Wazazi, walezi wadaiwa kukwamisha vita ya rushwa ya ngono

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 01:22 PM Oct 15 2024
Wadau wakiwa katika maandamano ya maadhimisho hayo.
Picha: Sabato Kasika
Wadau wakiwa katika maandamano ya maadhimisho hayo.

WAZAZI na walezi wametupiwa lawama kwa kukwepa kutoa ushirikiano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto.

Lawama hizo zimetolewa na Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Kinondoni Dar es Salaam, Furaha Dibango, katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike Duniani.

Maadhimisho hayo yaliyoambatana na mwendelezo wa awamu ya sita ya kampeni ya 'Safari Salama Bila Rushwa ya Ngono' Inawezakana', yaliandaliwa na Shirika la Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI) na kufanyika  Bunju A.

Furaha amesema Manispaa hiyo inashirikiana na wadau mbalimbali kupambana na ukatili wakiwamo WAJIKI, lakini juhudi hizo zinakwamishwa na baadhi ya wazazi na walezi.

Taarifa za ukatili zinatolewa, tunafuatilia na kubaini ukweli na kufikisha matukio katika vyombo vya sheria, lakini wanapoitwa kuja kutoa ushahidi hawajitokezi," amesema Furaha.

Amesema badala yake, wamekuwa wakimalizana na wahalifu, na kwamba mtindo unakwamisha vita ya rushwa ya Ngono.

"Wito wangu kwa wazazi na walezi ni kwamba wawe mstari wa ,Mbele kutoa ushirikiano ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Ofisa wa TAKUKURU, Bibie Msumi akizungumza katika maadhimisho hayo.
Mkurugenzi wa WAJIKI, Janeth Mawinza amesema wameanza awamu ya sita ya  kampeni ya 'Safari Salama Bila Rushwa ya Ngono' ambayo itadumu kwa miaka miwili.

"Wafadhili wetu ambao ni Women Fund Tanzania Trust (WFT), wametuwezesha Sh. milioni 800 kwa ajili ya kampeni hii ambayo tumeongeza kata tatu za Bunju, Tandika na Kitunda," amesema Janeth.

Amefafanua kuwa wakifanya kampeni kwenye baadhi ya kata za wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke, na kwamba awamu hiyo ya sita wameongeza kata hizo tatu.

Lengo letu kama tutapata uwezo zaidi wa kifedha, ni kuimaliza Dar es Salaam yote na kisha kwenda mikoani ambao ninaamini Kuna tatizo la rushwa ya ngono' " amesema.

Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU), mkoa wa Kinondoni, Bibie Msumi anasema, mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika vita vya ukatili wa kijinsia ni mkubwa.

"Kwa sasa jamii umepata uelewa wa kutosha kupitia elimu inayotolewa na mashirika hayo, wamekuwa walitoa taarifa za matukio ya ri'ushwa ya ngono ambazo zinatusaidia katika majukumu yetu," amesema Bibie.

Ofisa Maendeleo ya Jamii, Furaha Dibango akielezea hofu kuhusu wazazi na walezi kukwepa kutoa ushirikiano katika kesi za ukatili wa kijinsia.