TFF angalieni kwa jicho la pili tabia hizi za vilabu vyetu nchini

Nipashe
Published at 07:29 AM Jul 27 2024
Shirikisho la Soka Nchini (TFF) .
Picha: Mtandao
Shirikisho la Soka Nchini (TFF) .

HAKUNA ubishi, kwa sasa ligi yetu ni miongoni mwa ligi bora Afrika na huenda ikawa ligi namba moja kwa ubora katika ukanda wa Afrika mashariki na kati.

Ubora wa ligi yetu unatokana na makampuni na wadau kuwekeza fedha nyingi katika udhamini na hata baadhi ya wafanyabiashara kufanya uwekezaji kwenye baadhi ya klabu zetu.

Hii imepelekea hata baadhi ya klabu zetu kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa hususani mashindano yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika, CAF.

Hayo yote yamepelekea kwa sasa wachezaji wengi kutoka sehemu mbalimbali kutamani kuja kucheza hapa nchini tofauti na miaka ya nyuma ambapo ligi pendwa zilikuwa kwenye baadhi ya nchi kama Afrika Kusini, Misri, Morocco na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hata hivyo kipo kitu kinachotia doa uzuri na ubora wa ligi yetu kinachofanywa na baadhi ya klabu zetu.

Kwa sasa taarifa za klabu kufungiwa kusajili kwa sababu ya kuvunja mkataba wa mchezaji au kocha kimakosa ni jambo la kawaida hapa nchini.

Shirikisho letu la soka linapaswa kutupia jicho katika suala hili, linatia doa soka letu kuona kila wakati klabu zinafungiwa kwa makosa yale yale ya kila siku.

TFF kama msimamizi wa soka hapa nchini, ichukue hatua ya kutoa elimu kwa watendaji wakuu wa klabu na viongozi namna ya kuheshimu mikataba wanayoingia na wachezaji au makocha.

Lakini pia watoe elimu namna ya kuvunja mkataba pale inapobidi kufanyika hivyo ili kukwepa rungu la FIFA la kufungia fungia klabu zetu na kutia dosari soka letu.

Ndani ya kipindi kifupi tumeshuhudia taarifa ya TFF kuelezea maamuzi ya FIFA kufungia baadhi ya klabu kwa kushindwa kumlipa mchezaji au kocha baada ya kuvunja mkataba.

Taarifa ya karibuni imetoka jana ambapo klabu ya Singida Fountain Gate imefungiwa na FIFA kufanya usajili mpaka itakapomlipa aliyekuwa kocha wake, Thabo Senong raia wa Afrika Kusini.

Sababu ya kufungiwa kwao ni kutokana na kuvunja mkataba kinyume cha taratibu huku akiwa hajalipwa mishahara yake kwa miezi kadhaa mpaka kupelekea kufungua kesi FIFA.

Lakini si Singida tu peke yao waliokutana na rungu hilo la FIFA, tumesikia kuhusu mabingwa wa soka nchini, Yanga kuwa na kesi tofauti na kufungiwa, lakini pia ipo klabu ya Tabora United na nyinginezo ambazo zimekumbana na rungu hili. 

Klabu zetu na hata wachezaji wa klabu hizo ni lazima waheshimu mikataba wanayoingia.

Kwa sasa hakuna ujanja ujanja kwenye mikataba, FIFA wapo wazi kwenye sheria na taratibu zao hasa upande mmoja unapovunja mkataba na upande mwingine bila makubaliano ya pande mbili.

Na kama kuna ulazima wa kuvunja mkataba , basi pande zote zikae mezani kujadiliana na kukubaliana kabla yakufikia hatua hiyo, hii itasaidia kuondoa mashtaka kama haya huko FIFA.

Ligi yetu ilipofikia hapa ni juhudi za wadau wote, vilabu, Shirikisho lenyewe na wadhamini mbalimbali, ni vizuri kuilinda hatua hii ili nchi yetu izidi kufanya vizuri katika soka.

Tunaweza kuepuka fungia fungia hizi za FIFA kama pande zote zitaheshimu mikataba wanaoyoingia na kuitekeleza kikamilifu.