Majina ya mipaka vijiji, vitongoji ni muhimu uchaguzi huu S/mitaa

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:49 AM Oct 16 2024
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa.
Picha: Mtandao
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa.

UCHAGUZI wa serikali za mitaa unafanyika wiki ya mwisho ya mwezi ujao, ni Jumatano Novemba 27, ukihusisha vijiji 12,333, mitaa 4,269 pamoja na vitongoji 64,274.

Kabla ya kufanyika uchaguzi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa anatangaza rasmi majina ya mipaka ya mitaa, vijiji na vitongoji.
 
 Lakini  uzoefu unaonyesha kuwa kumekuwapo na  sintofahamu ya kutozingatia mipaka wakati wa kubandika majina ya wapigakura kwenye vituo vya kupigia kura katika maeneo mbalimbali.
 
 Kwa mfano, katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliopita, baadhi ya watu walikwenda katika vituo vya kupigia kura na kukuta majina yao hayapo, wakaambiwa si wa mtaa huo waliouendea, kwa sababu ya mipaka.
 
 Walipokwenda wa jirani wakaambiwa huko nako hawapo, kwamba huo si mtaa wao. Vilevile, wengine majina yao yalibandikwa kwenye vituo ambayo si vya  mitaa wanayoishi.
 
 Hivyo, wakati huu ambao serikali imetangaza mipaka, ingekuwa ni vyema suala la kubandika majina ya wapigakura nalo likazingatia mipaka hiyo ili kuwapunguzia usumbufu wananchi na kuona kama kuna figisu.
 
 Nadhani si vyema kama mtu anaishi mtaa A anafika kituoni anakosa jina lake,  anaambiwa akaangalie mtaa B ambako nako  halipo au hata kama lipo, atachagua viongozi ambao si wa mtaa wake na hakuwaazimia tangu mwanzo.
 
 Kwa hiyo ingekuwa ni vyema TAMISEMI ikahakikisha kero kama hiyo haitokei tena katika uchaguzi unaokuja ili kila mwenye sifa za kupigakura aweze kushiriki katika uchaguzi huo bila kikwazo.
 
 Sintofahamu hiyo imo ndani ya uwezo wa ofisi hiyo  hivyo, ijitahidi kuchapisha majina ya wapigakura kulingana na mipaka ya sasa, ili kila mmoja atambue eneo atakalokwenda kupigakura.
 
 Vinginevyo, yanaweza kujirudia yale ambayo yamewahi kujitokeza katika uchaguzi uliopita na kusababisha baadhi ya watu kukata tamaa baada ya kuhangika huku na kule kutafuta majina yao kwenye vituo.
 
 Serikali ijitahidi kuwafahamisha wananchi majina ya maeneo
 na mipaka itakayohusika kujiandikisha na upigaji wa kura, ili wajue maeneo yao. Kikubwa ni kuwa majina yasibandikwe vituo vingine.
 
 Lakini si vibaya wapigakura wakapewa elimu ya kutosha kuhusu mipaka ya maeneo yao kwani inawezekana wapo wasioijua ili siku ikifika wajue watakwenda kituo gani kupiga kura, lakini wakute majina yao.
 
 Inaweza kukatisha tamaa kama mtu anaishi mtaa A halafu anakwenda kwenye kituo chake anakuta jina halipo limebandika kituo cha mtaa mwingine. Mtindo huo unaweza kusababisha  usumbufu usio wa lazima.
  
 Mipaka ina umuhimu wake, kwani inaondoa mkanganyiko wa kijiografia ambao unaweza kujitokeza na kusababisha wapigakura kwenda vituo vingine badala ya kule wanakoishi.
 
 Kwa maana hiyo, wananchi kutambua mipaka ya maeneo yao ni jambo la msingi, lakini pia kubandikwa majina kwenye vituo ambavyo wanapigia kura ni jambo lingine muhimu ili wasisumbuke.
 
 Ikumbukwe kuwa kila unapofanyika uchaguzi wa serikali za mitaa, kuna kero ambayo wapigakura hukumbana nayo, ambayo ni kukosa majina yao katika vituo vya kupigia kura kutokana na mipaka mipya ya mitaa inayowekwa na serikali kila mwaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa.
 
 Mipaka huwekwa kulingana na jinsi mtaa unavyozidi kupanuka. Lakini tatizo huwa linajitokeza ni kukosekana kwa majina ya baadhi ya wapigakura katika vituo vyao kuchagua viongozi.
 
 Hivyo, yale ambayo yamekuwa yakijirudia kila mwaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa wakati wa kuweka mipaka, yangeishia mwaka 2019 ili mwaka huu kila kitu kiende sawa bila usumbufu.