Afia kwenye gari baada ya kuwasha jiko la mkaa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:42 AM Jul 27 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Kamishna Msaidizi (ACP) Mahamoud Banga.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Kamishna Msaidizi (ACP) Mahamoud Banga.

DEREVA Thadei Mbawala (48), mkazi wa Mtaa wa Mjimwema, Halmashauri ya Mji Njombe, mkoani hapa, amefariki dunia ndani ya gari baada ya kuwasha mkaa ili kuota moto na kupitiwa na usingizi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Kamishna Msaidizi (ACP) Mahamoud Banga, alithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo juzi majira ya saa moja asubuhi ambapo pembeni ya mwili huo kulikutwa jiko la mkaa lililowashwa.

Alisema dereva huyo alikuwa kwenye gari lenye namba za usajili T 983 BZZ aina ya Fuso, mali ya kampuni ya maji ya Kitulo.

“Chanzo cha tukio hili ni dereva huyo Julai 24, mwaka huu, usiku kuingia kwenye gari akiwa na jiko la mkaa na wakati anachaji simu yake alipitiwa na usingizi na kufariki dunia kwa sababu ya kuvuta hewa ya sumu ya mkaa.

“Natoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Njombe kuacha tabia ya kutumia majiko ya mkaa wakiwa wamejifungia ndani kwa kuwa ni hatari kwa afya zao,” alionya Kamanda Banga.

Mke wa marehemu, Catherine Haule, aliliambia Nipashe kuwa mume wake baada ya kurejea kazini usiku, alimuaga anakwenda kuchaji redio katika gari lakini hadi saa 12 asubuhi alikutwa amejifungia humo.

“Hapa ndani kulikuwa na kigae (jiko) ambalo alikuwa akiota moto mara kwa mara ambapo mtoto wake alikuwa anapenda kumkolezea.

“Nikajua lipo kumbe mwenzangu alikichukuwa na kwenda nacho kwenye gari na alichukuwa pia, shuka la watoto akaenda nalo,” alisema.

Catherine alisema polisi walipofika walimkuta ndani ya gari hilo na mwili ukiwa umefunikwa na blanketi.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mjimwema, Theophil Mwinuka, alisema ni kawaida kwa dereva huyo kwenda kuchaji simu kwenye gari.

Baadhi ya wakazi wa kata ya Mjimwema akiwamo, Nolbert Mkalawa, alisema walipata taarifa majira ya moja asubuhi kuhusu dereva huyo tangu aingie kwenye gari hilo hajatoka na milango limefungwa.