Ushindani huu Ligi Kuu Bara ukiendelea utaipaisha zaidi

Nipashe
Published at 10:44 AM Nov 11 2024
Ligi Kuu Bara
Picha:Mtandao
Ligi Kuu Bara

LIGI Kuu Tanzania Bara imeingia raundi ya 10, huku kila timu ikiwa tayari imeshaonja ladha ya kufungwa.

Kwa raundi za mwanzo tu kabla hata kufika nusu msimu, pia kuelekea kipindi cha dirisha dogo ligi imeanza kuwa na ushindani mkubwa kuliko msimu uliopita.

Sare ya mabao 2-2 kati ya Simba na Coastal Union Oktoba 4, mwaka huu, katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam, ilianza kuonesha kuwapo kwa hali ya ushindani.

Ni mechi ambayo Simba ilikuwa inaongoza 2-0 hadi mapumziko, lakini kwa hali ya kushangaza Coastal walirudisha mabao yote kipindi cha pili.

Ushindi wa dakika za mwisho ambao Simba iliupata dhidi ya Mashujaa FC, Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, uliendelea kuonesha msimu huu si wa lelemama na timu zimejipanga.

Baada ya hapo tukashuhudia Mabingwa Watetezi, Yanga walipoteza kwa mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu, wakifungwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC, Jumamosi ya Novemba 2, Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam, kabla ya Alhamisi iliyopita kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Tabora United.

Hii inaonesha kuwa msimu huu timu zimejipanga kisawasawa kupambana kikwelikweli na kuondoa woga kwa timu kubwa.

Tulichoshuhudia ni kwamba msimu huu timu pamoja na kupaki basi zimekuwa zikipata muda wa kwenda kushambulia kwa kasi dhidi ya timu kubwa, ambazo mara nyingi huwa hazipo kwenye shepu nzuri zinapokuwa zinashambulia.

Tatizo ni kwamba timu nyingi zilikuwa na tabia ya woga na kutotumia nafasi zinapofanya mashambulizi ya kushtukiza.

Mpaka kufikia raundi hizi Ligi Kuu inaonekana imechangamka na kuvutia wengi. Hii sasa ndiyo inaweza kufanya mashabiki wakavutika kwenda viwanjani kwa sababu wanaona kuna upinzani. Mashabiki wa soka mara nyingi huwa hawapendi kutazama mpira ambao wanaona timu fulani ni lazima ishinde.

Mapokezi makubwa walioyapata Tabora United kila basi lao linapoonekana kuanzia Dar es Salaam hadi Tabora ni ishara tosha ya kwamba mashabiki wanapenda ushindani kwenye ligi.

Wachezaji wa Tabora United kwa walichokiona kiwe kama deni kwao, waendelee kucheza kwa nguvu na ari ile ile walioionesha kwenye mchezo dhidi ya Yanga, si baada ya hapo wanarudi tena kuwa kibonde kwani kufanya hivyo watakuwa hawajawatendea haki mashabiki wao.

Tunaamini hili pia litakuwa ni somo kwa timu zingine za Ligi Kuu hasa kwa kuangalia heshima, zawadi na mapokezi ambayo mashabiki wa soka waliokuwa wakiwaonesha wachezaji wa Tabora United kila wanapopita.

Hivyo hata zingine zinaweza kupata heshima hiyo kama viongozi na wachezaji wake watajitambua na kuweka mkazo kwenye kusaka ushindi dhidi ya timu zote zinazokutana nazo kwenye Ligi Kuu, zikiwamo zile kongwe na kubwa, Simba, Yanga na Azam FC.

Tunahitaji sana upinzani huu ili kuzidi kupandisha hadhi ya soka la Tanzania kwani pamoja na kutajwa kuwa linashika nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu, lakini bado limekuwa la farasi wawili ambao ni Simba au Yanga ambao si tu kwamba zimekuwa zikipokezana ubingwa tangu msimu wa 2013/14, pia timu zingine ukiondoa Azam FC, zimekuwa hazioneshi hata dalili ya kusaka ubingwa.

Safari hii tumeona Singida Black Stars ikionesha imeingia kwenye kinyang'anyiro cha kusaka ubingwa, ikiungana na Azam FC, hivyo kuwa na angalau timu nne zenye uzani wa juu.

Tunatarajia ushindani huu utazidi kuongezeka kadri ligi itakavyozidi kusonga mbele kiasi cha kuvutia zaidi, kusisimua kiasi kwamba msimu ujao wadhamini wengi wanaweza kujitokeza kwa wingi zaidi kuwekeza fedha zao na ligi kuendelea kupata umaarufu.