Baba Nyerere hata sasa tunathamini uliotuachia

By Jane Mathias , Nipashe
Published at 11:07 AM Oct 15 2024
Mwalimu Julius Nyerere
Picha: Mtandao
Mwalimu Julius Nyerere

TANZANIA imeadhimisha kumbukizi ya miaka 25 ya kifo cha mwasisi wake, Mwalimu Julius Nyerere kilichotokea Oktoba 14, 1997 nchini Uingereza , wakati akitibiwa saratani ya damu.

Kumbukizi hizo zilizofanyika jana mkoani Mwanza  zikiambatana na kuzima Mwenge wa Uhuru katika Uwanja wa CCM Kirumba, mgeni rasmi akiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa ujumla taifa linamkumbuka Nyerere kwa kuwa mwasisi wake tangu  kupigania uhuru kutoka kwa wakoloni wa Uingereza, hadi kuweka misingi ya kulitegemeza kiuchumi, kisiasa, kiuongozi na mifumo muhimu ya maendeleo inayoonekana leo.

Mifumo hiyo ni kama viwanda, umeme, maji, barabara na miundombinu ya reli, madaraja, majengo ya umma na hata taasisi kuanzia vyuo vikuu, sheria  na bunge.

Kuna  mambo mengi mazuri aliyolifanyia taifa na baadhi ya nchi za Afrika kupata uhuru kutoka kwa wakoloni, jamii inapaswa kuyaendeleza kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Yapo ambayo yanapaswa kumuenzi Mwalimu ikiwa ni pamoja na kuhifadhi mazingira. Itakumbukwa  wakati wa uhai wake alikuwa mstari wa mbele kupiga vita uharibifu wa mazingira ili kuepusha nchi na jangwa, ukame lakini ukiwezesha  kupata mvua za kutosha zinazoleta  maji ya kunywa na mifugo na kuendesha kilimo cha mazao ya chakula na biashara.

Kwa upande wa siasa, baadhi ya viongozi wanatakiwa kumuenzi kwa kujenga utamaduni wa kukubali kukosolewa pale ambapo mambo yanakwenda ndivyo sivyo.

Wanatakiwa kuendeleza umoja na kuacha ukabila, umimi, kugeuka miungu watu kwenye uongozi na kama alivyofanya, kung’atuka badala ya kuendelea kung’angania kubaki madarakani ili kujilindia heshima katika jamii.

 Viongozi wanatakiwa falsafa ya kujitegemea ili Tanzania ijenge uchumi imara kwa kutumia rasilimali za ndani kwenye kilimo, madini, mafuta na gesi ili kutimiza kauli mbiu ya kujitegemea  ambayo alikuwa akiitumia mara kwa mara kama njia ya kuwahimiza viongozi na wananchi ili kuondokana na umaskini.

Nyerere alitilia mkazo kilimo kwa sababu alibaini kuwa ni njia pekee kwa wananchi wengi ambao ni wakulima ya kuboresha maisha yao na  taifa kuondokana na njaa kwa kuzalisha chakula cha kutosha na ziada kwa ajili ya biashara.

Rais huyo wa kwanza wa Tanzania, kwa kutumia falsafa yake hiyo ya kilimo, aliwaagiza viongozi wa serikali na wananchi kushiriki, shabaha yake kuu ikiwa ni kuinua uchumi wa vijijini na kuboresha maisha ya wananchi.
 Katika maeneo hayo, aliwasisitiza wananchi kuishi na kufanya kazi kwa kushirikiana pamoja vijijini ili kuongeza uzalishaji katika kilimo kwa kushirikiana kwa rasilimali za ardhi, zana na nguvu kazi.
 
 Vilevile alianzisha vyama vya ushirika na ya kuwaunganisha wakulima ili kuwainua wakulima wadogo na kuimarisha uwezo wao kwa faida, kupata pembejeo kwa urahisi na kuinua hali zao kwenye mauzo ya kahawa, pamba, korosho na chai.

Kuhusu elimu, tunapaswa kumuenzi kwa kutilia mkazo kuwa kila mtoto awe wa maskini au tajiri anapata elimu sawa na mwingine kwa kuwa ni haki ya kila mmoja kwa manufaa yake na taifa zima.

Wiki  hii ni wakati wakumkumbuka Mwalimu na mambo mengi ambayo  alikuwa mstari wa mbele kuyatetea au kuyapiga vita kama rushwa na vitendo hivyo bado vinalalamikiwa kukithiri katika taasisi za serikali, hivyo kuwa chanzo cha kuwanyonya wananchi wanapohitaji kupata huduma.

Vitendo hivyo, vimekuwa vikilalamikiwa na wananchi wanyonge ambao wamekata tamaa kwa kukosa huduma muhimu  na maisha yao kuzidi kuwa duni.

 Kwa kumuenzi Nyerere wananchi kataeni kutoa rushwa na kuwafichua wanaojihusisha nayo kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo.