THPS yawaunganisha wenye VVU zaidi ya elfu 4 na huduma ya tiba na matunzo

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 06:15 PM Jul 25 2024
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwenye banda la Shirila la THPS.
Picha: Marco Maduhu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwenye banda la Shirila la THPS.

SHIRIKA la THPS kupitia mradi wa AFYA HATUA kwa kushirikiana na serikali, wamewapima watu 211,763 na kubainika watu 4,077 kuwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi,na kisha kuwaunganisha na huduma za tiba na matunzo.

Takwimu hizo ni kuanzia Oktoba 2023 hadi Juni 2024, ambapo THPS wanatekeleza mradi huo wa AFYA HATUA kwa ufadhili wa mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR) kupitia kituo cha kidhitibi na kuzuia magonjwa cha Marekani (CDC).

Hayo yamebainisha leo Julai 25,2024 na Meneja Programu wa THPS Mkoa wa Shinyanga Dk.Amos Scott ambapo ameeleza kwenye zoezi la upimaji wananchi magonjwa bure (afya code clinic) lililoratibiwa na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa ufadhili wa Campun ya Jambo group linalofanyika viwanja vya michezo vya CCM Kambarage hadi julai 27.

Amesema mradi huo wa AFYA HATUA THPS wanautekeleza katika mikoa minne ambayo ni Tanga,Kigoma,Pwani pamoja na Shinyanga na wanatoa huduma za saratani ya mlango wa kizazi,matiti,tohara, na upimaji wa virusi vya ukimwi.

"Elimu ya maambukizi ya virusi vya ukimwi tunatoa mwaka wa tatu sasa na tuna vituo 92 vya tiba na matunzo kwa Mkoa wa Shinyanga chini ya mradi wa afya hatua,na watu ambao wanabainika kuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi wanapewa dawa za kufubaza makali na mpaka sasa watu  71,183 wanatumia dawa za ARV,"amesema Dk.Scott.

Aidha,amesema kwa upande wa saratani ya mlango wa shingo ya kizazi, kwamba Oktoba 2023 hadi Juni 2024 waliwafanyia uchunguzi wanawake 21,759,na 563 waligundulika kuwa na viashiria vya saratani hiyo huku 552 kati yao walipatiwa matibabu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, akiwa katika banda la THPS, amewapongeza wadau hao kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ya kuimarisha afya za wananchi pamoja na kuwapatia elimu ya kujikinga na maradhi mbalimbali.

Ametoa wito kwa wananchi kwamba waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa ukimwi sababu bado upo, pamoja na kupata tohara,na wale ambao wanagundulika kuwa na virusi vya ukimwi,wafuate masharti ikiwamo na matumizi sahihi ya dawa ya kufubaza makali ili waishi miaka mingi.

Pia,amewasisitiza waendelee kupima afya zao mara kwa mara,pamoja na kufuata ushauri wa watalaamu wa afya na kulinda afya zao.