DR Congo inafungika, Stars kazeni buti twende AFCON

Nipashe
Published at 09:15 AM Oct 14 2024
Taifa Stars
Picha:Mtandao
Taifa Stars

KESHO Jumanne Timu ya Taifa (Taifa Stars), inatarajia kushuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salam kuikaribisha Timu ya Jamhuri ya Kidemorasia ya Congo (DR Congo), katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025).

Mchezo huo ni wa Kundi H, ambalo mbali ya Tanzania na DR Congo pia zimo Ethiopia na Guinea ambazo zilicheza mechi yao ya raundi ya tatu juzi na wenyeji wa mechi hiyo, Waguinea wakashinda mabao 4-1.

Ushindi huo unaifanya Guinea kufikisha pointi tatu na kujiimarisha kwenye nafasi ya tatu nyuma Stars yenye alama nne, huku vinara wa kundi hilo wakiwa ni DR Congo yenye pointi tisa na Ethiopia ikiburuza mkia kwa alama yake moja.

Hivyo, ushindi wa aina yoyote kwa Taifa Stars kesho ni muhimu sana, ili kujiweka katika njia sahihi ya kufuzu kwa mara ya nne kushiriki fainali hizo zitakazofanyika baadaye mwakani nchini Morocco.

Hii ni baada ya kutoka sare mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya Ethiopia na kwenda kushinda ugenini dhidi ya Guinea, hivyo bado itakuwa na kibarua kigumu ugenini kwa Wahabeshi.

Mechi nyingine ambayo itakuwa ni muhimu pia kwa Taifa Stars ni pale itakapowakaribisha nyumbani Guinea.

Kama Stars itapambana na kushinda dhidi ya DR Congo kesho, itafikisha pointi saba ama ikishindikana na kuambulia angalau sare itakuwa na alama tano, hivyo kuzidi kuongeza pengo kubwa dhidi ya wapinzani wao Guinea.

Ikumbukwe katika kila kundi kati ya makundi 12, vinara wawili watafuzu kushiriki fainali hizo, hivyo mpaka sasa DR Congo inahitaji pointi moja tu kufuzu na kuacha mbio kubwa kwa Tanzania na Guinea kuwania nafasi moja itakayobakia kutoka katika Kundi H.

Kwa maana hiyo kinachotakiwa kwa Stars ni kushinda kesho, ili kupunguza kucheza kwa presha kubwa katika mechi zake mbili za mwisho hususan itakapokutana na Guinea ambao wanafukuzana kuwania nafasi hiyo moja.

Sisi kama wadau namba moja wa sekta ya michezo nchini, tunaamini inawezekana kwa Stars kushinda ama kupata sare kesho, kwa sababu hata mchezo wao uliopita dhidi ya DR Congo ilicheza vizuri na kama si bao la kujifunga la Clement Mzize, ingeweza kupata sare ugenini.

Lakini pia tunaamini benchi la ufundi chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Hemed Suleiman 'Morocco', litakuwa limeona panapovuja katika kikosi chao na kufahamu ubora na udhaifu wa wapinzani wao.

Kinachotakiwa kufanya sasa, kazi kubwa iliyobaki ni kwa wachezaji kuona umuhimu na thamani ya jezi ya taifa na kutambua wanawakilisha zaidi ya Watanzania milioni 60, hivyo waingie uwanjani kwa kazi moja ya kusaka ushindi.

Katika hilo pia, kwa kuwa mechi hiyo inachezwa nyumbani, kuna haja ya mashabiki kuitumia vyema nafasi ya kuwa mchezaji wa 12 kwa kujitokeza kwa wingi na kuujaza uwanja kesho.

Nipashe tunatamani kuona hatuishii kuujaza tu uwanja, bali wingi huo uende sambamba na kuishangilia Stars mwanzo mwisho bila kujali tumetanguliwa kufungwa ama la. 

Mashabiki watakavyoishangilia kwa nguvu timu yao, itawaongezea nguvu wachezaji na kujiona wanadeni la kuhakikisha ushindi unapatikana kwenye ardhi ya nyumbani ya Mama Samia Suluhu Hassan.

Hilo likifanyika vyema kama ambavyo hufanyika pale klabu zetu pendwa zinapokutana, tunaamini DR Congo wataziacha alama tatu.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Taifa Stars.