Dawa za pumu, fangasi zatumika kujichubua

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 07:53 AM Jul 27 2024
Dawa za pumu, fangasi zatumika kujichubua.
Picxha: Mtandao
Dawa za pumu, fangasi zatumika kujichubua.

DAWA za pumu ya ngozi na fangasi zinatumiwa na baadhi ya watu kujichubua ngozi, mamlaka za serikali zimeonya ni hatari kiafya.

Mamlaka hizo pia zimeeleza kukabiliwa na changamoto katika kudhibiti uuzwaji, usafirishaji na uingiaji dawa kiholela na vipodozi haramu nchini kutokana na biashara hiyo kufanywa kinyemela.

Ofisa Udhibiti Ubora katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Athumani Kissumo, anasema vipodozi vina tafsiri yake kama ilivyo katika Sheria ya Viwango iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 baada ya baadhi ya majukumu ya Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TMDA) kuhamishiwa TBS.

Anasema vipodozi vyenye madhara vilivyopigwa marufuku nchini, vimeendelea kuingizwa, kuuzwa na kutumiwa kinyume na sheria kutokana na kuingizwa kwa njia za panya kama vile bandari bubu na magari ya malori ya mafuta kutumika kuvisafirisha.

"Kipodozi ni kitu chochote kinachotumiwa kupaka, kujipulizia, kujifukiza na kujimiminia kwenye mwili kwa lengo la kujipamba, kujisafisha na kubadili mwonekano na bila kuathiri mwonekano wa asili.

"Vipodozi havikisudii kutibu magonjwa wala kubadilisha maumbile ya mwili. Lengo la kipodozi ni kujiremba na kusihusishwe na kubadili maumbile au kuzuia magonjwa, hii ndio dhana kisheria,," anasema Kissumo.

Anasema vipodozi hivyo huwa na viwango kulingana na mtumiaji atakavyo na kwamba vipodozi ambavyo vinalenga kutibu au kubadili maumbile vinabadili tafsiri ya kipodozi na kuwa dawa.

"Shirika linahakikisha vipodozi vinadhibitiwa, viwango kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa, kikanda na mashirika mengine.

"Lakini, utakuta tu kipodozi tayari kipo sokoni. Hivi karibuni tulisikia kuna gari lilipita la mafuta ila ndani yake vimebebwa vipodozi," anasema.

Meneja Ukaguzi na Udhibiti wa Dawa kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), Emmanuel Alphonce anasema mtu akipata athari kutokana na matumizi ya kipodozi, hushirikiana na TBS kubaini aina ya bidhaa hiyo sokoni.

"Tukibaini tatizo huwa tunasimamisha matumizi na tunatoa taarifa kwenye vyombo vya habari kuufahamisha umma. Athari nyingi katika dawa ni ambazo zimeainishwa kisayansi kwamba ukitumia dawa hii utapata usumbufu fulani.

"Elimu kwa umma ni muhimu, wapo wanaotumia dawa za pumu ya ngozi na fangasi ili kung’arisha ngozi," alisema Alphonce. 

Ofisa Viwango Mwandamizi TBS, Alexander Mashalla anasema utaratibu wa kupokea malalamiko kuhusu bidhaa zilizowaathiri watumiaji huwasilishwa kwa njia tofauti, ili hatua zichukuliwe.

Ofisa Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Glory David, anasema uzito uliokithiri huwaathiri watu walio na mafuta mengi mwilini kulinganishwa na umri, jinsi na kimo.

"Pamoja na matumizi na dawa za kupunguza uzito, kuna vitu vya kuzingatia kwa ushauri wa daktari na mtindo wa maisha. Unaweza ukapunguza uzito kwa dawa kwa njia ya dawa hizo ila baadaye ukarudia hali ya awali," anahadharisha Glory.

Daktari wa binadamu, Fredrick Mashili, anasema vipodozi ni bidhaa zinazochangia kubadili ngozi na kuwa nyeupe zikiwa na 'steroids' na kuifanyia ngozi kuwa nyeupe, ndizo zinashika kasi na kuharibu mfumo wa homoni mwilini.

"Mtu anapoanza kutumia vipodozi hivi anasababisha mwili wake ushindwe kutengeneza homoni.  Steroids ni homoni ambazo zinahusika kuweka uwiano wa mwili wake usiongezeke sana.

"Na wanawake kwa kiasi kikubwa hupasuka ngozi, hii hutokana na matumizi haramu ya steroids," anaonya.

Mkuu wa Kitivo cha Famasia Chuo Kikuu cha Kimataifa Kampala (KIU), Prof. Wilbroad Kalala, anasema katika utafiti waliofanya kuhusu vipodozi hadi hatua ya ngozi kung’aa, walibaini, steroids zilizomo katika vipodozi hivyo ni viambata vinavyofanya ngozi kuwa nyembamba na kuhatarisha afya.

"Dhana zilizopo katika jamii ni kwamba mwanamke mweupe ndio mrembo, zimefanya wanawake baadhi kuanza kutumia vipodozi ambavyo vina athari katika uzazi," anaonya Prof. Kalala.

Anaongeza: "Mtu anayetumia kipodozi hatarishi, akipata ajali ni ngumu kumshona kwa sababu vipodozi hivi huingilia ‘melanin’ ya ngozi isifanye kazi kiasili."