Tanzania inahitaji masoko ya kimataifa

By Mhariri Mtendaji , Nipashe
Published at 10:19 AM Nov 08 2024
Eneo Huru la Biashara (AfCFTA).
Picha:Mtandao
Eneo Huru la Biashara (AfCFTA).

MACHI 21, 2018, nchi za Afrika zilisaini mkataba wa makubaliano ya Eneo Huru la Biashara (AfCFTA), ambalo linakadiriwa kuwa na watu zaidi ya bilioni 1.2 na pato la dola za Marekani trilioni 2.5 kwa mwaka.

Vipo vigezo ambavyo vitawawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kulifikia soko hilo na masoko mengine ya kimataifa ambayo yanaruhusu nchi nyingine kuuza huduma na bidhaa zake nchini.

Moja ya kigezo ni kuwa na biashara iliyosajiliwa ambayo inatunza kumbukumbu zake za kifedha, mauzo, ununuzi, uzalishaji (kwa wenye viwanda), na namna wafanyabiashara wanavyozingatia ajenda ya dunia ya maendeleo endelevu kwa sekta zote.

Hapa nchini, zipo mamlaka na taasisi zinazoratibisha masuala ya biashara na kuthibitisha uhalali wake, ambazo ni muhimu wananchi wazitumie kikamilifu ili AfCFTA na masoko mengine yawanufaishe Watanzania.

Moja ya taasisi hiyo ni Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), ambayo inasajili kampuni, majina ya biashara, nembo za biashara, leseni za viwanda, miliki ubunifu na uvumbuzi (hataza).

Takwimu za BRELA zinaonyesha kwamba ni Watanzania wachache wanaomiliki biashara changa, ndogo na za kati wanaoona umuhimu wa kuzisajili. Kibaya zaidi ni kwamba ni wavumbuzi wachache zaidi, wanaojisajili kwa wakala huo.

Jambo la kusikitisha ni kwamba gharama za kujisajili zinahimilika ukilinganisha na hasara ambayo mtu anaweza kuipata kwa kutoilinda biashara yake kisheria.

Mathalani, kiwanda kidogo chenye mtaji wa chini ya Sh. milioni 10, kinachosindika unga, viungo au kinazalisha mafuta kinasajiliwa kwa Sh. 50,000 inayolipwa mara moja tu katika uhai wake wote.

Kwa wavumbuzi, ada ni Sh. 22,000 inayolipwa kwa awamu mbili na Sh. 4,000 kila mwaka baada ya kusajiliwa. Hiki ni kiasi kidogo ambacho bila shaka, Mtanzania mwenye nia ya kufanyabiashara kwa uaminifu, anamudu kuilipa.

Kama tunavyofahamu, mazingira ya Afrika kwa maana ya changamoto zinazoikabili jamii zinafanana kwa kiasi kikubwa; inasikitisha kuona mtu anabuni kitu kinachoweza kutatua changamoto kwenye jamii, anakiweka mtandaoni, anakipa na jina, bila kulinda jina wala uvumbuzi wenyewe.

Hali ni hiyo hiyo wakati wa maonyesho ya biashara kama ya Kimataifa ya Sabasaba ambayo yako mbioni kuanza; unakuta mbunifu anaeleza hatua kwa hatua namna alivyofanikiwa kubuni zana fulani ya kuwasaidia wakulima au wananchi katika sekta muhimu, baada ya maonyesho hanufaiki na ubunifu wake kwa kuwa wajanja wachache wanaamua kwenda kuisajili BRELA na kuanza kuizalisha. Hii ni hasara sio kwake pekee bali kwa nchi pia.

Mpango wa serikali wa kuboresha mazingira ya biashara nchini umeweka njia rahisi za kujisajili ambayo ni kupitia mtandao (ORS), unapata huduma zote za kurasimisha biashara yako ukiwa sehemu yoyote yenye intaneti.

Tunaeleza haya ili kuukumbusha umma kwamba wajasiriamali wetu wanaweza kuzalisha bidhaa nzuri, kutoa huduma bora, tukajitangaza mtandaoni lakini mwisho wa siku, tutakuta kile tunachouza kimelindwa kisheria na mtu mwingine; ambaye atakuruhusu kuendelea kutumia nembo au jina ulilobuni, kwa kumlipa mamilioni ya fedha kwa kuwa tu ameshajisajili.

Sheria itamlinda ambaye ameitii. Hata kama utakuwa mwanzilishi wa huduma, jina, uvumbuzi au nembo, usipoisajili halafu akatokea mgeni akaisajili nchini, hutaweza kujitetea kwa sababu hutambuliki kwenye mifumo ya kisheria.