Malalamiko uandikishaji Daftari la Kura, pagumu pasahihishwe

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 11:04 AM Oct 17 2024
Rais Samia Saluhu Hassan akijiandikisha kupiga kura.
Picha: Ikulu
Rais Samia Saluhu Hassan akijiandikisha kupiga kura.

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura ni mchakato muhimu ambao unaendelea kutekelezwa nchini kwa sasa, chini ya usimamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, hata hivyo malalamiko kadhaa yamesikika hasa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani.

Wamelalamikia utaratibu wa uandikishaji  wakidai kuwa wapo ambao wanaandikishwa kinyume  na mfumo rasmi, ikiwamo uandikishwaji wasiotimiza umri wa miaka 18, pia wamekaririwa wakivitaja baadhi ya vituo ambavyo wamedai kuwa ni hewa. 

Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, ambaye mwenye dhamana na jambo hilo amejitokeza na kuwataka wenye malalamikio wayawasilishe kwenye wizara hiyo na ushahidi ili hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika. 

Naamini kwamba licha ya Waziri Mchengerwa kutoa rai hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi nayo haiwezi kufumbia macho malalamiko hayo kwa kuwa yanaelekea kuichafua hivyo itatoa ushirikiano unaostahili ili kuweka bayana hali ilivyo. 

Kama kuna vielelezo vya malalamiko hayo ni vyema viwekwe wazi kwa kuwa hayaleti picha nzuri kwa wananchi, pia inasababisha wengine kuwa na hofu ya kwenda kujiandikisha. 

Ni wazi kuwa wakati ni mali sasa mtu afunge safari kwenda kujiandikisha kumbe amejiandikisha kwenye kituo hewa kama kweli kipo, mwingine akisikia ni wazi anavunjika moyo wa kwenda huko, hali hii itasababisha mchakato huo kudorora. 

Tume ya Taifa ya Uchaguzi, hutumia watendaji mbalimbali wakati wa Uandikishaji na Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura. Watendaji hawa ni pamoja na waratibu wa uchaguzi wa mkoa, maofisa waandikishaji, maofisa waandikishaji wasaidizi, waandishi wasaidizi na mwendesha kifaa cha bayometriki.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 17 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Mwaka 2024, Chama cha Siasa chenye usajili wa kudumu kinaweza kumteua mtu mmoja katika kila kituo cha uandikishaji kuwa wakala wa uandikishaji wa wapigakura.

Wajibu au majukumu ya wakala wa uandikishaji, kufuatilia zoezi la uboreshaji na kutazama kama linazingatia sheria, kanuni na maelekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kushirikiana na waandishi wasaidizi, kutambua wakazi wa eneo hilo na kutoa taarifa juu ya watu wasio na sifa.

Pamoja na majukumu tajwa, wakala wa uboreshaji hawaruhusiwi kuingilia shughuli za uendeshaji wa zoezi la uboreshaji. Msimamizi wa kituo ndiye mwenye mamlaka ya mwisho juu ya nani anastahili kuandikishwa au kuboresha taarifa zake kwa mujibu wa sheria, kufanya kampeni za kisiasa katika kituo cha uandikishaji kuorodhesha majina ya watu wanaojiandikisha.

Kwa mujibu wa Mwongozo wa Elimu ya Mpigakura Wakati Wa Uchaguzi Mkuu Wa Mwaka 2020, Daftari la Kudumu la Wapigakura limeanzishwa chini ya Ibara ya 5(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na Kifungu cha 12(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na Kifungu cha 15B(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292. 

Tangu kuanzishwa kwa Tume, Daftari la Kudumu la Wapigakura limetumika kwa mara ya kwanza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. Kwa mujibu wa Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na mambo mengine inawajibika:- (i) Kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapigakura wapya waliotimiza umri wa kuandikishwa; na (ii) Kusimamia na kuratibu Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura. 

Sifa za kuandikishwa kuwa mpigakura Kwa mujibu wa Ibara ya 5(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na Kifungu cha 10 (1) na (2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Kifungu cha 15(1) na (2) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, sifa za mtu kuandikishwa kuwa Mpiga Kura ni:- (i) Awe Raia wa Tanzania; (ii) Awe ametimiza umri wa miaka 18; na (iii) Awe hajapoteza sifa kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi au Sheria nyingine yoyote iliyotungwa na Bunge.

Nashauri ni vyema madai au malalamiko hayo yawe na ushahidi lakini kama hayana ushahidi wahusika watakaobainika kuzusha wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria kwa kuwa  ni wazi watakuwa na lengo baya  la kuhujumu mchakato. 

Maana pia kuna taarifa zinazoonyesha kuwa baadhi ya vyama vina ukata hivyo vimeshindwa kuweka mawakala wao kwenye vituo, kwa hiyo siyo vyema kuhujumu mchakato huu ambao ni mwelekeo wa kupata viongozi wa mitaa watakaosaidia katika kuongoza kutafuta uchumbuzi wa kero zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.