Dua njema kidato cha nne 2024

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:05 AM Nov 12 2024
Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Said Mohamed
Picha:Mtandao
Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Said Mohamed

WANAFUNZI wa kidato cha nne wameanza mitihani ya taifa kukamilisha safari ya kuhitimu daraja hilo la taaluma.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Said Mohamed wakati akitangaza kuanza kwa mtihani huo Jumatatu wiki hii ukitarajiwa kuendelea hadi mwisho wa mwezi huu ifikapo Novemba 29.
 Anasema idadi ya wa watahiniwa mwaka huu ni 557, 731, ambao ni wa shule na wengine wa vituo vya kujitegemea maarufu QT.
 
 Wakati wanafunzi wakiwa katika mtihani huo, ni vyema kuendelea kuwakumbusha kujitenga na kila aina ya udanganyifu, badala yake waufanye kwa kuzingatia utararibu unaokubalika, si vinginevyo.
 
 Ninakumbushia hilo, kwa sababu ni karibu kila mwaka baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakifutiwa matokeo ya mtihani kutokana na sababu mbalimbali, kubwa ikiwa ni kufanya udanganyifu.
 
 Hivyo, ingekuwa ni vyema kama mtindo huo wa udanganyifu utafikia kikomo, ili wanafunzi wafanye mtihani na kutegemea akili zao kutokana na kile ambacho wamefundishwa kwa muda wa miaka minne.
 
 Mfano, katika matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana, wanafunzi 102 walifutiwa matokeo yao baada ya kubainika wamefanya udanganyifu, wakiwamo wengine walioandika matusi kwenye karatasi za majibu.
 
 Sidhani kwamba, kwa miaka minne kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, wanafunzi wanafundishwa kufanya udanganyifu au kuandika matusi kwenye karatasi za majibu. Hiyo ni tabia mbaya inayotakiwa kuachwa.
 
 Wanafunzi wa kidato cha nne wanaandaliwa kusonga mbele kielimu ili baadaye waje walisaidie taifa lao katika nafasi mbalimbali kulingana na kile ambacho watakuwa wamekisomea.
 
 Ufaulu wa mtihani wenye udanganyifu hauwezi kusaidia taifa kupata wataalam bora wa wa fani mbalimbali watakaolisaidia kwa miaka ya baadaye. Hivyo, mtindo huo ungekemewa na kila mdau wa elimu.
 
 Ingekuwa ni vyema walioanza mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka huu waonyeshe mfano bora wa kutojihusisha na kila ya aina ya udanganyifu ili isiendelee kujengeka vichwani mwa wanafunzi kuwa udanganyifu ni sehemu muhimu katika mtihani huo.
 
 Katika mazingira hayo, wanafunzi wengine wasio na tabia hiyo, wanaweza kushawishika na kujikuta wameingia kwenye mtego wa kutegemea udanganyifu badala ya akili zao.
 
 Vilevile, ikumbukwe kwamba, hadi mwanafunzi anafanya udanganyifu katika mtihani, maana yake kuna baadhi ya walimu na wadau wengine wa elimu wamehusika kwa namna moja au nyingine.
 
 Hivyo, ungefanyika ufuatiliaji wa kina ili kubaini mianya yote inayosababisha kuendelea kwa vitendo hivyo na kuwachukulia hatua kali wahusika ili wasiendelee kuvuruga utaratibu wa ufanyaji mtihani.
 
 Ikiwezekana, kila shule iwe na kitengo cha udhibiti ubora kinachosimamia mfumo mzima wa ufundishaji kutoka utungaji wa mitihani, usahihishaji hadi matokeo.
 
 Lakini pia si vibaya kama kutakuwa na mfumo wa kumtambua mtahiniwa kwa alama za vidole kabla hajaingia katika chumba cha mtihani, ili kuwadhibiti wale wanaotoa fedha kwa lengo la kufanyiwa mitihani waweze kufaulu kwa kutumia akili za wengine.
 
 Hata hivyo, ninadhani ipo haja sasa wadau wa elimu kuangalia uwezekano mwingine ambao wanaona unafaa kupima uelewa wa mwanafunzi nje ya mtihaani ambao sasa unaingiliwa na danganyifu.
  
 Mfumo wetu wa elimu kupimwa uelewa wa mwanafunzi kumejikitika katika mitihani kuanzia darasa la kwanza, lakini si vibaya kama wataalam wetu watakuja na njia mbadala wa mitihani.
 
 Pamoja na hayo, niwatakie kila la heri wanafunzi wa kidato cha nne walioanza mtihani wao wa taifa kwa mwaka 2024, wajiepusha na  udanganyifu, watumie akili ili wafaulu kihalali.