Serikali ije na chanzo, ufumbuzi wa kudumu moto kwenye masoko

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:41 AM Jul 19 2024
Moto masoko.

KWA miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la masoko kuungua nchini. Imekuwa ikitokea kila mara na kusababisha madhara na hasara kubwa kwa wafanyabiashara na wateja wao.

Ufunguaji wa masoko haya umeendelea kulitesa taifa, kwani masoko yote mashuhuri nchini yameshapitia kadhia hii, likiwamo Soko Kuu la Kariakoo, Dar es Salama.

 Kila madhara haya yakitokea timu ya uchunguzi huundwa ili kubaini tatizo na mara nyingi kinachobainika mara nyingi kinafanana kwa kiasi kikubwa, tofauti yake ni mazingira tu. 

Mara nyingi chanzo huo ni mshumaa, mama lishe kusahau alichokiacha kwenye jiko la mkaa, kama supu, maharage, au vingine vinavyofanana na hivyo.

 Kingine ni shoti ya umeme, hivyo vyote vinatajwa kuwa ni vyanzo vya moto kwenye masoko mbalimbali nchini. 

Cha kushukuru ni kwamba huwa hakuna vifo wakati wa masoko yakiungua, na sababu kubwa mara nyingi huungua usiku kipindi ambacho hakuna watu, wafanyabiashara wameshafunga biashara zao.

 Kwa sasa hatujui ni wapi tena kunafuata, kwa sababu matukio hayo wamekuwa mengi kiasi kwamba kama vile hata wananchi wameshaanza kuyazoea. 

Ambao wanahuzunishwa ni wale waliopata hasara, hasa wafanyabiashara, wateja wao, ndugu jamaa, marafiki, na hata watu wa eneo hilo, lakini wengi wameonekana kama kuyazoea. 

Ndiyo maana hata soko likiungua, mtu akiangalia kwenye mtandao wake wa kijamii, au akisikia kwenye vyombo vya habari, anaona kama vile huenda ni marudio ya masoko yalioungua huko nyuma, na si mapya. 

Ifike wakati sasa litafutwe suluhisho la kudumu kuhusu kuungua kwa masoko kwa sababu kunasababisha athari kubwa, ikiwamo kuwarudisha watu kwenye umasikini, na serikali inakosa kodi. 

Kuna watu wameshanunua bidhaa, pesa yote wameshaiweka kwenye mzigo, wana madeni ya mikopo sehemu mbalimbali, lakini moto unakuja na kuwatia umasikini ndani ya dakika 20 tu.

 Tume zimeundwa na kuundwa, lakini bado halijawa suluhisho. Sana sana zinakuja kujulisha umma tu chanzo chake ni nini.

 Mimi nadhani imefikia wakati wateuliwe wataalam, ambao watafanya kazi ya kufanya uchunguzi yakinifu ya sababu kuu ya masoko mengi kushika moto. 

Na kwa nini huwa hayaungui mchana wakati wa jua kali, badala yake usiku, hasa wa manane? Hawa waende mbali zaidi na kutafuta suluhisho la kufanya ili matukio haya wasijirudie tena. Itakuwa haina maana kujua chanzo tu, halafu tahadhari haichukuliwi. 

Ni sawa na mtu anayeumwa malaria, anakwenda hospitali kupima, akiambiwa ugonjwa anaoumwa, basi anaondoka bila kupata dawa, yaani yeye alichokuwa akitaka ni kufahamu tu anaumwa nini. 

Huyu malaria itamuua.
 Kama ni kubadilisha nyaya za umeme, basi zibadilishwe kwenye masoko yote, kama ni mama lishe, basi waambie supu au maharage yao wapikie majumbani, au nje ya soko, na waingie ndani wakiwa tayari vyakula vya vimeshaiva. Kama kuna kingine ambacho kitagundulika kuna ni sababu utengenezwe mpango mkakati wa kuondoa vyanzo vyote vinavyosababisha au viashiria vyake. 

Nadhani hapa ndipo masoko yetu yatapoanza kuwa salama, lakini tuacha tu tume ziwe na kazi tu ya kutaja chanzo halafu imeisha, wafanyabiashara wetu wataendelea kulia kila kukicha na serikali kushindwa kupata mapato yake kwenye kodi na hata Halmashauri kukusanya ushuru.