Utekaji, mauaji watoto vilaaniwe

Nipashe
Published at 09:14 AM Jul 23 2024
Utekaji, mauaji watoto vilaaniwe.
Picha: Mtandao
Utekaji, mauaji watoto vilaaniwe.

KUMEJITOKEZA matukio mfululizo ya utekaji, watoto kupotea au kukutwa wameuawa na kufanyiwa ukatili wa aina mbalimbali.

Mfululizo wa matukio haya unaleta tafakari kubwa kwa wazazi na walezi.

Hali hii pia imewaibua wadau wapenda haki za watoto na kulaani vitendo vya kutekwa, kuibwa na mauaji ya watoto, wakitaka serikali ichukue hatua kupambana na matukio hayo.

Wadau hao kutoka jijini Dar es Salaam, wameamua pia kuomboleza na kuwaombea watoto walioripotiwa kutekwa na kuuawa nchini hivi karibuni.

Vitendo hivi vilivyoibuka siku za karibuni vinatafakarisha na kuleta wasiwasi kwa jamii kwa kuwa kila mara lazima zipatikane taarifa za kupotea kwa watoto huku wazazi wakihaha kuwatafuta.

Wadau wamefikia hatua ya kuliweka suala hilo mikononi mwa Mungu kwa kufanya ibada ya kuwaombea watoto hao na kuwasha mishumaa kama ishara ya kukumbuka watoto hao. 

Katika baadhi ya matukio yaliyowahi kutokea ni la Juni 3, mwaka huu, mkoani Kagera, ambapo mtoto Asimwe Novart, mwenye umri wa miaka miwili, alitekwa akiwa mikononi mwa mama yake na baadaye kukutwa amefariki dunia akiwa amenyofolewa baadhi ya viungo.

Julai 15, mkoani Dodoma, kuliripotiwa tukio la mtoto Sumaiya Issa, kutekwa na mpaka sasa hajapatikana; Julai 7, mwaka huu, huko Mbagala Dar es Salaam, mtoto Nusra Omari alikutwa ameuawa na baadhi ya viungo kunyofolewa; Julai 17 mkoani Dodoma, mtoto Theresphoa Mwakalinga alikutwa amefariki dunia na baadhi ya viungo vyake vimenyofolewa.

Mdau wa haki za watoto kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Getrude Dyabene, alisema anatambua jitihada zinazofanywa na serikali kulinda watoto, lakini wanasikitika kuona ukatili dhidi yao unaendelea.

Kwa mujibu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), vitendo hivyo si tu kinyume cha haki za binadamu, bali pia ni kinyume cha Katiba ya Tanzania na sheria za nchi.

“Jeshi la Polisi limekuwa likitolea taarifa matukio ya aina hiyo, hata hivyo haturidhishwi na mikakati iliyowekwa ya ufutiliaji ili kukomesha vitendo hivyo.

“Kwa hali ilivyo sasa tulitarajia Jeshi la Polisi lifuatilie kwa umakini zaidi kujua chanzo cha haya matukio na wahusika wakamatwe na kuchukuliwa hatua stahiki.” 

Wadau hao wamewasilisha hoja zao kwa serikali, na walimfikishia Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo mdau kutoka Shirika la Msichana Initiatives, Rebeca Gyumi, alimwomba Rais kama Amiri Jeshi Mkuu, aendelee kusisitiza ulinzi na usalama wa mtoto. 

“Taasisi zote zenye mamlaka ya ulinzi wa raia zitimize majukumu yake na kukamilisha kwa haraka uchunguzi wa kiini cha matukio haya na upelelezi kwa matukio yaliyotokea.”

Kutoka Mtandao wa Haki za Watoto, Msafiri Mwajuma, ameshauri Jeshi la Polisi kufuatilia kwa haraka na kuweka kipaumbele taarifa za watoto kupotea bila kusubiri kupita saa 24.

Katika kufanikisha hilo, wazazi, walezi, jamii, walimu kwa ujumla wametakiwa kuongeza ulinzi kwa watoto na kuwahamasisha kutembea katika makundi, kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi katika jamii na kuwaelimisha watoto wasikubali kuambatana na watu wasiowafahamu.

Hizi ni baadhi tu ya hatua zinazoweza kusaidia watoto kutokumbana na matatizo hayo.

Kwa pamoja suala hili likifanyiwa kazi hakuna kitakachoshindikana.