KUMEKUWAPO na ongezeko kubwa la watoto wa mitaani wanaolala nje ya maduka usiku nchini hasa kwenye majiji mkubwa.
Hilo limemshtua Mbunge wa Kilombero, Abubakar Assenga, akalizungumza bayana bungeni wakati akichangia Maendeleo ya Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/26.
"Watoto wanakwenda mitaani na yatima wamezidi, hivi sasa tuna utamaduni wa kujenga vituo vya kulelea yatima na hatulei watoto yatima kwenye nyumba zetu. Hatuwezi kufikia maendeleo ya kweli, kama tunaongeza watu kiholela kwa namna hiyo," alisema.
Hilo la mbunge huyu, limenisukuma kuongea vitu ambavyo siku zote nilikuwa najiuliza kama yeye.
Serikali kwa kiasi chake imekuwa ikijitahidi sana kudhibiti watoto wa mitaani, kwa kuwachukua na kwenda kuwalea kwenye vituo vyao.
Taasisi za kidini, pia zimekuwa mstari wa mbele kuisaidia serikali, kwani zimekuwa zikiwatwaa watoto hao kuwapeleka kwenye vituo vilivyopo kwa ajili ya kuwahudumia ya msingi.
Wanawapa elimu, wanawajenga kisaikolojia, burudani wanapata na stadi za kazi, ili kuwafanya wajione wapo kama binadamu wengine wa kawaida.
Kumbuka watoto hawa wa mitaani au yatima wanakuwa wameathirika kisaikolojia, pale wanapoona wenzao wana wazazi lakini wao hawana, wametelekezwa, au kukimbia makwao kutokana na sababu mbalimbali.
Lawama kubwa hapa ziende kwenye familia. Matatizo makubwa ya yote haya yanasababishwa na familia, ambazo ndizo zimewapata hawa watoto katika mazingira ambayo hajaandaliwa na kuleta tabu.
Kingine ni kwamba, jamii zetu za sasa, kuanzia familia, ndugu na marafiki kuwa wabinafsi. Miaka ya sasa watu wengi wamekuwa wabinafsi sana tofauti na wa zamani.
Hayo yote ndiyo wamesababisha kuongezeka kwa watoto wa mitaani. Ngono zembe zinasababisha kupatikana kwa watoto wasiotarajiwa, ambao wazazi wa pande zote mbili baba na mama kwa sababu hawajajiandaa, wanashindwa kuwapa malezi mema.
Mwanaume anaweza kuikataa mimba, au kumtoroka mwanamke ambaye naye hata kama akikifungua anashindwa kulea mtoto wake na mara nyingi mtoto wa kike anakuwa ametengwa na familia.
Mateso ya walezi hasa ambao wameachiwa jukumu la kulea baada ya wazazi kufariki, yanasababisha watoto kukimbia na kuingia mtaani ambako wanaona wapo salama.
Wengine wanakuwa wamefukuzwa na walezi wao, hasa ndugu za baba na mama zao baada ya wazazi yao kufariki.
Zamani ndugu akifariki, jukumu la malezi linakuwa kwa ndugu ambao walikuwa wakipeana majukumu ya kuwalea watoto kwa mpangilio ambao wao waliona unafaa.
Acha ndugu, hata marafiki na majirani kipindi cha nyuma walikuwa wanaweza kuwatunza na kuwalea watoto ambao wazazi wake wamefariki, kiasi kwamba hawataki mwingine kujua kama hawana wazazi.
Ubinafsi wa kizazi cha sasa kukumbatia familia zao pekee, pamoja na dai la ugumu wa maisha, umewafanya wengi kushindwa kuwasaidia watoto wa mitaani, yatima wanaolala nje ya maduka na chini ya madaraja.
Ni wakati sasa wa kila mmoja kuchukua nafasi yake kifalsafa na kimatendo. Serikali na taasisi ya dini ziendelee kulea watoto, lakini huku kwenye ngazi ya familia, watu waache ngono zembe, ili kuepuka kuongezeka kwa watoto wa namna hiyo. Pia, jamii zisikwepe majukumu yao, kwani kulea watoto hao wa ndugu, jamaa na marafiki ni wajibu wao wa msingi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED