Zinahitajika zaidi shule za umma za Kiingereza

By Joyce Lameck , Nipashe
Published at 09:18 AM Jul 23 2024
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.
Picha: Mtandao
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.

MPANGO wa kuanzisha shule za umma za Kiingereza hivi karibuni katika baadhi ya miji na majiji, unashika kasi.

Lakini kazi hiyo inapingwa na   wadau mbalimbali wa elimu wanaoona kuwa huenda ukawa mwanzo wa kutengeneza matabaka kwenye elimu unaofanywa na serikali yenyewe.

Itakumbukwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, anatangaza mpango wa serikali wa kuanzisha shule zake zinazofundisha Kiingereza, unaolenga kuwapa wazazi machaguo wanayoweza kuyamudu katika kuamua hatima ya elimu ya watoto wao.

Aidha, anaeleza kuwa mpango huo unakuja na lengo la kuboresha ufundishaji wa Kiingereza, kwa sababu wamebaini kuna udhaifu mkubwa kwa wanafunzi kwenye kutumia lugha hiyo, baada ya kumaliza elimu ya msingi na kuendelea na sekondari.

Inavyoonekana ni kwamba kuwa na shule za mchepuo wa Kiingereza ni kutengeneza matabaka kwenye elimu ya umma, kwani serikali tangu uhuru imekuwa ikifundisha shule zake kuanzia darasa la awali hadi kidato cha sita sasa kwa Kiswahili.

Aidha, inatoa elimu kwa kutumia sera ya serikali kugharamia elimu bila wazazi kuchangia ada wala kutoa fedha kusomesha watoto wao mijini na vijijini.

Hata hivyo, kwenye shule hizi za serikali za Kiingereza, wazazi wamekuwa wakitakiwa kuchangia au kulipa Shilingi 400,000 ambacho hulipwa kila mwaka, kwa ajili ya kukidhi gharama za uendeshaji wa shule hizo.

Ikumbukwe serikali imeandaa utaratibu ambao inasema hautaleta usumbufu wa kulipa ada, pia kuathiri mzazi yeyote ambaye yupo karibu na shule hiyo na hakuna shule nyingine ya serikali ya Kiswahili, kwani atakubaliwa kumpeleka mtoto wake hapo.

Vile vile hata kama atamhamisha mtoto kwenye shule ya Kiswahili, hatalazimishwa kulipa ada katika shule zote za umma, zinazofundisha masomo yote kwa Kiswahili, katika ngazi ya msingi huku Kiingereza kikifundishwa kama somo na kuanzia ngazi ya sekondari na kuendelea.

Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya elimu, matarajio ya mfumo huo yalikuwa kwamba miaka saba ya kufundishwa Kiingereza katika ngazi ya msingi, ni maandailzi ya kumfanya mwanafunzi aweze kufundishika na kuelewa masomo mengine katika lugha hiyo, atakapofika sekondari na vyuoni.

Hata hivyo, takwimu zinaonyesha kwamba matarajio ya kuelewa Kingereza katika miaka ya awali hayafikiwi, katika kipindi cha walau miaka mitano iliyopita, takwimu za Baraza la Mitihani ya Taifa la Tanzania (NECTA) zinaonyesha kwamba zaidi ya wanafunzi wanaomaliza mitihani ya shule ya msingi huwa hawafaulu somo la Kingereza.

Hata katika matokeo ya mtihani wa ngazi ya Diploma ya Ualimu mara nyingi ufaulu huwa ni wa kuanzia kiwango cha daraja C kushuka chini, kwa mujibu wa takwimu tofauti zinazotolewa na wasomi na watafiti katika sekta ya elimu  nchini.

Kama zaidi ya wanafunzi wanaoingia sekondari huwa hawajui Kiingereza, hii inaonesha kuwa wanakwenda kufundishwa masomo ambayo watapata taabu kuyaelewa, huu ndiyo msingi hoja ya wanaotaka lugha iwe Kiswahili kwa sababu ndiyo ambayo wanafunzi wanaielewa itumike sekondari.

Wanaotaka Kiingereza kipewe nafasi zaidi wanafanya hivyo, kwa hoja kwamba ndiyo lugha yenye maarifa na taarifa zaidi duniani kwa sasa, pia kuifahamu kunampa mwanafunzi wigo mpana zaidi wa kufanikiwa katika maisha yake ya sasa na badaye ikiwamo kupata fursa mpaka nje ya nchi.

Wanaoamini katika shule hizo wanasema zitasaidia wanafunzi kuingia kwenye ushindani wa elimu kimataifa, hivyo wanafunzi watapata fursa kutokana na kujifunza na kutumia Kiingereza.

Wanaopinga ujio wa shule za umma, wana haki ya maoni yao lakini ukweli ni kwamba muda au wakati ni sasa Watanzania kuungana na wadau wa elimu, ambao wameliona suala hili litaleta mabadiliko katika mfumo wa elimu nchini.

Kwa kutumia Kiingereza kufundisha kwenye masomo yote, kuanzia shule za awali, msingi, sekondari hadi  watakapofikia hatua ya vyuo vikuu ni wazi itawapa ari, nguvu na uwezo kujiamini katika kuitumia lugha hiyo na kuinuka kimaisha.