Mfumo kidijitali kukusanya taarifa waathirika wa wanyamapori wakali

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 09:56 AM Dec 04 2024
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana.
Picha:Mtandao
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana.

SERIKALI imeandaa mfumo wa kidijitali wa kukusanya na kuchakata taarifa za matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu uwandani ili kumaliza tatizo la ucheleweshaji taarifa za wananchi wanaoathiriwa kwa ajili ya ulipaji wa kifuta jasho na kifuta machozi.

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana, alisema hayo jana jijini hapa wakati akifungua semina ya siku mbili kwa maofisa wanyamapori wa wilaya nchini.

 “Ili kutatua changamoto hiyo wizara imeandaa mfumo wa kidijitali utakaotumika kukusanya na kuchakata taarifa za matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu uwandani (PAIS) ili kuharakisha utoaji wa taarifa na taratibu katika ulipaji wa kifuta jasho na kifuta machozi kwa wakati,” alisema.

 Pia alisema hivi sasa kumekuwapo malalamiko mengi kuhusu waathirika wa wanyamapori wakali na waharibifu kucheleweshewa malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi kutokana na taarifa kutofika kwa wakati wizarani.

 “Hivi sasa wabunge wengi wanalalamika lakini pia wananchi wanalalamika kucheleweshewa malipo yao kutokana na taarifa za matukio hayo kuchelewa kufika wizarani, hivyo mfumo huu utakwenda kumaliza tatizo hilo,” alisema. 

Alisema pamoja na mchango wa sekta ya maliasili na utalii katika uchumi na ustawi wa nchi na jamii bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kuongezeka kwa migongano baina ya binadamu na wanyamapori. 

Alisema migongano hiyo inayosababishwa na uvamizi wa shughuli za kibinadamu karibu na maeneo ya hifadhi na kwenye shoroba za wanayamapori hususani shughuli za kilimo, ufugaji na makazi ya kudumu na hivyo kupelekea kuzibwa kwa shoroba.

 Pia alisema changamoto nyingine ni kuongezeka kwa vitendo vya ujangili wa wanayama na migogoro ya mipaka ya hifadhi na vijiji vinavyozunguka maeneo yaliyohifadhiwa.

Kutokana  na hali hiyo, alisema  serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kutatua changamoto za uhifadhi nchini ikiwa ni pamoja na kuandaa sera, kanuni,mikakati,mipango na miongozo mbalimbali.

Mkurugenzi wa Wanyamapori, Dk. Alexander Lobora, alisema semina hiyo inajumuisha maofisa wanyamapori wa wilaya nchini. 

Alisema lengo ni kubadilishana uzoefu pamoja na kuwapatia mafunzo kuhusu mfumo huo wa ukusanyaji wa taarifa za matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu uwandani ili kuharakisha mchakato wa malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi kinachotolewa na serikali. 

“Matukio ya mgangano baina ya wanyamapori na binadamu yanachangia sana katika kuathiri uchumi wa mtu mmojammoja na taifa kwa ujumla kuanzia mwenzi Julai mwaka huu hadi sasa serikali imeshalipa Sh. bilioni 2.5 kwa watu walioathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu,” alisema.