DC Dodoma atahadharisha matumizi mabaya ya mitandao upotoshaji taarifa

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 04:57 PM Dec 04 2024


Mkuu wa wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri akizungumza kwenye mkutano mkuu wa Misa-Tan.
Picha: Marco Maduhu
Mkuu wa wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri akizungumza kwenye mkutano mkuu wa Misa-Tan.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, amewataka waandishi wa habari pamoja na watumiaji wa mitandao kuwa makini wanaposambaza maudhui yao mtandaoni, akisisitiza umuhimu wa kufuata sheria za maudhui ya mtandaoni ili kuepuka upotoshaji.

Akizungumza leo, Desemba 4, 2024, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-Tan) Tawi la Tanzania, uliofanyika Dodoma katika ofisi za Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Shekimweri alionya dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao yanayoweza kuleta athari kwa taifa.

“Tunapaswa kuwa wazalendo na nchi yetu kwa kutumia mitandao kwa uwajibikaji na weledi. Taarifa zikiandikwa kwa upotoshaji zinaweza kuleta machafuko. Sheria zipo, na watu watakaokiuka watachukuliwa hatua kali za kisheria,” amesema.

Pia aliwasihi waandishi wa habari kuwa na wivu na heshima kwa taaluma yao kwa kuhakikisha hawatumiki vibaya katika kuchafua taaluma hiyo. Amesisitiza umuhimu wa kushirikiana na mamlaka husika, ikiwemo Tume ya Uchaguzi, kutoa elimu sahihi kwa wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.

1

Mkuu huyo wa wilaya ametoa pongezi kwa MISA-Tan kwa kusimamia Katiba yao na kuandaa mkutano mkuu wenye lengo la kujadili masuala muhimu, ikiwemo uchaguzi wa viongozi wapya wa taasisi hiyo.

Naye Mwenyekiti wa MISA-Tan, Salome Kitomari, ambaye muda wake wa uongozi umefikia kikomo, amesema teknolojia ya mtandao na matumizi ya akili bandia (AI) yamechangia ongezeko la maudhui yenye upotoshaji.

“Kwa sasa tupo kwenye dunia ya teknolojia ya mitandao, ikiwemo akili bandia, ambayo imeleta changamoto kubwa ya habari za upotoshaji. Ndiyo maana tunasisitiza mafunzo kwa waandishi wa habari ili wawe makini katika matumizi ya mitandao,” amesema.

Mkurugenzi wa Uendeshaji kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Albert Richard, akizungumzia kuhusu mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano, amesema minara 306 tayari imewashwa na kunufaisha wananchi milioni 8.5.

Mkutano huo umeambatana na mafunzo ya kudhibiti maudhui potofu ya mtandaoni na uchaguzi wa viongozi wa MISA-Tan, ukilenga kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari kwa kutumia teknolojia kwa uwajibikaji.