Yatengenezwe mazingira ya kuvutia mashabiki viwanjani

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:23 AM Jul 22 2024
Mashabiki wa soka.
Picga: Mtandao
Mashabiki wa soka.

LICHA ya kwamba mashabiki wengi nchini kwa sasa wanapenda soka, lakini bado kuna tatizo kubwa la kuingia viwanjani.

Msimu uliomalizika, Yanga iliongoza kwa kuingiza mashabiki wengi viwanjani, kwa mujibu wa takwimu za Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB), ikiingiza mashabiki 141,911, ikifuatiwa kwa karibu na Simba ambayo iliingiza mashabiki 112,717.

Ukiifanyia tathmini ya kina idadi hii na jinsi mashabiki wa soka nchini wanavyopenda mchezo huo ni ndogo sana.

Ukitaka kujua hilo, hebu angalia mechi za Matamasha ya Simba Day na Wiki ya Mwananchi ambapo Uwanja wa Benjamin Mkapa hufurika mashabiki wengi ambapo pungufu yake inakuwa ni 50,000, lakini kiwango cha juu kinakuwa ni 60,000 kwa mechi moja tu.

Kimahesabu inaonyesha matamasha hayo mawili ya timu hizo kubwa moja tu ni wastani wa idadi ya watazamaji wa timu zao msimu mzima.

Hii inaonyesha kuwa bado wahudhuriaji mpirani ni wachache sana, japo kuna mwanga tofauti kwa miaka ya nyuma.

Siku hizi unaweza kuona hata kinamama, kinadada na watoto uwanjani, tofauti na zamani ambapo ni zaidi ya asilimia 95 wanakuwa ni wanaume tu.

Kwa ligi ya Tanzania ambayo imevutia wachezaji wengi kutoka nje ya nchi, wenye uwezo mkubwa, huku ikiwa nafasi ya sita kwenye ubora wa Afrika, bado ni mashabiki wachache sana.

Ukitaka kujua hilo ni jinsi wanavyojazana hotelini, kwenye mabaa, majumbani na vibanda umiza kufuatia mechi za soka zinapokuwa zinaonyeshwa kwenye televisheni.

Hata hivyo, kutokana na upenzi wa mpira wa miguu ulivyo kwa sasa, kama juhudi za makusudi zikifanywa, wanaweza kupatikana mashabiki wengi sana kwenye viwanja vya soka, achilia mbali wanaotazama kwenye luninga.

Ilitakiwa baada ya msimu uliopita kumalizika ligi, wadau wangetafuta sababu zinazofanya mashabiki wasipende kwenda viwanjani, japo wanapenda soka.

Wangepata sababu zingefanyiwa kazi kuelekea msimu mpya. Hata hivyo, kwa uchunguzi wangu mdogo nimegundua tatizo hakuna mazingira mazuri yanayowashawishi kwenda viwanjani.

Wenzetu wameshatoka kufanya uwanjani kama polisi au mahakamani ambako unatakiwa kukaa kwa nidhamu iliyopitiliza, badala yake ni burudani kwa kwenda mbele.

Katika viwanja vyetu, mtu akifika uwanjani kwanza kabisa anakutana na mbwa aliyefungwa kwenye mlango wa kuingilia. Milango yenyewe ni michache kiasi cha kuwa na msongamano mkubwa kabla ya kufika ndani, mpaka akiingia yupo hoi.

Hakuna vitafunwa, juisi, vichangamsha mdomo ambavyo vitauzwa kwa bei iliyozoeleka. Hakuna vinywaji vya kuchangamsha mwili. Hakuna anayeruhusiwa kuingia na chupa ya maji, hivyo mtu kukaa muda mrefu bila huduma hiyo, na hata hayo yanayouzwa ndani kwenye glasi nyepesi yanauzwa ghali sana.

Wenzetu viwanja vyao vina migahawa, na mabaa, ambapo yanawezesha mashabiki kuingia mapema, wanakunywa, wanakula, na inakuwa kama mtoko wa familia kiasi hata mtu ambaye si mpenzi sana wa soka anaweza kwenda kwa ajili tu ya mazingira na mahitaji yanayopatikana uwanjani ambayo yanapatikana pia kwenye mabaa na migawaha mingine.

Nadhani wenye mamlaka wakianza kuvitengeneza viwanja kuwa kama sehemu ya mtoko wa kifamilia, ndipo vitaanza kuvutia watu kujazana viwanjani.

Kuwe ni vivutio na viwezeshi vingine zaidi ya mpira kama vyakula, maji, juisi, vitafunwa, mishkaki, supu, tena maeneo yote na si kwa ajili ya wale wa VIP pekee, vikiuzwa kwa bei ya kawaida tu ya kumwezesha shabiki yeyote kuweza kununua. Hapo tutakuwa tumepiga hatua kubwa ya kushawishi watu kwenda viwanjani.