Samia ataka uchaguzi Serikali za Mitaa usichukuliwe poa

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 01:55 PM Oct 15 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kutokuchukulia poa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu na kuwa ndio utaleta taswira nzima ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Alitoa kauli hiyo jana jijini Mwanza wakati wa maadhimisho ya kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru na kueleza ni fursa kubwa ya kukuza demokrasia na ushiriki katika maendeleo ya jamii.

“Kama vijana wanavyosema ‘tusiuchukulie poa’ ni uchaguzi kama uchaguzi mwingine, ni uchaguzi unaotupa taswira jinsi mambo yatakavyokuwa kwenye uchaguzi mkuu wa 2025 hivyo niendelee kuwasihi wananchi wote wenye sifa kuhakikisha wanashiriki kwenye uchaguzi huu muhimu,” alisema Samia.

Aliwataka kutofautisha kati ya orodha ya wapigakura inayotumika katika kupiga kura uchaguzi wa serikali za mitaa (Daftari la Wakazi) pamoja na Daftari la Kudumu la Wapigakura ambalo hutumika katika uchaguzi mkuu mwakani.

“Niwaombe na kuwahimiza wananchi wote twende kwenye maeneo yetu tukajiandikishe, ili kushiriki uchaguzi ujao kwani utasaidia kuonesha ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya maeneo yao sambamba na kubuni, kusimamia na kutekeleza shughuli za kiuchumi katika ngazi ya jamii kwa maendeleo jumuishi ya watu katika maeneo husika ya kiutawala,” alisema Samia.

Aidha, alisema msingi wa kuwapo kwa ngazi za kiutawala kikatiba katika mikoa, wilaya, miji na vijiji ni kupeleka madaraka kwa wananchi na ughatuzi huo wa madaraka unaongeza ushiriki wa wananchi katika maamuzi ikiwa ni dhana ya kujitawala.

MAZINGIRA

Kuhusu uharibifu wa mazingira, Rais Samia alisema hali ya uchafuzi imekuwa tatizo nchini pamoja na ulimwenguni kwa pamoja hali inayosababisha athari zake kurejea kwa kasi.

“Athari za uchafuzi au uharibifu wa mazingira zinaturudia sisi wenyewe kwa kutokea kwa mabadiliko ya tabianchi na misimu ya mvua na jua mabadiliko yanayosababisha upungufu wa mvua pamoja na mvua kupita kiasi, mvua zisizotabirika na ukame katika baadhi ya maeneo ya nchi vyote hivi vinaleta dhiki kwetu au kwa wananchi.

Kadhalika, alisema maeneo yote yaliyolalamikiwa katika mbio za Mwenge serikali itayafanyia kazi sambamba na maoni na mapendekezo ya wakimbiza mwenge kitaifa.

Kuhusu uzinduzi wa kitabu cha historia ya falsafa ya Mwenge wa Uhuru alichokizindua jana, Rais Samia alisema kitabu hicho kitasaidia kueneza na kutunza na kuendeleza historia na misingi ya Mbio za Mwenge pamoja na mchango wa vijana katika shughuli hizo.

Awali, akitoa taarifa ya Mbio za Mwenge Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, alisema Mwenge huo umekimbizwa kwa zaidi ya kilomita 37,235.62 katika mikoa 31, halmashauri 195 kwa siku 195 ukiongozwa na vijana sita wawili kutoka Zanzibar, Kigoma, Kilimanjaro, Dar es Salaam huku kiongozi wa mbio hizo akitokea mkoani Mwanza.

MAENEO KOROFI 

Akitoa ripoti ya mbio za Mwenge kitaifa, Kiongozi wa Mbio hizo, Godfrey Mzava alitaja maeneo matatu korofi yaliyobainika wakati wa mbio hizo huku akimwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuyatilia mkazo ikiwezekana yaangaziwe maeneo hayo pekee katika mbio zijazo.

Alitaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na tatizo la ukataji wa kodi za serikali katika fedha za serikali zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

“Viwango vya kodi hizi vinajulikana na ni kwa mujibu wa sheria lakini mamlaka husika hazitimizi wajibu wake wa kuhakikisha zinakatwa na kurudishwa TRA. Changamoto hii imekuwa ikiibuliwa na Mwenge wa Uhuru na imekuwa ikijitokeza katika miradi mingi inayotekelezwa hapa nchini hili ni eneo la kufuatilia kwa makini,” alisema Mzava.

Aidha, alitaja zabuni za miradi mingi ya umma kuwa zinazotolewa nje ya mfumo wa kidigitali wa manunuzi ya umma (NeST) hatua ambayo ni kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2023 pamoja na Sheria ya Ubadhirifu wa Mali ya Umma na Utoaji wa Zabuni za Umma usiyo ridhisha.

Kadhalika, alitaja eneo lingine kuwa ni pamoja na halmashauri nchini kushindwa kutumia mapato ya ndani kubuni na kutekeleza miradi ya maendeleo na kuishia kutegemea fedha kutoka serikali kuu na taasisi za umma.

Mzava alisema ni halmashauri chache tu nchini zinazotekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi kwa kutumia fedha za ndani.

Aidha, alisema halmashauri nyingi hazina maelezo yanayoridhisha kuhusu matumizi ya fedha za mapato ya ndani wanayokusanya hasa katika eneo hilo la utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.

“Ikitokea Rais akaelekeza kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2025 zishughulikie miradi inayotekelezwa na mapato ya ndani ya halmashauri zetu hapa nchini, watu watakimbia halmashauri zao,” alisema Mzava.

Aidha, alimwomba Rais kuelekeza kwa mwaka 2025 Mwenge wa Uhuru ushughulike na miradi inayotekelezwa na mapato ya ndani ya halmashauri nchini.

Suala lingine alilolitaja kuwa korofi ni pamoja na usambazaji wa nishati vijijini chini ya usimamizi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kueleza kuwa utekelezaji wake ni kero katika maeneo mengi nchini na kuomba pia eneo hilo kupewa kipaumbele zaidi katika ufuatiliaji.

“Ukielekeza hivi Rais utashuhudia maendeleo makubwa ya watu kwa muda mfupi kupitia Mwenge huu wa uhuru na itakuwa ni hatua muhimu katika kuunga mkono jitihada unazozifanya katika kujenga nchi kupitia serikali kuu kwa kishindo kikubwa saana,” alisisitiza na kukabidhi kitabu cha majumuisho ya risara za maeneo yote ulipozunguka Mwenge huo wa uhuru.

Pamoja na mambo mengine Rais Samia Suluhu Hassan alishiriki ibada ya kumbukizi ya miaka 25 ya kifo cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alitembelea na kukagua maonesho ya wiki ya vijana yaliyohitimishwa katika viwanja vya Furahisha pamoja na kuzindua kitabu cha Falsafa ya Mwenge wa Uhuru kilichoandikwa na miongoni mwa mawaziri wa kwanza Tanzania, Job Lusinde na kuhaririwa na Dk. Bashiru Ally.