Dodoma Jiji yaanza kuiwinda Coastal

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:44 AM Oct 15 2024
Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Nizar Khalfan.
Picha: Mtandao
Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Nizar Khalfan.

BAADA ya mapumziko ya Kalenda ya FIFA, Dodoma Jiji FC imeanza mazoezi kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union utakaopigwa Ijumaa ijayo Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, uwanja ambao wapinzani wao wameuchagua kuwa wa nyumbani.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Nizar Khalfan, amesema jana kuwa kikosi hicho kimeanza mazoezi kwa kazi moja tu kuhakikisha wanashinda mchezo huo ili kuelekea kwenye malengo waliyojiwekea ya kucheza mechi za kimataifa msimu ujao.

"Tulipata mapumziko ya siku kama tatu nne hivi, tumerudi kuendelea pale tulipoachia, nakumbuka mechi ya mwisho tulishinda na hii tunakwenda kucheza ugenini dhidi ya Coastal Union kwa hiyo tunajiandaa vizuri.

"Michezo saba tuliyocheza bado haijatuharibia malengo, yako pale pale kuhakikisha msimu ujao tunacheza mechi za kimataifa kwa kushika nafasi nne za juu," alisema.

Katika michezo hiyo, Dodoma Jiji imekusanya pointi tisa, ikishinda miwili, sare tatu na kupoteza miwili, ikikamata nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hata hivyo, alisema wamerejea wakiwa hawana baadhi ya wachezaji ambao ni majeruhi, lakini wanaendelea vizuri na siku mbili tatu watajumuika na wenzao.

"Tuna Ibrahim Ajibu alipata majeraha katika mchezo dhidi ya Simba, halafu kuna nahodha wetu, Hassan Mwaterema naye ni mgonjwa, lakini hawa wote hali zao zinaendelea vizuri, tunaamini mpaka Ijumaa watakuwa wameungana na wenzao, hata kama hawakucheza mechi dhidi ya Coastal Union, basi watacheza mchezo unaofuata dhidi ya JKT Tanzania, Oktoba 29.

Katika mchezo wao wa mwisho kabla ya mapumziko, Dodoma Jiji iliishindilia Tabota United mabao 2-0.