BBT uvuvi yaanza kulipa vijana wafugaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:28 PM Oct 15 2024
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, akionesha sehemu ya samaki waliovunwa kwenye vizimba vya ufugaji samaki.

MAONO ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuwezesha vijana kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT) yameanza kuzaa matunda baada ya kuwezeshwa kufuga samaki kwenye vizimba jijini Mwanza na kuanza kuvuna.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alisema hayo aliposhiriki awamu ya kwanza ya uvunaji samaki aina ya sato uliofanywa na Kikundi cha Vijana cha TWIHAME kinachofanya shughuli zake za ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba katika eneo la Kisoko, Kata ya Luchelele, wilayani Nyamagana jijini Mwanza, mwishoni mwa wiki.

Akizungumza baada ya kushiriki uvunaji, Waziri Ulega alimshukuru Rais Dk. Samia kwa kutoa Sh. bilioni 2.2 na kuviwezesha vikundi 11 vya vijana kufanya ufugaji wa samaki katika eneo la Kisoko na kuwekeza vizimba zaidi ya 100 katika eneo hilo. 

“Leo katika kizimba hiki kimoja tu ambacho watavuna samaki takriban 4,000, vijana hawa watapata kiasi cha shilingi zaidi ya milioni 30, inaleta matumaini makubwa sana, na mwitikio wa uwekezaji katika Ziwa Victoria kupitia vizimba ni mkubwa sana, mwitikio huo utasaidia kupunguza masuala ya uvuvi haramu kwa sababu wavuvi wanakwenda kuwa na kazi mbadala,” alisema.

Mmoja wa wanufaika wa vizimba, ambaye pia ni Katibu wa wanufaika, Wilaya ya Nyamagana, Omary Mangu, alimshukuru Rais Dk. Samia kwa kuwawezesha mkopo ambao hauna riba ili waweze kufanya shughuli za kufuga samaki na matunda ya mkopo huo wameanza kuyaona.

Septemba 25, 2024, Vijana wa Kikundi kingine kinachojulikana kwa jina la Nguvu Kazi walianza kuvuna tani 13.37 kutoka katika vizimba sita na baada ya kuwauza walifanikiwa kupata zaidi ya Sh. milioni 100.

Januari 30, mwaka huu, akiwa jijini Mwanza, Rais Samia alizindua mradi wa vizimba 222 na boti 160 kwa ajili ya kuwakopesha wavuvi nchi nzima ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija na kuboresha kipato chao.