Wanaorudisha nyuma maendeleo wanapaswa kuadhibiwa

By Mhariri Mtendaji , Nipashe
Published at 11:01 AM Oct 15 2024
wasiojulikana kubomoa madarasa mapya
Picha: Mtandao
wasiojulikana kubomoa madarasa mapya

TUKIO lililotokea katika Kata ya Tembela, jijini Mbeya la watu wasiojulikana kubomoa madarasa mapya yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi linarudisha nyuma maendeleo.

Wananchi wamejitolea kutumia nguvu zao kujenga madarasa hayo ili kupunguza uhaba wa vyumba vya kusomea, lakini watu wachache wasiopenda maendeleo wameamua kuyabomoa.

Tukio hilo limezua taharuki kwa sababu limefanyika usiku, ikionesha kuwa watu hao walikuwa na nia ovu ya kudhoofisha nguvu za wananchi hao.

Kwa mujibu wa mwananchi mmoja wa eneo hilo, wananchi kwa kuchangishana fedha waliamua kujenga madarasa hayo na hakukuwa na mgogoro wowote wa ardhi.

Aidha, wananchi hao waliamua kuchangishana Sh. 12,000 kila mmoja ambazo kwa sehemu kubwa zinatokana na biashara ya mazao wanayolima.

“Kitendo hichi kimetushtusha sana, sisi hatuna vyanzo vikubwa vya mapato zaidi ya kilimo ambacho ni cha msimu, tumeshindwa kuelewa hawa watu wana nia gani kwa sababu hapa hapana mgogoro wowote wa ardhi kwamba useme ndio unaosababisha,” anasema mmoja wa wananchi hao.

Ukitafakari matukio kama hayo yanafanywa na watu wasio na nia njema na wanaopenda kuona kila mara kukitokea migogoro na vurugu ili kuharibu amani iliyopo.

Watu waliofanya tukio hilo wana nia ovu ya kudhoofisha harakati za wananchi wapenda maendeleo wanaopenda kuona nchi yao ikisonga mbele katika sekta ya elimu.

Kama wakulima wameamua kuchanga sehemu ya mapato yao ili yaweze kujenga madarasa ya kusomea watoto wao, na pengine hata hao walioshiriki kuyabomoa kuna watoto wao ambao wangesoma kwenye madarasa hayo, lakini wameamua kufanya uovu huo bila kufikiri siku za usoni yatakuja kusaidia vizazi vyao.

Matukio yenye kuashiria uvunjifu wa amani yanapotokea katika eneo moja kila wakati, yanafanya watu wajiulize kulikoni, hata kama kuna kitu hakiko sawa njia nzuri ni kukaa pamoja na kufikia mwafaka, lakini si njia ya kufanya uharibifu wa miundombinu ambayo itakuja kusaidia vizazi vya sasa na vya baadaye.

Kwa mujibu wa kiongozi mmoja wa eneo hilo, awali lilianza kubomolewa jengo la mtaa wa Tembela na baadaye likabomolewa jengo la mtaa wa Relini na kwamba majengo hayo yalibomolewa kwa siku tofauti.

Ilidaiwa kuwa mwanzo wananchi walifikiri jengo walilolikuta limebomoka, walifikiri limejengwa chini ya kiwango, lakini lilivyobomolewa la pili wakajua kuna watu wenye nia ovu walioshiriki kufanya uharibifu huo.

Wanaofanya vitendo hivyo vya uharibifu wanapaswa wajitafakari badala ya kufanya uamuzi ambao hauna tija na kudidimiza kasi ya wananchi wanaopenda maendeleo ya nchi yao.

Ndio maana kuna haja ya watu kwenda kupima afya ya akili ili kujitambua kama wako sawa. Kwa sababu mwenye afya ya akili iliyo sawa hawezi kuchukua uamuzi huo usio na tija.

Serikali inafanya juhudi kuhakikisha shule zinakuwa na madarasa ya kutosha ili kila mtoto anayekwenda kupata elimu, anaipata katika mazingira yaliyo bora.

Na kwa kuitikia wito huo wa serikali, wananchi wameamua kujitolewa nguvu zao kuanza ujenzi wa madarasa kwenye maeneo ambayo bado hayajafikiwa na bajeti, ili yatakapofikiwa bajeti imalizie mambo mengine.

Lakini, waliofanya uharibifu huo ni lazima wasakwe na kuchukuliwa hatua.