Adaiwa kumuua mpenzi wake kisha naye kutaka kujimaliza

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:02 AM Jul 27 2024
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro.

MFANYAKAZI wa kiwanda cha pombe kali cha Nguvu Banana Wine, Mussa Sasi (32), mkazi wa Goba Matosa, mkoani Dar es Salaam, anadaiwa kumuua mfanyakazi mwenzake, Lucy Haule (29), ambaye ni mpenzi wake na yeye kutaka kujiua.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro, alisema hayo jana kwamba tukio hilo lilitokea juzi asubuhi huko Goba.

Alisema Jeshi la Polisi lilipokea taarifa za kuwapo kwa mauaji hayo yaliyotokana na ugomvi kati ya wawili hao wanaodaiwa kuwa ni wapenzi.

Kamanda Muliro alisema baada ya polisi kufika eneo la tukio, walibaini kuwapo kwa mwili wa Lucy, mfanyakazi wa kiwanda hicho cha pombe.

“Uchunguzi wa awali umeonesha Lucy aliuwawa na mpenzi wake Musa anayefanya kazi ya kibarua katika kiwanda hicho,” alisema.

Muliro alisema mtuhumiwa huyo ambaye amekamatwa baada ya tukio hilo inadaiwa alijaribu kujiua kwa kutumia kisu kwa kujichoma eneo la shingoni.

Alisema hali ya mtuhumiwa huyo ni mbaya na kwamba amelazwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya  Mwananyamala, huku chanzo cha ugomvi wao kikiendelea kuchunguzwa.

Kamanda Muliro alitoa wito kwa wananchi wanapokuwa na migogoro au matatizo ya kijamii wazishirikishe taasisi mbalimbali za kisheria za kiserikali au binafsi ili kusaidia kutatua matatizo yao badala ya kujichukulia sheria mkononi.

Alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi wamekuwa wakifanya jitihada za kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na watu wazima.