Nishati safi ya kupikia itaondoa kadhia za kuni, mkaa kwa wenye nmahitaji maalum-Ummy

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:14 PM Oct 15 2024
Naibu Waziri Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiananga.

Naibu Waziri Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiananga amesema kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yanaenda kuwaokoa watu wenye mahitaji maalum na kadhia zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia ikiwemo kuni na mkaa.

Amesema kadhia hizo wanazipata nyakati za utafutaji na utumiaji wa nishati hizo zisizo safi za kupikia ambazo hutoa moshi mwingi unaoleta pia athari kwenye mfumo wa upumuaji.

Nderiananga ameyasema hayo jijini Dodoma wakati alipokuwa akihamasisha wananchi kupika kisasa kwa kutumia nishati safi ya kupikia kupitia programu ya Pika Kisasa inayoendeshwa na Wizara ya Nishati.

"Natoa rai kwa jamii kuwa na mtazamo chanya juu ya nishati safi ya kupikia ili kuongeza kasi ya matumizi ya nishati hii nchini." amesema Nderiananga

Ameongeza kuwa, Viongozi katika ngazi mbalimbali nchini wataendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa vitendo na hii inajumuisha Wabunge wanawake  nchini kuwa na programu maalum ya kuelimisha jamii majimboni.

Akizungumzia mazingira, amesema faida mojawapo ya nishati safi ya kupikia ni uhifadhi wa mazingira utakaopelekea mvua kupatikana kwa wakati.

Ametaja faida  nyingine ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kuwa ni jamii kuondokana na magonjwa yanayotokana na matumizi ya nishati isiyo safi  ikiwemo athari katika  mapafu  inayopelekea tatizo la upumuaji.