Rais amtwisha zigo Ridhiwani PSSSF, NSSF

By Restuta James , Nipashe
Published at 07:37 AM Jul 27 2024
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Ridhiwani Jakaya Kikwete kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ikulu jijini Dar es Salaam jana.

RAIS Samia Suluhu Hassan, jana aliwaapisha vviongozi aliowateua hivi karibuni huku na kuwatwisha majukumu mazito huku akimtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, kusimamia vizuri mifuko ya hifadhi ya jamii iwe endelevu na isifilisike.

Aidha, amewataka wateule hao kuheshimu viapo na kuwakumbusha kuwa  madaraka waliyopewa ni nguo ya kuazima ambayo wanaweza kuvuliwa wakati wowote iwapo  hawatatimiza wajibu wao kikamilifu.

Rais Samia alitoa maelekezo hayo Ikulu, Dar es Salaam alipokuwa akiwaapisha mawaziri wawili, Naibu Mawaziri na Makatibu Tawala wa Mikoa miwili.

“Ridhiwani nenda kaisimamie iendeshwe kisayansi ina fedha za watu siyo za serikali. Ni za wafanyakazi ambao wanaweka akiba yao ya baadaye. Nenda kasimamie na uhakikishe inakuwa endelevu na haiendi kupotea au kufilisika. 

“Simamia miradi inayotekelezwa na mifuko hii. Kuna fedha nyingi imeingizwa kwenye miradi na haifanyi vizuri. Anayetoka atakunong’oneza,” alisema na kumtaka pia afanye uratibu wa ajira za vijana na kuhakikisha sekta zote zinatengeneza ajira kwa kundi hilo na kulinda maslahi yao.

Kwa Waziri wa Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Jerry Silaa, alisema vyombo vya habari na sekta hiyo ni muhimu kwa nchi. Alimtaka ahakikishe uhuru wa habari unakuwapo na kuonya kuwa hakuna uhuru usio na mipaka.

“Unakwenda kuiongoza wizara inayosimamia falsafa ya 4R kuhakikisha uhuru wa habari unakuwapo. Hakuna uhuru usio na mipaka. Nenda kashirikiane na wadau wa sekta ya habari,” alisema.

Rais Samia pia alimtaka kuhakikisha wananchi wengi wanaunganishwa na mawasiliano ya simu ili kukuza uchumi wa dijitali.

“Ifikapo Desemba mwaka huu, mifumo ya serikali iwe inasomana. Taarifa inayosomeka sekta moja isomeke sekta nyingine kwa zile zinazoingiliana. Nenda kalisimie hilo,” alisema.

Kuhusu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alimwelekeza Waziri Deogratias Ndejembi kuendeleza kazi zilizofanywa na Silaa hasa utatuzi wa migogoro na kutekeleza mradi wa upimaji wa vijiji.

Akitoa maelekezo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Naibu wake, Costo Chumi, aliwataka kufanya kazi kwa ushirikiano ili kulinda taswira ya nchi kimataifa.

 “Taswira ya nchi yetu iko kwenye wizara yako au kwako (Mahmoud). Zana za wizara ukifika pale utakabidhiwa. Nimekuwekea wasaidizi wawili. Upo kwenye mlango, macho na masikio ya serikali. Pana kazi nyingi sana pale.

 “Kila mtu ana majukumui yake. Waziri, Naibu na Katibu Mkuu. Hakuna ndani ya wizara mtu mmoja anaweza kuyajua yeye peke yake, lazima mshirikiane. Nimeisema sana wizara yenu kwa sababu ndiyo jicho, masikio na ndiyo mlango wa mahusiano ya nchi kimataifa,” alisema.

Kwenye Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, aliwataka mawaziri wasimamie haki, nidhamu na uwajibikaji wa watumishi wa umma.

Pia aliwataka Makatibu Tawala wa Mikoa kusimamia fedha za umma kuondoa kero za wananchi na kuhakikisha zile zitakazopelekwa kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa, mwaka huu zinasimamiwa na kuleta tija inayotakiwa.

KUHESHIMU VIAPO

“Mmekula kiapo hapa mbele ya mamlaka iliyowateua na mbele ya wananchi mnaokwenda kuwatumikia. Kiapo chenu kina maana kubwa. Kila mtu alishika kitabu anachokiamini inamaana ulikuwa unaongea na Mungu. Mungu amewashuhudia, mamlaka imewashuhudia na wananchi wamewashuhudia. Kila mtu aende akijitafakari kiapo alichokula, kuwa mwaminifu kwa kiapo alichokula,” alisema.

Aliwataka kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akikumbusha Ibara ya 8(a), inasema wananchi ndio msingi wa mamlaka yote ya serikali.

“Taifa kwanza yenu baadaye. Wale mliozoea kutumia nafasi zenu kujinufaisha au kujinyanyua, badala ya kunyanyua taifa, kama upo kwenye madaraka rekebisha kabla sijakuona. Na ninyi mnaoingia tambueni hivyo.

“Madaraka ni dhamana, inataka kufanyiwa kazi. Kila mmoja awajibikie kwa maneno, matendo na kauli njema. Waswahili wanasema ni nguo ya kuazima. Niwakumbushe haisitiri mambo, saa yoyote inaweza ikakuvuka,” alisisitiza.

Awali, Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, aliwakumbusha viongozi hao kwamba hakuna nafasi isiyozibika.

“Rais amewaapisha viongozi hao siku chache baaya ya kutengua uteuzi wa  Mawaziri, January Makamba, aliyekuwa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Naibu wake, Stephen Byabato, Nape Nnauye aliyekuwa Wizara ya Habari, Sayansi na Teknolojia ya Habari, na kujiuzulu ubunge na unaibu waziri, Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk, aliyekuwa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,” alisema.