgery) ambao wote ni wanaume na watano watatunukiwa Shahada ya Uzamili ya Magonjwa ya wanawake (MMED, Obstretics and Gynaecology).
Alisema takwimu hizo zinaonyesha kuwa matokeo ya wahitimu wa kike ni mazuri sana na hiyo inatokana na dhamira ya Chuo ya kuwawezesha wanawake kupata fursa sawa katika elimu ya juu.
“Chuo kinaheshimu usawa wa kijinsia katika elimu na tumetekeleza agizo la Serikali la kuwa na Dawati la Jinsia chuoni linalotumiwa na wanafunzi na wafanyakazi kupeleka changamoto za kijinsia zinazowakuta na zinapatiwa ufumbuzi na ushauri nasaha,” alisema.
“Nawapongeza Wahadhiri, Maprofesa, Wanataaluma wote pamoja na watumishi wa Chuo kwa kazi nzuri ya kuwalea na kuwafundisha wahitimu hawa katika miaka yote waliyokuwa hapa Chuoni,” alisema.
Alisema katika mwaka wa masomo wa 2024/2025, Chuo kimedahili wanafunzi wapya 513 katika fani mbalimbali.
Alisema ongezeko hilo la wanafunzi wa mwaka wa kwanza litafanya Chuo kuwa na jumla ya wanafunzi 1,992 kulinganisha na wanafunzi 1,781 katika mwaka wa masomo 2023/2024 hivyo kuwa na ongezeko la wanafunzi 211.
Alisema Serikali imeendelea kuwekeza kwenye elimu ya msingi na sekondari ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa, maabara, maktaba na kutoa kutoa elimu bure kwa wanafunzi wote kaika ngazi hizo.
Alisema kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia, uhitaji wa nafasi za kusoma elimu ya juu utaongezeka mara mbili zaidi ifikapo mwaka 2030.
“ Ongezeka hilo lisiposhughulikiwa mapema litaleta changamoto kubwa kweye Vyuo Vikuu nchini hivyo kushindwa kukidhi mategemeo ya wenye kiu ya kupata elimu ya juu,” alisema.
Alisema katika kukabiliana na ongezeko hilo la wanafunzi wenye uhitaji wa elimu ya juu, Chuo kumeendelea na mpango wake wa kujenga Kampasi yake Boko.
Alisema ukamilishwaji wa ujenzi wa Kampasi hiyo itakiwezesha Chuo kudahili wanafunzi wengi na kuanzisha programu mpya za masomo hivyo kupunguza upotevu wa vijana wenye sifa ya kujiunga na elimu ya juu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED