Turekebishe makosa uchaguzi wa mitaa

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:43 AM Nov 13 2024
Turekebishe makosa  uchaguzi wa mitaa
Picha:Mtandao
Turekebishe makosa uchaguzi wa mitaa

WAKATI uchaguzi wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu, Novemba 27, lakini vilio vya kuenguliwa kwa wagombea katika kinyang’anyiro hicho vinasikika kila kona.

Idadi kubwa ya wagombea hao ni kutoka vyama vikuu vya upinzani vya CHADEMA, ACT-Wazalendo na CUF ambao walijaza fomu katika ngazi ya mitaa, vijiji na vitongoji.

ACT Wazalendo, inaripoti kuwa asilimia 60 ya wagombea wake wameenguliwa, huku CHADEMA ikilalamika wagombea 242 wameondolewa katika wilaya ya Kilosa na wengine kadhaa katika mikoa tofauti.

Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi, Novemba 8, ilikuwa ni siku ya uteuzi wa wagombea waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, anavikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wengine wa uchaguzi kuwa  asiyeridhika na taratibu za uchaguzi akate rufani.

Pamoja na kauli hiyo ya kutia moyo ya Mchengerwa,  bado songombingo zilionekana kuongezeka kwa maofisa wa uchaguzi kudaiwa kufunga ofisi na hivyo rufaa hizo kukwamishwa.

Wakati hali hiyo ikiibua vilio kila kona, kuna hoja za msingi zimejitokeza kiasi kwamba zinaonyesha wasiwasi wa kuwepo na ombwe au upungufu katika maandalizi na uratibu wa uchaguzi wa serikali za mitaa nchini.

Kuanzia vyama vya siasa vyenyewe vinatakiwa kujitafakari kwa kina njia vinavyotumia kupata wagombea wake, kwani kuwa wasiwasi vyama vingi vya siasa havina utaratibu bora wa kuwaandaa na kuwateua  wagombea ili kwenda kushindana.

Kutokana na makosa ambayo yanadaiwa kujitokeza na hatimaye kuondolewa kwa wagombea hao, inaelezwa wengi wao hawakujaza kama inavyotakiwa fomu za wagombea na wengine kushindwa hata kutaja umri wao.

Kutokana na makosa hayo madogo.

Kama vyama vya siasa vingekuwa na maandalizi mazuri yasingejitokeza kwani yangesahihishwa na vyama husika kabla ya kupelekwa kwa ofisi za uchaguzi kwa ajili ya kupitiwa.

Lakini hayo hayakufanyika, kinachoonekana hapo baada ya kupitishwa katika mchujo, wagombea hao walikwenda kuchukua fomu na kuzijaza bila usimamizi wa vyama husika na hatimaye kuzalisha wimbi hilo la wagombea kutokubaliwa kwa kukosa sifa.

Utaratibu huo wa wagombea kujaza fomu bila usimamizi wa vyama husika, sio wa leo wala wa jana, kwani kila uchaguzi unapotokea manung’uniko hayo hujitokeza na kusababisha taharuki miongoni mwa wadau wa siasa hapa nchini.

Viongozi wa vyama vya siasa watambue asilimia zaidi ya 90 ya wanachama wao hawana uelewa mpana kuhusu kanuni za uchaguzi, hivyo ni muhimu  kutoa elimu ya chaguzi kabla na baada ya kuwapata wagombea ili iwe rahisi kuondokana na makosa kama hayo.

Kwa kueleza hivyo, sio kwamba kuondolewa kwao ni halali, la hasha, bali ni kujaribu kuondokana na visingizio ambavyo vinaweza kutumika kwa ajili ya kuwanyima haki yao.

Kuhusu TAMISEMI inayosimamia uchaguzi huo, ni muhimu isimame kama mlezi na msimamia haki  zaidi, kukuza na kuimarisha demokrasia katika uchaguzi wa serikali za mitaa, badala ya kuendeleza sintofahamu.

Kuyaondoa majina kwa makosa madogo kama kukosea herufi ya jina, ambayo Rais Samia Suluhu Hassan, alikataa haipaswi kuwa ni moja ya vigezo vya kukosa sifa.

Itumike njia bora zaidi ya kuwaelemisha na kuyaona makosa kama hayo ni ya kibinadamu na si jambo la kuongeza mpasuko kwenye uchaguzi.

Malalamiko kama hayo yakizidi kuendelea yanaweza kuweka nchi katika nafasi mbaya ya watu kukosa usawa wa haki zao za msingi za kuchagua au kuchaguliwa.  Tamko la Waziri Mchengerwa limekuja kwa wakati katika kurekebisha suala hilo, lakini hilo halitoshi kwani kuwaagiza maofisa kuzifanyia kazi rufaa hizo kwa uhalidilifu na kuwarudisha wale waliondolewa kimakosa ni hatua inayosubiriwa na wengi.

Watanzania wanategemea Waziri  Mchengerwa atasimamia vyema uchaguzi wa mitaa na itakuwa moja ya mtihani wake mkubwa katika nafasi yake ndani ya serikali ya awamu ya sita, hivyo asiondoe imani hiyo.

Pamoja na hali hiyo, Watanzania wameonekana kuhamasika kushiriki uchaguzi baada ya kujiandikisha kwa asilimia kubwa, hivyo wanaamini wataenda katika masanduku ya kura kukiwa haki na uwazi na ushindani na si zaidi.

Shime wekeni sawa mambo ili uchaguzi usiwe kama wa 2019.