Hongera TFF, Bodi ya Ligi kukataa kupunguza wageni

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:15 AM Jul 20 2024
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Picha: Mtandao
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

WAKATI wa uzinduzi wa vifaa vya wasaidizi wa waamuzi vya njia ya picha za video maarufu kama 'VAR', hivi majuzi, pamoja na mambo mengine, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, aliweka wazi kuwa wachezaji wa kigeni wataendelea kuwepo kwa idadi ile ile ya 12 na hata kanuni ya watakaotumika kucheza uwanjani itabaki vile vile kama zamani.

Karia akasema kuwa kuwepo kwa idadi hiyo ya wachezaji wa kigeni kumezifanya timu za Tanzania kufanya vyema kwenye mechi ya kimataifa za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, hivyo kupunguza idadi ni kujirudisha nyuma, kwani miaka ya nyuma klabu za hapa nchini zilipokuwa zikitegemea zaidi wachezaji wa ndani hata kutinga hatua ya makundi tu ilikuwa 'mtihani'.

"Kwa takwimu tulizonazo wachezaji wa kigeni hawajafika hata 70 kati ya wachezaji 600 ambao huwa wanashiriki Ligi Kuu kila msimu, hivyo wachezaji wetu wanatakiwa na wao watoke nje ili wakapate changamoto mpya na kuongeza uwezo wao na siyo sisi kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni," alisema Rais Karia na kuongeza, 

"Tulipokuwa tukicheza na DR Congo na Zambia wachezaji wengi wa Tanzania walikuwa wa ligi ya ndani lakini walifanya vizuri sana kiasi cha kushangaza wengi, kwa sababu hawana tena ule woga wa kuogopa wachezaji wa kigeni, kila siku wanacheza na wachezaji hao hao ligi au wapo timu moja, hiyo imetusaidia sana kama taifa," alisema Karia.

Binafsi nampongeza sana Karia kwa kuliona hilo, na mara kwa mara wanaolitakia mema soka la Tanzania wamekuwa wakisisitiza kuendelea kuwapa nafasi wachezaji wa kigeni kuja nchini na kuendelea kulikuza soka la nchi na kuwakomaza wachezaji wetu.

Rais huyo alisema hayo kutokana na mapendelezo ya kanuni mpya ya Ligi Kuu msimu ujao, ambapo baadhi ya wadau walipendekeza kuwa wachezaji wa kigeni wapunguzwe kwa kile kinachodaiwa eti wanaziba nafasi za wachezaji wazawa.

Hii ni hoja mfu, kwa sababu kurudia alichosema Karia kuwa kuna wachezaji 70 tu kati ya 600, sasa ukifanya hesabu za kutoa hapo, bado wanabaki wachezaji wengi tu ambao wanaweza kuonyesha ubora wao na kuchaguliwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa.

Tatizo ni kwamba kuna baadhi ya watu wanadhani kuwa ili uchezee Stars ni lazima uwe Simba, Yanga au Azam, ambako huko ndiko kwa kiasi kikubwa wanasajili wachezaji 12 wa kigeni.

Klabu zingine zinasajili lakini hawafiki idadi hiyo, sasa wao wanadhani wale 12 wanazuia wazawa kupata namba na kuonekana. Lakini ukifanya uchunguzi mdogo tu, utagundua wachezaji wengi wa Stars wanatoka timu hizo hizo wanazoona zina wachezaji wengi wa kigeni yaani Simba, Yanga na Azam. 

Wale wale wachache tu wanaopata nafasi ndiyo tegemeo kwenye kikosi. Kwenye vikosi ambavyo wazawa wanajiachia, wapo kibao kwa idadi kubwa, bado hawapati nafasi ya kuchaguliwa timu ya taifa.

Ningekubaliana nao kama Simba, Yanga na Azam wasingekuwa na wachezaji Taifa Stars, halafu timu zingine ndizo zingetoa wachezaji wengi kwenye kikosi hicho, hapo tungesema wageni wanabana nafasi za wazawa. 

Hii inaonyesha kuwa kiwango cha mchezaji binafsi ndiyo kinatakiwa.

Mimi nadhani hili limekuwa likipigiwa chapuo na baadhi ya mameneja wa wachezaji wa Kibongo ambao wanaona kama wachezaji wao hawapati nafasi ya kucheza ili kuwaongezea thamani, kwa sababu ya kuwepo kwa wageni wengi.

Mimi nawaasa tu mameneja au madalali wa wachezaji, wawafunde wachezaji wao kuongeza bidii ya mazoezi, kujitambua ndani na nje ya uwanja pamoja na wao wenyewe kuwatafutia timu nje ya nchi, badala ya kutaka kung'ang'ania waendelee kuwepo hapa hapa na kutaka wageni wapunguzwe.