NILIUTAZAMA mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Fountain Gate iliyokuwa ikicheza nyumbani dhidi ya Pamba Jiji FC, nikakubaliana na mawazo ya viongozi wa klabu mbalimbali nchini kusajili makipa kutoka nje ya nchi.
Mechi hiyo iliyochezwa, Novemba 5, Uwanja wa Kwaraa, Babati mkoani Manyara, ilishuhudiwa, Fountain Gate FC ikipoteza kwa mara ya kwanza nyumbani kwao ilipochapwa mabao 3-1 dhidi ya Pamba Jiji, ambayo ilikuwa haijapata ushindi wowote kwa michezo 10 ya nyuma. Ukawa ni ushindi wa kwanza kwa timu hiyo.
Kilichovutia au kunishangaza ni jinsi mabao yalivyokuwa yakiingia. Yalikuwa ni mabao rahisi na ya kizembe kiasi kwamba unashangaa kama kweli anayefungwa ni golikipa wa hadhi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo ni ya sita kwa ubora Afrika.
Mfano mzuri ni bao la tatu, ambalo kwa hali ya kawaida halikutakiwa kufungwa hata kwa bahati mbaya.
Faulo ilitokea kwenye kibendera cha kona kuelekea kwenye lango la Pamba Jiji. Golikipa Bakari Fikirini, ndiye aliyekwenda kupiga. Cha kushangaza badala ya kuupiga mbele, aliupiga ndani, tena kule kule nyuma ya lango lake wakati yeye mwenyewe hayupo langoni.
Kilichotokea ni kwamba, mpira ule ulimkuta mchezaji wa Pamba Jiji akiwa na lango tupu akaukwamisha wavuni. Nadhani ni bao ambalo lilimkera kila shabiki wa Fountain Gate, pia kuwashangaza wengi uwanjani na waliokuwa wanautazama mchezo huo kupitia televisheni.
Hata kipa wa timu za mchangani hawezi kufanya hiki ambacho kipa huyu alikifanya katika mchezo huo.
Ingawa bado hazijathibitishwa, lakini habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema uongozi wa klabu hiyo umewasimamisha wachezaji wawili ambao ni golikipa Fikirini, Abal Kassim na kocha wa makipa, Ally Mustapha 'Barthez'.
Taarifa zinasema kusimamishwa kwao kunahusiana na mchezo huo, lakini mpaka sasa uongozi wa klabu hiyo haujatoa taarifa rasmi.
Ni kipa huyu huyu Fikirini, aliyewahi kudaiwa kufanya kosa lililoigharimu timu yake ya Ihefu FC ikafungwa na Yanga bao 1-0, Januari 16, 2023, katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Ligi Kuu msimu wa 2022/23.
Aliudunda mpira na kuuweka chini wakati nyuma yake kulikuwa na Fiston Mayele, akauwahi na kupachika bao pekee katika mchezo huo ambao kabla ya hapo ulikuwa mgumu na usiotabirika.
Kwa hili lililotokea naungana na baadhi ya viongozi wa klabu ambao wameanza kusajili makipa kutoka nje ya nchi.
Kuna mjadala ulizuka kwa baadhi ya wachambuzi wakihoji kwa nini kumekuwa na wimbi la kusajili magolikipa kutoka nje ya nchi, badala ya kusajili vipaji vilivyo hapa nchini.
Wakataka itungwe kanuni ambayo itafuta uwapo wa makipa wa kigeni nchi, badala yake wawe wazawa tu, ili wapate muda mwingi wa kucheza kwa ajili ya manufaa ya taifa.
Wasichokijua wachambuzi wengi ni kwamba viongozi wa klabu si kwamba wanakwenda kusajili makipa wa nje kwa sababu hapa nchini hakuna makipa bora au wazuri, bali ni wanatafuta uaminifu.
Baadhi ya makipa wazawa kwa sasa wamekuwa hawaaminiwi kutokana na tabia ya kile kinachoelezwa kuhujumu au kuuza mechi kwa timu pinzani, tofauti na makipa kutoka nje.
Wala si kwa bahati mbaya, Simba, Yanga, Azam na timu zingine kuwa na makipa kutoka nje. Wao wenyewe wanajuana na hawaaminiani.
Kwa hili lililotokea nadhani Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), na Bodi ya Ligi iendelee tu kuziruhusu klabu zinazotaka kusajili makipa kutoka nje ya nchi. Kingine ni kwamba hii ni kengele kwa makipa wazawa waanze kujitazama wenyewe na kujiuliza ni kwa nini kwa miaka ya hivi karibuni wameanza kutoaminika kukaa langoni hata kwa timu ndogo tu kama KMC, Coastal Union, au Namungo?
Hali ikiendelea hivi tusije kushangaa ukafika msimu klabu zote 16 zikawa na makipa wa kigeni. Wazawa sasa ni wakati wakujitafakari na kujirekebisha wenyewe, badala ya kusubiri kutungwa kanuni za kuwabeba.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED