BINTI WA YOMBO: Hatima ya 'afande' kujulikana leo

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 11:23 AM Oct 15 2024
Wakili Peter Madeleka akiwa ofisini kwake.
Picha: Mtandao
Wakili Peter Madeleka akiwa ofisini kwake.

MAHAKAMA ya Wilaya ya Dodoma leo inatarajiwa kutoa uamuzi wa maombi ya Wakili Peter Madeleka ya kukamatwa na kuwekwa rumande Fatma Kigondo, maarufu afande, mshtakiwa katika kesi ya kuwatuma vijana kumbaka na kumwingilia kinyume cha maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Saalam.

Hatima ya mshtakiwa huyo inatarajiwa kujulikana leo kama mahakama hiyo itatoa amri ya kukamatwa kwake na kuwekwa rumande kama ilivyokuwa kwa washtakiwa wengine kwa ajili ya usalama wake.

Wakili wa upande wa mlalamikaji Peter Madeleka alitoa maombi hayo Oktoba 7 mwaka huu katika Mahakama ya Wilaya Dodoma.

Madeleka aliomba mahakama hiyo kutoa amri ya kumkamata na kumweka rumande mshtakiwa huyo kwa ajili ya usalama wake kama ambavyo ilifanya kwa washtakiwa wengine.

Fatma anakabiliwa na shtaka la kubaka kwa kundi kinyume cha kifungu cha 131 A (2) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura 16, ambacho kinaelekeza kuwa ni kosa kisheria kuwasaidia wahalifu kutenda kosa la ubakaji, afande huyo akidaiwa anahusika na ukatili wa ubakaji wa kundi.

Kesi hiyo ambayo ilipangwa kusikilizwa Oktoba 7, mwaka huu, lakini iliahirishwa hadi leo baada ya mshtakiwa kutofika mahakamani kwa madai kuwa ni mgonjwa.

Wakili Madeleka akiwasilisha maombi hayo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, Nyambuli Tungaraja, akidai mahakama itoe amri ya kukamatwa kwa Fatma na kumwekwa rumande katika Gereza la Isanga jijini hapa.

Wakili Madeleka alidai anaiomba mahakama hiyo kutoa amri hiyo ili mshatakiwa huyo akamatwe mara moja na kunyimwa dhamana kama ilivyokuwa kwa washtakiwa wengine.

Wakali wa Mlalamikiwa, Sedrick Mbunda alidai mteja wake hakufika mahakamani kutokana na kuwa mgonjwa na kuiomba mahakama impangie siku nyingine ya kusikiliza shauri hilo.

Ni hoja iliyopingwa na Wakili Madeleka ambaye alihoji kuwa kama mshtakiwa huyo ni mgonjwa, kwanini wakili huyo hakuwasilisha ushahidi wa daktari mbele ya mahakama hiyo.

“Kama anaumwa lazima wangeleta ushahidi wa daktari kama ambavyo wanatakiwa kufanya kwa mujibu wa sheria, lakini hii kusema tu mtu anaumwa, si kazi ya mahakama kubaini kama mtu anaumwa kweli au haumwi, walipaswa kuleta ushahidi wa kimatibabu hapa si kuzungumza tu," alidai Wakili Madeleka.

Hakimu Tungaraja aliahirisha shauri hilo hadi leo kwa ajili ya hoja hizo kutolewa uamuzi.