Ni wakati kwa waamuzi nao kujiweka fiti Ligi Kuu

Nipashe
Published at 10:20 AM Jul 22 2024
Ligi Kuu Tanzania Bara.
Picha: Mtandao
Ligi Kuu Tanzania Bara.

HIKI ni kipindi ambacho timu zote za Ligi Kuu Tanzania Bara zinafanya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano.

Kuna ambazo zimesafiri kwenda nje ya nchi, zingine zikitoka ndani ya mikoa yao na kwenda mikoa mingine, lengo likiwa ni lile lile kuandaa mazingira ambayo yanaweza kuwafanya makocha kufanya kazi zao kwa utulivu na ufanisi.

Ndicho kipindi ambacho wanafanya kazi kubwa kuviandaa vikosi vyao kuanzia utimamu wa mwili, pumzi, stamina, ufundi na mifumo, vitu vyote hivyo vinatarajia kutumika msimu mzima.

Nasema hivi kwa sababu najua kutokana na ratiba zilivyo, sidhani tena kama makocha wanaweza kupata muda huo tena, kwani kazi yao kubwa itakuwa tu ni kuikochi timu kwenda kucheza kulingana na jinsi mpinzani wao anavyocheza, kusafiri na kuweka miili sawa. Hawatopata tena muda mrefu wa kufundisha kama huu.

Kwa sasa wapo kwenye kazi ngumu wakihangaika kuziweka timu zao kwenye hali nzuri wakitegemea kupata matokeo mazuri uwanjani.

Tahadhari tunaipeleka kwa waamuzi kuwa makini mno kwenye maamuzi yao msimu ujao ili kila mmoja avune alichopanda na si vinginevyo.

Tumeshuhudia huko nyuma baadhi ya maamuzi yamekuwa wakiumiza makocha, wachezaji na mashabiki wa timu zao, hivyo kuonekana kama walichokifanya katika maandalizi kama haya ni kazi bure.

Baadhi ya waamuzi wamekuwa wakishindwa kutafsiri vema sheria 17 za soka kwa bahati mbaya au makusudi, hivyo kuzinyima pointi timu ambazo zilitakiwa kushinda, na kuzinufaisha zisizostahili kwa sare ama ushindi.

Matokeo yake baadhi ya makocha wamekuwa wakitimuliwa kazini wakati mwingine si kwamba uwezo wa kufundisha ni mdogo, bali kunyongwa na baadhi ya maamuzi ya waamuzi.

Msimu uliopita jumla ya makocha 18 walitimuliwa kwenye Ligi Kuu Bara kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kufanya vibaya, lakini ukiangalia wapo ambao waliathiriwa na maamuzi ya waamuzi.

Kwa bahati mbaya sana waamuzi wao husimamishwa kwa mechi kadhaa kabla ya kurudishwa baadaye, lakini makocha wakishatimuliwa inachukua muda mrefu kupata timu.

Tunajua kuwa msimu ujao kutakuwa na Video ya Kuwasaidia Waamuzi (VAR), kufanya maamuzi sahihi, lakini tunatambua kwamba si kila tukio ni lazima aende akaangalie, lakini pia wanaiongoza VAR ni watu, hivyo pamoja na kuwapo teknolojia hiyo, bado wanatakiwa kuwa makini na uchezeshaji, kwani kawaida kusikia hayo ni makosa ya kibinadamu.

Inaumiza na kukatisha tamaa makocha wanaotumia muda mrefu kuandaa timu, tena wengine wakitoka kabisa nje ya nchi au ya mikoa yao kwa ajili ya kukiweka fiti kwa muda mrefu wa wiki nne mpaka sita, lakini mwamuzi anatumia dakika 90 tu kuweza kumnyima ushindi kocha anayeonekana amemshinda mwenzake kwa mbinu.

Wakati makocha wapo kazini kwa sasa, tunataka waamuzi nao wawe mazoezini na kupata semina zaidi ili kuwa fiti kimwili jambo litakalowasaidia wasipitwe sana na matukio kutokana na kasi ya mpira, pia kuwa waadilifu na kuiacha mechi kujicheza yenyewe bila kulazimisha mambo.

Na hii itakuwa ni faida kwa soka la Tanzania kwani kuiacha timu iliyozidiwa mbinu ipoteze mechi kunaisaidia kwenda kusahihisha makosa ili warejee imara, lakini inapopewa ushindi au kubebwa na mwamuzi haiisaidii bali kuwadumaza viongozi, makocha na mashabiki wao kwa kuona wana timu nzuri, kumbe imesaidiwa kupata ushindi.