Utekelezaji mfumo mpya elimu una umuhimu mkubwa kwa sasa

Nipashe
Published at 10:56 AM Oct 17 2024
Mwalimu darasani.
Picha:Mtandao
Mwalimu darasani.

KWA miongo kadhaa, wadau wa elimu wamekuwa wakitoa maoni kwamba mfumo wa elimu ulioko nchini, hauendani na mazingira ya sasa ya sayansi na teknolojia pamoja na hali halisi ya maisha.

Sababu kubwa ambayo imekuwa ikitolewa ni kwamba mfumo huo umerithiwa kutoka ule wa kikoloni na kwa mazingira ya sasa haufanyi vijana wanaohitimu kuwa na maarifa mapana katika kukabiliana na changamoto za siku kwa siku katika maisha hasa kujitegemea. 

Licha ya kudaiwa kuwa mfumo huo umerithiwa kutoka kwa mkoloni, baadhi ya wadau hao wamekuwa wakisema mabadiliko ya sera na falsafa kutoka uchumi hadi uliokuwa chini ya Ujamaa na Kujitegemea kwenda uchumi wa soko katika muktadha wa soko huria na utandawazi, yameathiri kwa kiasi kikubwa sekta hiyo. 

Hoja kubwa wanayoitoa ni kwamba kuwapo kwa soko huru na kuruhusu sekta binafsi kuingia kwa nguvu zote katika sekta ya elimu, kumesababisha kuwapo kwa shule na vyuo vingi ambavyo falsafa yao ni kufaulisha watoto. Kwa maneno mengine, elimu imegeuzwa kuwa biashara, hivyo kinachozingatiwa hapo ni fedha na si ubora au kiwango cha elimu inayotolewa. 

Kuondolewa kwa elimu ya kujitegemea ambayo ilikuwa inawafanya vijana kujifunza pia stadi za maisha kama vile mapishi, kilimo, mifugo, useremala na uashi,  kunaelezwa kuwa ni moja ya sababu zilizofanya elimu  kupungua thamani yake. Vijana wengi wanaomaliza hata chuo kikuu, hawana maarifa wala uwezo wa kufanya mambo ya kuwawezesha kupambana na changamoto katika maisha. 

Aidha, sababu nyingine inayoelezwa kuwapo kwa hali hiyo ni mwanzoni mwa miaka ya 2000 wakati wa serikali ya awamu ya tatu. Katika kipindi hicho, alitokea Waziri ambaye kwa utashi wake aliamua kubadilisha mtaala uliofuta baadhi ya masomo yakiwamo ya sayansi na kilimo.  

Hatua ya kuwapo kwa utitiri wa shule na vyuo bila kuwekwa mifumo thabiti ya uthibiti, imetajwa kuwa sababu kwa kuwapo kwa hali iliyoko katika sekta ya elimu. Vijana wengi wanahitimu vyuo na kukosa ajira kwa sababu serikali na sekta binafsi hazina uwezo wa kuajiri idadi yote hiyo ambayo ni takriban wanafunzi 400,000 kwa mwaka. 

Kutokana na kuwapo kwa hali hiyo, serikali imeanzisha mtaala mpya ambao  umejumuisha stadi za maisha na kupokewa na wadau wengi kwamba utasaidia kuboresha elimu na kuwawezesha baadhi ya vijana kujiajiri badala ya kusubiri ajira kwenye kampuni na ofisi za umma na binafsi. Kupitia mtaala huo, vijana wanaomaliza hata elimu ya juu, watafunzwa maarifa ya namna ya kujiajiri badala ya kutegemea ajira. 

Katika baadhi ya nchi, kutokana na ukosefu wa nafasi za ajira, serikali zimechukua jukumu la kuhamasisha uanzishwaji wa stadi za maisha katika ngazi zote za elimu ili kuwawezesha vijana kubadilika kifikra kuwa anapomaliza masomo ajiajiri badala ya kuajiriwa. Kwenye nchi hizo kama vile Afrika Kusini, Nigeria, Ghana na Botswana, vijana wengi wanawezeshwa ndiyo maana kuna idadi kubwa ya mamilionea vijana wanaoibukia. 

Serikali, kutokana na umuhimu wa mtaala unaoangazia vijana kujitegemea baada ya kuhitimu masomo, ni vyema ikaanza utekelezaji huo mara moja ili kuondokana au kupunguza ombwe la ajira lililoko nchini kwa sasa. Jambo hilo ni muhimu kwa sababu litawezesha kutengenezwa kwa ajira nyingi kupitia makundi ya  vijana kujiajiri ambao nao wataajiri wengine, hivyo kupunguza tatizo la ajira.