Serikali tangu awamu ya tano, iliamua kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji ikiwamo ya reli ya kisasa (SGR) ambayo hadi sasa treni zimeanza safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma.
Hatua hiyo imerahisisha usafiri wa abiria katika eneo hilo ambalo reli imekamilika. Badala ya watu kutumia usafiri wa mabasi ambao kutoka sehemu moja hadi nyingine unatumia saa 10 za zaidi, usafiri wa SGR unatumia chini ya saa nne kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.
Kwa mantiki hiyo, ni usafiri unaorahisisha mambo mengi zikiwamo shughuli za kibiashara au mikutano na kuokoa gharama. Awali, mtu alikuwa akitaka kwenda Dodoma akitoka Dar es Salaam au vinginevyo kwa ajili ya mkutano au shughui za kibiashara, alikuwa anatumia saa 10 na kuendelea njiani na kulazimika kutafuta malazi katika miji hiyo. Lakini kutokana na kuwapo usafiri wa treni ya SGR, alipunguza gharama kwa kuwa anaweza kutoka sehemu moja hadi nyingine na kufanya shughuli zake na hatimaye kurejea klwenye eneo lake.
Baada ya kuwapo kwa unafuu huo, kiu ya watu wa mikoa ya mbali kama vile Mwanza, Kigoma, Tabora na Shinyanga ni kuona ujenzi wa reli hiyo unakamilika haraka ili kuwawezesha nao kunufaika na aina hiyo ya usafiri na kuokoa muda mwingi wa kukaa barabarani kwenye basi.
Usafiri kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma kwa njia ya Barabara, kwa mfano, ni saa 18 au zaidi kutegemea hali ya chombo cha usafiri. Iwapo usafiri wa SGR utakamilika ni muda mfupi utatumika, hivyo kuwaondolea abiria uchovu ambao wanakumbana nao sasa kwa kutumia mabasi.
Pamoja na mambo hayo kurahishshwa, hhivi karibuni kumekuwa na taarifa za treni kukwama katika baadhi ya maeneo hali inayotia wasiwasi kuhusu usalama wa miundombinu na mabehewa pamoja na abiria. Hali hiyo inatia shaka kwa kuwa inawezekana kukawapo hujuma ndani yake.
Kutokana na kuwapo kwa hali hiyo, kumetolewa ushauri wa kufungwa kwa kamera za usalama (CCTV) katika mradi huo ili kudhibiti uhalifu na hujuma dhidi ya miundombinu zinazoweza kujitokeza.
Ikumbukwe kwamba kuanza kwa usafiri wa treni ya SGR kumesababisha wamiliki wa mabasi yaliyokuwa yakifanya safari kati ya Dar es Salaam hadi Dodoma walikosa biashara, hivyo kulazikimka kuhamishia mabasi yao maeneo mengine. Hali hiyo pia inaweza kuongezeka zaidi baada ya miundombinu hiyo ya SRG kukamilika.
Kutokana na hali hiyo, Kamati za Kudumu za Bunge ya Bajeti na Miundombinu zimeshauri Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuweka mifumo ya ulinzi wa miundombinu hiyo ikiwamo ufungaji wa kamera za CCTV ili kudhibiti uharibifu wa miundombinu ya nyaya za umeme unaofanywa na watu wasio na nia njema na mradi huo.
Wakati wa ziara za kamati hizo jana kwenye reli hiyo jana jijini Dar es Salaam, ilielezwa kuwa hivi karibuni kumeripotiwa kusimama kwa treni mpya ya mwendokasi, huku sababu zilizobainishwa ikiwa ni uharibifu wa miundombinu ya nyaya za umeme, hivyo hakuna budi kuimarishwa ulinzi. Katika ziara hiyo, ilibainika kuna upungufu na kasioro kadhaa katika miundombinu ya SGR zikiwamo za kiulinzi katika baadhi ya maeneo.
Kwa hakika, serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu hiyo iliyokwisha na inayoendelea hivyo si vyema ikaachwa bila ulinzi kama ilivyobaikishwa na kamati hizo. Kwa mantiki hiyo, suala la ulinzi wa miundombinu hiyo si l;a mjadala ili kudhibiti hujuma zinazoweza kujitokeza na kuhatarisha usalama wa abiria pia.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED