KAMANDA MSSIKA: Kutoka fundi gereji hadi msaidizi wa IGP

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 12:00 PM Oct 15 2024
Picha tofauti za Kamanda Abdallah Mssika.
Picha: Nipashe Digital
Picha tofauti za Kamanda Abdallah Mssika.

MARUFUKU kukata tamaa! Jaribu kufikiria kuhusu hili: Alianzia kwenye mafunzo ya ufundi gereji, juhudi zake katika safari ambayo hakuwa na uhakika wa hatima yake, zikambeba hadi kuwa afande mwandamizi katika Jeshi la Polisi, hata kuwa Msaidizi wa Mkuu wa jeshi hilo, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).

Kamanda Abdallah Mssika aliyelitumikia Jeshi la Polisi kwa miaka 40 akishika nyadhifa mbalimbali, leo anasimulia milima na mabonde aliyopitia maishani tangu akiwa na umri wa miaka 15 hadi kustaafu kwake jeshini.

Kamanda Mssika aliwahi kuwa Mkuu wa Polisi (OCD) Wilaya ya Kinondoni, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mara, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mwanza na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dodoma.

Mstaafu huyo aliyewahi kuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, pia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ni miongoni mwa makamanda waanzilishi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam mwaka 2006.

Pia amewahi kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera na baadaye kuwa Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi hadi alipostaafu utumishi kwa umri wa lazima mwaka 2010.

Katika mazungumzo maalum na mwandishi wa habari hii yaliyofanyika Septemba 15 mwaka huu, mkoani Dar es Salaam, Kamanda Mssika anasimulia alivyoshindwa kuendelea na elimu ya sekondari baada ya baba yake kufariki dunia.

Anasema kifo cha baba yake kilibadili safari yake kimasomo, mama yake mzazi akilazimika kumpeleka kwa Mkuu wa Wilaya wa Iringa Mjini ili kumwomba msaada.

Ilikuaje? Kamanda Mssika anasema kuwa tofauti na watoto wengine, katika utoto wake hakuwahi kufikiria angetamani kuwa nani akiwa mkubwa.

"Nimesoma shule mbili hadi kuhitimu darasa la nane. Nilianza masomo Shule ya Ilole na baadaye kumalizia Shule ya Malangali, Iringa.

"Nikiwa darasa la sita, baba yangu alifariki dunia na kwa msaada wa kaka yangu mkubwa (Adam Mssika) nilihamishiwa Shule ya Malangali na kumaliza darasa la nane. Sikuendelea sekondari.

"Nikiwa na umri wa miaka 15, mama yangu alinichukua na kunipeleka kwa DC (Mkuu wa Wilaya) kumwomba msaada kwa sababu sina baba, anisaidie kuendelea sekondari au anitafutie kitu cha kufanya," anasimulia.

Kamanda Mssika anasema kuwa baada ya kumpeleka kwa DC, mama yake aliondoka na hivyo Mkuu wa Wilaya alikwenda kumkabidhi kwa fundi mkuu katika moja ya gereji iliyokuwa mjini Iringa wakati huo, ili kujifunza ufundi. Alikaa hapo hadi mwaka 1966 alipokimbilia Dar es Salaam.

MSHAHARA SH. 166

Anasema alipofika Dar es Salaam, alifikia kwa ndugu yake na katika kipindi cha mpito cha kutafuta ajira, alikwenda kujiandikisha Idara ya Kazi na mwezi Agosti mwaka huo (1966), alipata ajira ya muuguzi msaidizi katika Hospitali ya Muhimbili kwa mshahara wa Sh. 166.

"Nilifanya kazi wodi ya Kibasila. Nilifanya pale hadi mwaka 1970 na wakati wa likizo nikiwa Moshi, Kilimanjaro kwa kaka yangu Adam ambaye alikuwa trafiki, alinishawishi kuacha kazi ya uuguzi ili kuingia Jeshi la Polisi.

"Haikuwa kazi rahisi kuacha uuguzi kisha kwenda polisi kwa sababu tayari nilikuwa nimepata mafunzo ya uuguzi na nilikuwa katika hatua ya kubadilishiwa nafasi ya awali.

"Alimshirikisha pia baba yetu mdogo ambaye naye alinieleza umuhimu wake, ndipo Machi 17, 1970, nilijiunga rasmi Jeshi la Polisi na kupata mafunzo Chuo cha Usalama (Chuo cha Polisi Moshi - CCP).

Kamanda Mssika anasema kuwa baada ya kuhitimu mafunzo, alipangiwa mkoani Arusha na kuanza kazi za doria, kipindi hicho matukio makubwa yalihusisha wizi wa majumbani na mengine yaliyokuwa yakichunguzwa na ofisi za upelelezi.

Anasimulia kuwa baadaye alihamishiwa Dar es Salaam na miongoni mwa kazi alizofanya ni pamoja na kuwa dereva, akifanya kazi kama msaidizi.

"Nikiwa dereva, wakati maofisa wa polisi upelelezi wa makosa ya wizi wa kalamu au kughushi walikuwa wakitoka kwenda kufanya kazi zao, niliambatana nao.

"Yote niliyokuwa ninafanya sikuwa na uelekeo, lakini kupitia fursa mbalimbali zilizokuwa zinakuja mbele yangu na nikiangalia nilikotoka, nikawa ninaona ni nguvu zangu mwenyewe kunipeleka ninakotaka.

"Kulinganisha Dar es Salaam na Arusha nilikoanzia kazi, ofisi hii ilikuwa inashughulika na uhalifu wa aina zote. Wizi wa kalamu, matukio yalikuwa mengi wakati ule.

"Hivyo, nilivyokuwa nikitoka na wapelelezi wakifika eneo la tukio, badala ya kuwasubiria kwenye gari, nilipenda kuambatana nao, wanapohoji ninasikiliza, wakiandika maelezo ya mashahidi ambayo niliona ni rahisi kuliko ya watuhumiwa, nilikuwa ninaangalia hivyo ikafika wakati nikawa ninapewa fursa ya kuandika maelezo ya mashahidi," anasema.

Kamanda Mssika anasema kitendo hicho kilimpa uzoefu kujua wapi anakosea ili kurekebisha na mwaka 1975, alihamishwa kutoka Ofisi ya Mpelelezi Mkoa kwenda Makao Makuu ya Upelelezi na majukumu mengine yakawa kitengo cha makosa ya binadamu na vitendo vinavyohusisha wizi.

KESI YA UHAINI

Kamanda Mssika anasema kutokana na uzoefu mkubwa aliopata, mwaka 1976 kulitokea kesi ya kwanza ya aina yake iliyomhusu mtendaji mwandamizi wa ulinzi na usalama wa nchi, Juma Thomas Zangira, aliyedaiwa kusaliti taaluma yake na nchi.

"Nikiwa makao makuu ya upelelezi, niliitwa na viongozi wangu wakuu na kunijulisha kwamba, nimeteuliwa katika timu ya wapelelezi Idara ya Usalama ya Taifa, ikiwa imeandaa operesheni maalum ya kumfuatilia tabia na mwenendo wa Zangira.

"Wakati huo nilikuwa kijana mwenye umri wa miaka 26 tu. Nipo Idara ya Upelelezi na cheo cha sajenti na ni mpenzi wa filamu hasa za kiupelelezi James Bond. Umeaminiwa na kupewa kazi hiyo, unakula kiapo mbele ya jopo.

"Sikufika sekondari, lakini katika utumishi wangu ndani na nje ya Jeshi la Polisi baada ya kustaafu, nimeingia katika taasisi ninapewa majukumu nyeti kupitiliza.

"Ilibidi kumfahamu mtuhumiwa anakaa wapi, alikuwa Mtaa wa Nkurumah (Dar es Saalam). Operesheni ikaanza, ikabainika mawasiliano, alikuwa anatoa siri akiwa ofisa mpelelezi wa juu aliyefunzwa kutoka taasisi mbalimbali za kiusalama nchi mbalimbali na ni kachero.

"Alikuwa ameandaliwa ofisi ya kuendesha majukumu yake ya kazi, ilikuwa (anataja moja ya hoteli kubwa iliyoko katikati ya jiji la Dar es Salaam)," anasimulia.

Kamanda Mssika anasema kuwa wakati huo kulikuwa na matatizo ya kampeni ya ukombozi nchi za kusini mwa Afrika na Tanzania ikiiongoza.

"Wengi walitaka kujua siri, namna Tanzania inavyofanya, ndio wakampata yeye (Zangira) na akawa anafanya kazi hiyo.

"Operesheni iliyofanyika ilikuwa ni mwendelezo kujua nini kinachofanyika? Nani anakifanya? Anakifanyaje? Akishirikiana na nani? Na kina nani?" anasema.

IDI AMINI

Kamanda Mssika anasema moja ya matukio yaliyotokea akiwa mafunzoni Chuo cha Polisi Kurasini, Dar es Salaam, wakati huo wakiwa likizo, Rais akatangaza wanaingia vitani, wakiwamo askari polisi.

"Tulitangaziwa tukarudi chuoni, ndipo tukakuta magari ya kutupeleka vitani. Amri ni utii. Tukatoka Dar es Salaam hadi Monduli, Arusha, tukapata mafunzo ya medani kivita ndipo hatimaye tukapelekwa mstari wa mbele tukianza Kagera na hatimaye kuvuka mpaka kuingia Uganda.

"Mimi baada ya kufika Monduli na kwenda Kagera, nilikuwa kikosi ambacho hatimaye nilibidi nichukuliwe na kuwekwa kitengo cha intelijensia kwa kuangalia wasifu wangu wa kufanya kazi katika ofisi za upelelezi za wilaya, mikoa na hali kadhalika Makao Makuu ya Upelelezi Tanzania (DCI)," anasimulia.

Kamanda Mssika anasema alikwenda na wasifu ambao ulimwaminisha kutoka kuwa askari wa miguu wa kawaida na kuingia kitengo hicho kama Msaidizi wa Mkuu wa Intelijensia wa Kikosi.

Anasimulia kuwa baada ya kuteka Kampala, kikosi chao kilipewa majukumu ya kwenda uwanja wa ndege ndogo wa mafunzo ya marubani wa kawaida katika Mji wa Soroti, kaskazini mwa Uganda na kumaliza operesheni. Mwaka 1979 walirejea nyumbani Tanzania.

*KESHO USIKOSE MOTO WA CHEO IGP NA MAZITO MATATU HATOSAHAU