MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ametangaza rasmi kugombea kiti hicho, huku akijibu hoja za maridhiano, ubadhirifu wa fedha na rushwa.
Aidha, jana alichukua fomu ya kutetea nafasi hiyo ambayo anachuana na Makamu wake, Tundu Lissu, na anatarajia kuirejesha leo.
Mbowe ambaye alihutubia kwa saa 1:18, kwenye mkutano wake na wahariri wa habari pamoja na waandishi wa habari, uliofanyika nyumbani kwake, Mikocheni mkoani Dar es Salaam, alinukuu kauli 10 za viongozi mashuhuri duniani kuhusu maridhiano.
Alisema kinachomsukuma kugombea uongozi kwa awamu nyingine ni dhamira yake ya kuhakikisha CHADEMA inaendelea kuwa chama kikubwa na hatimaye kushika dola.
“Hakuna kiwango cha matusi, kejeli wala dharau kinachoweza kuniondoa Mbowe kuifikiria kesho ninayoitamani. Na kesho ninayoitamani ni kuona chama hiki kikiwa na nguvu na uwezo wa kuongoza serikali ya nchi hii kuleta uhuru wa kweli na maendeleo ya kweli kwa wananchi,” alisema.
Alisema watu wanaompinga na kumkejeli hawamnyimi usingizi kwa kuwa anawaza namna ya kujenga CHADEMA imara.
“Nikiangalia minyukano ndani ya mitandao, naona kabisa makundi yanasigana pasipo sababu. Nimeonya mara nyingi na ninaonya tena tusije baadaye tukatafutiana lawama kwenye chama. Baada ya mwezi mmoja, uchaguzi utakuwa umekwisha. Tutakuwa wageni wa nani?
“Nimesema mara nyingi sana nataka kuondoka, lakini siwezi kuondoka katikati ya minyukano iliyopo. Kwa hiyo CHADEMA nipo, nitakuwapo, nitagombea na mimi na viongozi wenzangu wanaoniunga mkono na wasioniunga mkono. Naamini tutakutana kwenye mazungumzo tukiweke chama chetu,” alisema na kusisitiza kuwa anayetaka kugombea wakutane kwenye sanduku la kura.
“Tufanye kampeni za kistaarabu. Kila mmoja afanye kampeni akitambua ana wajibu wa kukilinda chama. Wanaoniunga na wasioniunga mkono, watambue naheshimu haki yao lakini hawana haki ya kunitukana,” alisisitiza
Alisema kiongozi yeyote atakayeshinda kukiongoza anahitaji watu wote wakiwamo walioshindwa ili kuendelea kukijenga.
“Hii minyukano inahitaji utu uzima. Nimeangalia na nimetafakari kwa kina. Tunahitaji Katiba kwa kucheza miguu yote, ya diplomasia, ushirikishwaji, barabara na kila silaha itumike. Na hii ni ajenda ya msingi katika chama chetu,” alisema.
Alisema ajenda nyingine ni mifumo mizuri ya uchaguzi itakayoweka uwazi, uhuru na haki pamoja na sheria nzuri za uchaguzi, ambazo ni miongoni mwa hoja 11 zilizokuwa zimewasilishwa kwenye meza ya maridhiano.
Mahitaji hayo ya Watanzania, alisema yanahitaji mazungumzo na makundi yote, wakiwamo wanasiasa, taasisi za kidini, wanasheria na wanazuoni. Alisema pamoja na minyukano inayoendelea mitandaoni, chama hicho kiko imara na hakitapasuka wala kufa.
Kuhusu ukomo wa madaraka, alisema unapaswa kufanywa kwenye sanduku la kura na chama hicho kina uhuru wa kidemokrasia kuchagua na kuchaguliwa.
“Sijui ni kigezo gani kinatumika kusema Mbowe amechoka. Sijachoka. Ninaweza kufanya mikutano nane kwa siku bila kula. Namtaka huyo mwenye nguvu hii kuliko mimi. Nimekaa CHADEMA miaka 33 ya shuruba,” alisema.
AJIBU TUHUMA
Kuhusu tuhuma zinazotolewa na Lissu kwamba kuna baadhi ya viongozi wamekula rushwa, alisema si za kweli na kwamba kama zina ushahidi zinapaswa kuwasilishwa kwenye kamati ya nidhamu inayosiamamiwa na kiongozi huyo (Lissu).
Alisema Lissu ana mamlaka ya kumwamuru Katibu Mkuu wa chama kumwandalia kikao na kwamba madai kuwa ofisi hiyo haijatekeleza hilo si ya kweli.
Mbowe alianza kwa kunukuu kauli 10 za viongozi mashuhuri duniani, akiwamo Hayati Nelson Mandela aliyekuwa mpigania uhuru na Rais wa Afrika Kusini, Makatibu Wakuu wastaafu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon na Koffi Anan, marais wa Marekani, Jonh Kennedy na Barack Obama, Kansela mstaafu wa Ujerumani, Angela Markel, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Wiston Churchil na Waziri Mkuu wa India, Mahatma Gandhi, ambao kwa nyakati mbalimbali walihimiza umuhimu wa maridhiano hasa kunapotokea tofauti kubwa za kisiasa.
Alisema Kamati Kuu na Baraza Kuu la CHADEMA, waliomba mara kadhaa kufanya mazungumzo na Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, ili kutafuta mkwamo wa kisiasa wakati huo lakini alikataa na kwamba Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani, alikubali ombi hilo.
Alisema anaamini kwamba hata sasa, chama hicho kimefanikiwa kufanya uchaguzi katika ngazi mbalimbali kutokana na maridhiano ambayo yalifanikisha kufuta katazo la miaka saba la kuzuia mikutano ya vyama vya siasa.
“Maridhiano si jambo jepesi lakini ni jambo lisiloepukika katika siasa duniani kote. Makundi mbalimbali yanachukua upande wa maridhiano kutokana kile inachotamani,” alisema.
Alisema CHADEMA ilikuwa na hoja 11 kwenye mazungumzo hayo kati yake na serikali pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizofanikisha zaidi ya kesi 400, zilizokuwa zimebambikwa kwa makada na viongozi wake kufutwa, wafungwa wa kisiasa kuachiwa huru, kufunguliwa kwa mikutano ya kisiasa na kulipwa ruzuku ambayo ni stahiki ya chama hicho.
Hata hivyo, alisema maridhiano yalipingwa na wahafidhina pamoja na wanufaika wa uchaguzi mbovu wa mwaka 2020, ndani ya CCM. Alisema upinzani wa maridhiano ndani ya CCM uliongezewa nguvu na ule uliokuwa ndani ya CHADEMA.
“Mtu yeyote unayejaribu kutaka akuunge mkono, anatarajia kuona unamheshimu na mkubali kukosa ili kupata kikubwa zaidi mnachokitaka wote. “Ninajivunia sana mazungumzo na uamuzi wetu wa kuingia kwenye maridhiano,” alisema.
Katazo la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, alisema liliiumiza zaidi CHADEMA kwa kuwa wabunge, madiwani na viongozi wake wa ngazi mbalimbali waliumizwa na wengine kuuawa, jambo lililowafanya wananchi waogope kuwa upande wa vyama vya upinzani.
Alisema pamoja na kwamba maridhiano yalikwama, Tanzania inahitaji Katiba Mpya, Mifumo huru ya uchaguzi na sheria nzuri za kusimamia uchaguzi. Alisema chama hicho kimeazimia kutengeneza ajenda za kitaifa ambazo ni Katiba Mpya, mifumo huru ya uchaguzi na sheria nzuri, ambazo hakiwezi kusimama peke yake na kufanikiwa kuzipata.
TUHUMA RUSHWA
Alisema hawezi kuiuza CHADEMA kwa ahadi ya cheo kikubwa serikalini; na kwamba angetaka kufanya hivyo angekubali ahadi za hayati Magufuli.
“Aliniahidi ahadi zote duniani. Aliniambia nijiunge na CCM nichague cheo chochote unachotaka, nikamwambia sitaki. Akasema achana na CHADEMA chagua biashara yoyote unayotaka nitakurejeshea mali zako zote ulizonyang’anywa, nikakataa. Siwezi kukubali sasa hivi,” alisema na kuongeza kuwa hajaahidiwa cheo wala fedha kutoka sehemu yoyote.
Kuhusu ubadhirifu, alisema CHADEMA inaendeshwa kwa michango ya wanachama na kwamba kwa miaka mitano mfululizo, imepata hati safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED